Alhamdulillah, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametunyooshea tawfiq Yake kwa kumaliza tarjuma na tafsiri ya kitabu hiki muhimu kuhusu historia ya Dola Kuu ya Wauthmaniya.
Ni hishma na adhama kubwa kwangu kwa mara nyingine kuuletea Ulimwengu wa Kiswahili historia hii iliyotukuka juu ya kuchomoza, kustawi, kudhoofika na kuanguka kwa Dola hii iliyotawala mabara matatu kwa muda wa miaka 623.
Kitabu hiki chenye kurasa 778 ni tafsiri ya kitabu maridhawa cha: Al-Uthmaniyyuun, rijaaluhum al-idhaam wa muassasaatuhum al-Shaamikhah kutoka kwa mwalimu wetu Sheikh Uthman Nuri Topbash kutoka Uskudar, Istanbul.
Wakati wa kutafsiri kitabu hiki cha 35 katika mfululizo wa tarjuma zangu za vitabu na cha 39 katika vitabu vyangu vyote, ilinilazimu kuchukua mtindo maalumu wa maisha, khususan maisha ya kimaanawi ya mhandisi mkuu wa Dola hii, Sinan Pasha au Mimar Sinan aliyeupa ulimwengu tunu za kiuhandisi zisizomithilika ambazo ziliakisi uhandisi maridhawa wa Kiislamu katika majengo na miradi yake. Mfumo wa Mimar Sinan Pasha wakati wa ujenzi wa “Sulaymaniyah Jami”, moja katika uhandisi bora kabisa aliowahi kuufanya, ulitiririsha nguvu na ithibati katika moyo wangu, khususan tukio la kutoweka kwake kwa kipindi cha mwaka mzima na kuzusha wasiwasi juu ya himma na azma yake kuu ya kukamilisha ndoto muhimu sana ya Sultan Sulayman Al-Qaanuuni.
Ujasiri na uthubutu wa Sultani Muhammad Al-Faatih aliyeifungua Konstantinopoli katika umri mdogo kabisa na kuthibtisha Bisharah ya Mtukufu Mtume (s.a.w) juu ya ufunguzi wa mji huo muhimu kwa Wabezanti, ilikuwa kioevu cha hamasa na nguvu wakati wa kufanya tarjuma hii.
Himma ya Sultani Salem I aliyeliongoza jeshi kubwa na kutembea umbali wa kilometa 2500 akivuka milima, mabonde na misitu mpaka alipokutana na Dola ya Safawiya, ambayo ilikuwa miongoni mwa madola makubwa wakati huo, akaishinda; himma yake katika kampeni yake ya kijeshi dhidi ya Misri, ambapo alivuka jangwa lenye kuogofya la Sinai, ambalo wakati huo ilikuwa ikiaminika kuwa hakuna anayeweza kulivuka, na ambapo mpaka leo hakuna aliyeweza kutoa tafsiri ya uvukaji huo ulivyokuwa kwa nyenzo za kimaada, ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa nguzo ya ujasiri katika kampeni yangu ya kutafsiri kitabu hiki.
Kupitia kwake, historia iliandika kwenye kurasa zake za dhahabu wasifu wa mtawala adhimu asiye kifani. Katika umri wake wote, hakuwahi kupungukiwa na umahiri au kushindwa. Kwani alikuwa akitaka msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kila jambo na kuamini kuwa kwa kufanya hivyo jambo hilo litapata ufumbuzi.
Jangwa la Sinai wakati wa mchana huwa kama moto wa Jahannam, na wakati wa usiku hugeuka kuwa mithili ya mji wenye baridi kali. Lakini Sultani Salem alilivuka ndani ya siku 13 bila kupoteza askari hata mmoja, huku Napoleon aliyekuja miaka 300 baadaye akishindwa kulivuka jangwa hilo na askari wake kuuana wao kwa wao. Hata katika Vita Kuu ya Dunia, baada ya kuvumbuliwa kwa zana na ufundi wa hali ya juu, askari wa vita hiyo walilivuka jangwa hilo ndani ya siku 11.
Beti za ushairi wa Yunus Emre zilikuwa kama ala tamu katika moyo wangu na kunipa hamasa na saadah kuu. Hakika, kilichomfanya Yunus kuwa Yunus kimekuwa na taathira kwangu.
Ushupavu na ushujaa wa Khayrud-Din Barbarossa Pasha aliyeigeuza Bahari ya Mediterania kuwa mithili ya ‘Ziwa la Wauthmaniya’ na kuwaadabisha wazungu katika vita vya Baharini, ilikuwa kama karamu ya moyo kwangu. Hakika, Khayrud-Din Barbarossa ni tunu ya historia hii iliyotukuka.
Nakumbuka mzee wangu mmoja nilipomsimulia kuhusu khabari ya Barbarossa Pasha jina hili liliendelea kutoa mwangwi katika akili yake.
Miongozo ya kimaanawi ya wahandisi na masultani wa kiroho wa Dola hii kama vile Sheikh Adibali, Aziz Mahmud Hudayi na Mawlana Khalid Al-Baghdadi ilitoa mwanga adhimu kila nilipozifunua kurasa za kitabu hiki na kunifanya niamke mapema nikiwa na himma kubwa ya kuikamilisha kwa wakati. Alhamdulillah, baada ya wiki 4 za juhudi na himma kubwa, kazi hii iliyokuwa na kurasa 656 ilikamilika.
Hakika ni mengi ninayoweza kuyasema kuhusu kitabu hiki, lakini ni imani yangu kuwa wachapishaji wake, Darul-Arqam, watakuwa na hamasa ya kuwapatia wazungumzaji wa Kiswahili duniani chakula hiki maridhawa chenye virutubisho adhimu.
Shukrani zangu za dhati kwa wale wote walionitia moyo wa hamasa, bila kumsahau mhariri wangu mahiri, Ali Hassan Kingu ambaye aliupitia kwa umakini muswada wa kitabu hiki muhimu.
Panapo majaaliwa, hivi karibuni nitaandika hapa mukhtasari wa anguko la Dola hii adhimu wakati tukisubiri wachapishaji watuletee meza hiyo ya karamu.
Na kwa kuwa “hadhi ya akili ya mtu huonekana katika aathari zake, basi: HIZO NI AATHARI ZETU, BAADA YETU ZITAZAMENI AATHARI HIZO”.
Wabillah tawfiq.