Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Thursday, July 12, 2012

jinsi ya kuipata taqwa katika ramadhani

Maana ya Taqwaa daima huambatana na ibaadah katika Qur-aan, 'Ibaadah maana yake ni kufanya yale Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyotuamrisha na kuepukana na yale Aliyotukataza. 'Ibaadah pia inamaanisha vitendo vyote ambavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anapenda na kukubali kama ni matendo ya moyo, ulimi, au maungo. Kwa hiyo Taqwaa inaambatana na kufanya yaliyokuwa sawa na yasiyokuwa sawa. Taqwaa ni tunda la kufanya vitendo vya 'Ibaadah. Kwa maneno mengine, ikiwa mmoja atafanya Allaah aloamrisha, na kukaa mbali na aliyoyakataza, itakuwa kapata Taqwaa. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kataja katika kitabu Chake:

{{Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm, kama walivyoandikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu.}} Al-Baqarah 2:183

Katika Aayah hii na nyingi nyengine, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuonyesha kuwa Taqwaa ni matokeo au matunda ya kufanya vitendo vyema vya 'Ibaadah.


Maana ya Taqwaa

Baada ya kuwa tushafafanua jinsi gani ya kupata Taqwaa, tutaainisha nini maana ya mada ya Taqwaa. Taqwaa maana yake: ni kusafisha moyo au nafsi. Jambo hili limethibitika katika baadhi ya Aayah katika Surat Ash-Shams ambapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kasema:

{{Naapa kwa jua na mwangaza wake. Na kwa mwezi unapolifuatia. Na kwa mchana unapolidhihirisha. Na kwa usiku unapolifunika. Na kwa mbingu na kwa aliyeijenga. Na kwa ardhi na kwa aliyeitandaza. Na kwa nafsi na kwa aliyeitengeneza. Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake, Hakika amefanikiwa aliyeitakasa,Na hakika amekhasiri aliyeiviza.}} Ash-Shams 91:1-10

Allaah (Subhanahu wa Ta'ala) Kaanza katika Surah hii kwa kuapa viapo saba. Popote Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anapoanza Surah kwa kuapa, Yeye (Subhaanahu wa Ta'ala) Hufanya hivyo kwa kutuonyesha chochote kitachofuatia baada ya hapo ni muhimu sana kwetu kukifahamu na kukifuata. Kwa hivyo, tuwe makini sana kwa kinachosemwa, na tuwaze maana yake. Kusafisha mmoja moyo wake na kusafisha nafsi, mmoja lazima atekeleze vitendo vyema ambavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anapenda sisi tufanye, na angamizo huwepo katika kufanya vitendo ambavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katukataza. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni Muongozi na Mlindaji wa Nafsi, tunahitajika kufanya kila kitendo chema kwa kutegemea rehma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kuogopa adhabu Zake, kuwa na imani dhabiti na kumuamini.
 

Usafishaji wa Nafsi


Miongoni mwa ujumbe wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kamtuma na amri ya kuzisafisha nafsi za Waislamu hususan, na binaadam wote kwa ujumla. Allaah (Subhanahu wa Ta'ala) Kasema:

{{Yeye Ndiye Aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, awasomee Aya Zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, japokuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri.}} Al-Jumu'ah 62:2


Katika Aayah hii tunapata mambo matatu muhimu,

1. Kufundisha Qur-aan,

2. Kufundisha Sunnah,

3. Kuonyesha njia ya kujisafisha nafsi.


Usafi huu unapatikana kwa kufanya matendo ya 'Ibaadah na kujiepusha na madhambi na maasi.


Kanuni za kupata Taqwaa

Jinsi gani mtu anaweza kujua kuwa vitendo vyake vya 'Ibaadah vitamsaidia kupata Taqwaa? Kukuza Taqwaa, mtu lazima atimize kanuni zifuatazo:


1) Ikhlaas, niyyah ya dhati kuwa vitendo vinavyofanywa ni kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Pekee, kwa mapenzi naye, ambapo wakati huo huo unategemea malipo na rehma Zake, pamoja na kuogopa ghadhabu na adhabu Zake.

2) Kufanya vitendo kwa kadiri ya Sunnah sahihi inavyosema. Kuwa na elimu ya lazima ya 'Ibaadah inayotekelezwa. Kujua jinsi gani Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kafanya vitendo hivyo na wakati muwafaqa wa kufanywa vitendo hivyo.

Ikhlaas, ni lazima iwepo wakati ule wa kabla kitendo kinapofanywa na baada ya kufanya kitendo hicho, bila ya riyaa au sum'ah (kufanya mambo kwa kujionyesha au kutaka kujulikana na watu). Kwa mfano, baada ya kufanya kitendo chema, mmoja asiseme kwa wengine, "Angalia mema yote ninayofanya", au "Mimi hasa ni mtu bora kwa sababu nafanya hichi na kile."


Ukiufuata mfumo huu wa kisayansi wa kuipata Taqwaa, na kuhakikisha unatekeleza masharti yake na haki zake, basi bila shka yoyote utaipata hiyo Taqwaa inshaAllaah.

fadhila za mwezi wa ramadhani

Ama kwa hakika katika mwezi wa Ramadhaan kuna fadhila nyingi ambazo mimi nitazitaja kwa uchache namuomba Allaah Aniwafiqishe 'asaa yawe na manufaa katika Duniya na Akhera Insha-Allaahu  Aamiyn.
 
1)     NI MWEZI WA QUR-AAN: 
Kama Alivyosema  Mwenyeezi Mungu Mtukufu katika kitabu Chake:
"Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi ambao imeteremshwa Qur-aan ili iwe uongozi kwa watu na hoja na upambanuzi (Baina ya haki na batil)”Qur-aan 2:185
Na imekua makusudio yake  ni kuteremshwa Qur-aan kutoka katika Lawhum-Mahfuudh ilaa samaai dduniya (Kutoka Lawhim-Mahfuudh mpaka mbingu ya kwanza). 
Vilevile kama ilivyopokewa na Ibn 'Abbaas (radhiya Allaahu 'anhu) kuwa  makusudiyo yake   kwa hakika kuteremshiwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Qur-aan mwanzo ni katika mwezi wa Ramadhaan na vilevile Qur-aan mwanzo wa kuteremka ni usiku wa Laylatul-Qadir na Laylatul-Qadir iko katika mwezi wa Ramadhaan.
Hivyo basi ni juu yetu kufanya juhudi katika mwezi huu kukithirisha sana kusoma Qur-aan.  Walikua Salafus-Swaalih (Wema Waliotangulia) wakikilinda kitabu cha Allaah kwa kukisoma na kuyafanyia kazi yaliyokuwemo kwa mazingatiyo. Pia Tunaambiwa kuwa Sayyidnaa Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akimfundisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Qur-aan katika mwezi wa Ramadhaan, na alikuwa 'Uthmaan bin 'Afaan (Radhiya Allaahu 'anhu)  kila siku akisoma Qur-aan yote yaani anakhitimisha mara moja kwa siku,  kwa maana,  msahafu mzima anausoma kwa siku moja. Na walikuwa baadhi yao katika wema wakisoma Qur-aan yote kwa siku tatu, wengine kwa wiki moja na wengine kwa siku kumi. Walikuwa wakisoma Qur-aan ndani ya Swalah na nje ya Swalah.
Mwenyeezi Mungu Atuwafiqishe mimi na wewe tuisome Qur-aan na kwa mazingatiyo khasa katika mwezi huu tufanye juhudi sana ili tuweze kupata fadhila za mwezi huu mtukufu.
 
2)     NI MWEZI WA SUBIRA:
Subira ni katika jambo gumu na halipati ila kwa mtu mcha Mungu na mnyenyekevu kwa Allaah. Na katika kufunga kunatakiwa subira pale mtu anapojizuilia kutokana na kutokula, kunywa, matamanio na mengineyo. na imekua Swawm ni nusu ya subira na subira malipo yake ni pepo kama alivyosema Mwenyeezi Mungu Mtukufu:
"Kwa hakika (Mwenyeezi Mungu) Atawapa wenye kusubiri malipo bila ya hisabu"Qur-aan 39:10:
 
3) MILANGO YA MOTO INAFUNGWA, MILANGO YA PEPO INAFUNGULIWA NA MASHETANI WANAFUNGWA:
Kama ilivyokuja katika Hadiyth iliyopokelewa na Maimamu wawili:
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema, "Pindi inapokuja Ramadhaan inafunguliwa milango ya pepo, na hufungwa milango ya moto, na mashetani wanafungwa kwa Minyororo" (imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim)
Kwa hakika utaona katika mwezi huu watu wengi wanajitahidi kujiepusha na maasi, watu wanajaa misikitini kwa kufanya ibada ya mwezi huu hii ni kwa sababu mashetani wamefungwa na shetani juu ya uasi wake lakini anauogopa mwezi wa Ramadhaan na vitimbi vyake vinakuwa dhaifu ndio mana wengi nyoyo zinabadilika wanaswali  na kujitahidi kufanya kheri.  Lakini ikimalizika Ramadhaan tu basi Swalah imekwisha kama vile Allaah yupo Ramadhaan tu. Huu ni msiba ndugu zangu Waislamu Allaah Asitujaalie katika hao.
 
4)     LAYLATUL QADR:
Katika mwezi huu kuna siku ya Laylatul-Qadr siku ambayo ni bora kuliko miezi elfu kama  Alivyosema Mwenyeezi Mungu:
"Huo ni usiku wa hishima ni bora kuliko miezi elfu.
 Huteremka Malaika na roho (za viumbe watakatifu) katika (usiku) huo  
  kwa idhini ya Mola kwa kila jambo.
 Ni amani (usiku) huo mpaka mapambazuko ya alfajiri"
Qur-aan 97:3-5
Imehisabiwa mtu atakapofanya ibada katika usiku huo mmoja ni kama amefanya ibada sawa na miaka 83 na hii ni katika fadhila kubwa kabisa. Na katika kitabu Muwatwaa, Imamu Maalik  amesema.
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ameona umri wa umma za mwanzo ni mrefu, na umri wa ummah wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul-Qadr uwe ni bora kuliko miezi elfu.
(Muwatwaa1/321 (Muhammad Fuad 'Abdul-Baaqy)
Hakuna siku tukufu na kubwa kama siku hii ni wajibu kwetu kuutafuta usiku huu katika kumi la mwisho kufanya ibada ili tupate fadhila hizo.  Ninamuomba Allaah atuwezeshe kwa hilo, AAMIYN.
 
5)     DU'AA NI ZENYE KUKUBALIWA:
Katika hadiyth iliyopokewa na Imaam Ahmad:
Kutoka kwa Jaabir (radhiya Allaahu 'anhu) kwa isnadi iliyo nzuri
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Amesema: "Kila Muislam du'aa zake ni zenye kukubaliwa atapomuomba katika mwezi wa Ramadhaan"
Na imepokewa katika Hadiyth kuwa du'aa ya mwenye kufunga pia ni yenye kukubaliwa. Basi mtu ajipinde katika kumuelekea Allaah kumuomba mambo ya kheri ya dunia na akhera aombe pepo ya Jannaatul Firdaus na alete maombi mengine Insha Allaah Mwenyeezi Mungu Atayapokea maombi yetu, AAMIYN.
 
La mwisho ambalo nitakua nimekamilisha maudhui yangu:
 
6) MWEZI HUU NI MWEZI WA KUTOA:
Na alikua Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akizidisha kheri nyingi katika mwezi wa Ramadhaan.
Imepokewa na At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu 'anhu) Kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) "Bora ya (wakati wa) kutoa sadaqa ni kutoa katika mwezi wa Ramadhaan"
Na imepokewa na Zayd bin Aslam kutoka kwa babake, amesema nimemsikia 'Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu 'anhu) anasema, "Ametuamrisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) tutoe sadaqa nikatoa mali yangu nikasema leo nimemtangulia Abu Bakr nimekwenda na nusu ya mali, akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kuniambia, "Umewabakishia nini watu wako?" Nikasema, nusu kama hii, na akaja Abu Bakr na kila mali yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuuliza, "Umewabakishia nini watu wako?Akasema, nimewabakishia Mwenyeezi Mungu na Mtume wake. Nikasema huyu Abu Bakr hapitiki na kitu chochote abadan"
Kuonyesha wema waliotangulia walikua wakishindana katika kheri lakini tofauti kubwa katika zama zetu hizi watu wanashindana katika mambo ya kidunia na kujifakharisha nayo. 
Tunamuomba Allaah Atuonyeshe mema tuyafuate na mabaya tuyawache na tushindane katika kila kheri ili tuwe ni wenye kufuzu na kupata daraja ya juu ya Pepo.

Njia 10 Za Kuukaribisha Vizuri Mwezi Wa Ramadhaan

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:


((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ)) (( أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ وَأَن تَصُومُواْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ))  ((شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلاَ يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ  وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ  وَلَعَلَّكُمْ  تَشْكُرُونَ))  

((Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa Swawm, kama waliyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah))(([Mfunge] siku maalumu za kuhisabika. Na atakayekuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine. Na wale wasioweza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakayefanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua))  ((Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi. Basi atakayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Allaah Anakutakieni yaliyo mepesi wala Hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Allaah  kwa kuwa Amekuongoeni ili mpate kushukuru)) [Al-Baqarah: 183-185]

Inatupasa tumshukuru Allaah سبحانه وتعالى kwa Kutujaalia uhai na afya mpaka tunakaribia kufika mwezi mtuku wa Ramadhaan na hii ni fursa nyingine Anayotupa katika maisha yetu kushuhudia mwezi huu na kupata fadhila zake.  
Na hii ni neema ya Allaah سبحانه وتعالى  Ambaye Ametujaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au siku bora au masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu zake za mema yanayotendeka humo huwa ni zaidi ya nyakati nyingine. Mfano wake ni kama kunapokuwa na mauzo yaliyopunguzwa bei dukani (sale), ambayo kawaida yake huwekwa kwa muda mdogo tu maalum.  Na muda huu mtu huweza kununua vitu vingi kwa malipo kidogo tu. Hali kadhalika Ramadhaan, ni mwezi mmoja tu, lakini malipo yake huwa ni mengi kuliko hata malipo ya miezi yote mingine.  Ikiwa mtu atatimiza Swawm yake inavyopaswa na kufanya mema mengi, na akawa katika Twa'a (utiifu) kamili na kuomba maghfira, basi hutoka katika mwezi huu akiwa ameghufuriwa madhambi yake.
Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :
  (( من صام رمضان إيماناً واحتساباً ، غفر له ما تقدم من ذنبه )) أخرجه البخاري ومسلم  
((Atakayefunga Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]  
Ramadhaan ni mwezi ambao tunatimiza Fardhi mojawapo ya Kiislamu. Ni mwezi uliojaa baraka, kheri na Rahma za Allaah سبحانه وتعالى. Kila Muislamu inampasa aukaribishe mwezi huu kwa furaha na matumaini kamili.
Zifuatazo ni njia kumi za kujitayarisha kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan na kupata manufaa makubwa pindi utakapotimiza:
1.    Du'aa
Anza kwa kuomba Du'aa kwamba mwezi huu ukufikie wakati umo katika hali ya siha nzuri na usalama hata uweze kufunga na kufanya ibada zako kwa hamu kubwa na wepesi.  

2.      Mazoezi katika mwezi wa Sha'abaan  
Funga Sunnah nyingi katika mwezi wa Sha'abaan, soma Qur-aan Juzuu moja kila siku au chini yake, amka usiku uswali japo Raka'ah mbili, kisha zidisha kidogo kidogo hadi inapoingia Ramadhaan uwe tayari umeshapata mazoezi mazuri.
3.      Shukurani   
Mshukuru Allaah سبحانه وتعالى  Kukupa uhai na siha hata uifikie Ramadhaan nyingine.  Imaam An-Nawawy alisema, kwamba shukurani inapasa kwa kila jambo jema unalojaaliwa kubwa au dogo na vile vile shukurani inapasa kwa kila jambo baya Analokuepusha nalo Allaah سبحانه وتعالى.  Kwa hivyo fanya 'Sajdatush-Shukr' [Sajda ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)] kwa neema hii tukufu.  
4.      Furaha   
Furahia kukufikia mwezi wa Ramadhaan kama unavyomfurahikia mgeni mpenzi anapokuja kwako na kumuandalia mazuri yote.  Maswahaba رضي الله عنهم, walikuwa wakiamkiana unapoingia mwezi wa Ramadhaan na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisema hivi anapowapa habari nzuri za mwezi wa Ramadhaan:
((جاءكم شهر مبارك افترض عليكم صيامه تفتح فيه أبواب الجنة وتغلق فيه أبواب  الجحيم وتغل فيه الشياطين  فيه ليلة خير من ألف شهر من حرم خيرها فقد حرم)) رواه أحمد  
((Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, ni mwezi wa Baraka.  Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi alfu.  Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa [yote ya kheri] )) [Ahmad]
5.      Jipangie wakati na weka maazimio
Ni jambo la kusikitisha kuona watu wengi wanafurahia kuingia mwezi wa Ramadhaan kwa kujiandaa kupanga mambo ya kidunia badala ya mambo ya Akhera.  Wengi hukimbilia kwenda sokoni kununua nguo za 'Iyd, na kufurahikia vipindi vya Ramadhaan katika televisheni ambavyo sio vya dini kama 'misalsal' (maonyesho ya sinema yanayoendelea [series]), na pia kuanza kukusanya video za filamu, mipira, na mambo ya kupotezea muda usiku wa Ramadhaan. Pia wengine kunua karata, dhumna, meza ya mchezo wa keram kwa maandalizi ya vipumbazo na vipoteza muda katika mchana wa Ramadhaan ili wasiihisi Swawm au kuupeleka muda haraka kama wanavyoamini wao. Badala ya kufanya maandalizi ya kununua misahafu ya ziada, kanda za mawaidha, Qur-aan, kukusanya video za mawaidha na mafunzo mbalimbali ya Dini, vitabu vya Dini kwa lugha wanayoifahamu kwa wepesi na kadhalika.
Huu ni mwezi wa kufanya ibada na fursa ya kujichumia mema mengi yamfaayo mtu Akhera. Kwa hiyo ndugu Waislamu, tujitahidi kuutumia wakati wetu wote bila ya kupoteza hata dakika moja, na muhimu sana kujipangia mapema wakati wako kama ifuatavyo:
  • Ni bora kujipangia nyakati zote za mwezi mzima vipi utatumia muda wako wa mchana na usiku. Weka maazimio ya dhati kuchukua fursa kamili ya wakati wote wa mwezi huu.
  • Weka mpango maalum wa kazi zako hata uweze kuswali kwa wakati kila kipindi, kusoma Qur-aan, kula daku na mengineyo kama tutakavyotaja hapa chini.
  • Kama ni mwanafunzi na kama unakuwa ukisoma usiku, lala mapema, kisha uamke uswali Qiyaamul-Llayl na usome masomo yako baada ya hapo.

  • Anza mpango wako kwa siku chache na kama unahitaji kurekebisha kuboresha nidhaam yako fanya hivyo uweze kujua nidhaam ipi itakayowafikiana na hali yako.

Nasaha kwa kina Mama na kina Dada:
  • Fanyeni maandalizi mapema ya kununua vyakula vya mwezi wa Ramadhaan na kuviandaa vyenye kuandalika mapema kabla Ramadhaan haijaanza, kama vile; sambusa, madonge ya chapati, maji ya matunda n.k. na kuweka kwenye mashine ya kugandisha barafu (freezer) au jokofu ili ikifika Ramadhaan muwe na kazi chache za jikoni na muweze kupata nafasi kubwa ya kushughulika na Ibaadah mbalimbali kama kusoma Qur-aan, kusikiliza mawaidha na hata kuhudhuria Darsa za Dini.
  
6.     Tawbah na Maghfirah      
Omba Tawbatun-Nasuuha kwa Mola wako na waombe msamaha wale uliowakosea. Kufanya hivi kutanufaisha zaidi Swawm na Swalah zako na  pia kukupa imani kuwa huna haki ya mtu.
7.      Jifunze Fiqhi ya Swawm
Jifunze elimu ya mambo yanayohusu Swawm (Fiqhi ya funga), hiyo ni muhimu ili usije kufanya jambo la kuharibu Swawm yako.  Jifunze Swawm kama aliyokuwa akifunga Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  ndio mfano bora kabisa wa kuufuata.
Swawm haifunguliwi kwa kula na kunywa tu, bali pia ni kujiepusha na maneno mabaya na kufanya mambo mabaya kama kusengenya, kutukana, kugombana. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  amesema:
 ((من لم يدع قول الزور والعمل به والجهل فليس لله حاجة في أن يدع  طعامه وشرابه)) البخاري   
((Yeyote asiyeacha kusema maneno mabaya? Na vitendo vibaya basi hana haja kuacha chakula chake na maji)) [Al-Bukhaariy]
8.      Jitayarishe kuchuma mema mengi  
Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa ukarimu, huruma, rahma na mapenzi.
·        Panga kabisa na kuweka kiwango fulani cha kutoa Sadaka na kutoa kwa maskini, anzia kwanza kwa ndugu na jamaa.
·        Kama inakupasa kutoa Zakah, na umependa iwe katika mwezi wa Ramadhaan fanya hima uitimize Fardhi hii pia.
·        Weka 'azma ya kufuturisha kwa kualika ndugu, jamaa, jirani na marafiki kwani kumfuturisha mtu ni thawabu.
                                
((قال صلى الله عليه وسلم :  من فطر صائماً كان له مثل أجره غير أنه لا ينقص من  أجر الصائم شيء)) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألباني
((Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم "Atakayemfutarisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy na kasahihisha Imaam Al-Albaaniy]
·        Kama unaye jirani asiye Muislamu, mjulishe kuhusu Ramadhaan, faida na Fadhila zake. Hii ni njia na fursa mojawapo ya kufanya da'awah kwa jirani yako.
9.      Hitimisha Qur-aan, Hifadhi na jifunzeTarjama 
Jipangie wakati uweze kuhitimisha Qur-aan kwani Ramadhaan ndio mwezi ulioteremshwa Qur-aan na hii ni Sunnah aliyokuwa akifanya Jibriyl عليه السلام   kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kusoma naye Qur-aan yote
((عن ابن عباس رضي الله عنهما قال: "كان رسول الله صلى الله عليه وسلم أجود الناس، وكان أجود ما يكون في رمضان حين يلقاه جبريل، وكان يلقاه في كل ليلة من رمضان فيدارسه القرآن؛   ((رواه البخاري
((Kutoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kwamba: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, lakini alikuwa mbora  zaidi katika Ramadhaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan))  [Al-Bukhaariy]
Hadiyth hii inatufundisha yafuatayo:
  • Kusoma Qur-aan katika Ramadhaan;
  • Kukutana kwa ajili hiyo;
  • Kupima hifdh yako ya Qur-aan kwa kukaa na Mwalimu au mwenye elimu nzuri ya Qur-aan kwa kukusikiliza au kukufundisha;
  • Kuongeza juhudi za kusoma Qur-aan zaidi katika mwezi wa Ramadhaan:
Katika muda wa masaa 24 weka saa moja au mbili khaswa iwe ya Qur-aan kusoma na kujifunza maana ya maneno ya Mola wako uonje ladha ya Qur-aan. Vile vile jitahidi kujiwekea wakati wa kuhifadhi japo sura ndogo ili ukitoka katika Ramadhaan uwe una surah zaidi za kusoma katika Swalah zako. 
10.    Darsa
Hudhuria Darsa katika mwezi huu au soma vitabu vya dini, au sikiliza mawaidha.  Jambo hili ni muhimu sana kwani kusikiliza mawaidha ni njia muhimu na bora kabisa katika kuzidisha imani yako.  Kwa hakika unahitaji saa tu kuweza kutimiza jambo hili muhimu kila siku.  Kama huwezi kuhudhuria msikitini, Alhamdulillah, MUSLIM OF AFRICA  imewatayarishia mawaidha mengi ya kusikiliza na ya VIDEO.  Kwa hiyo badala ya kutazama televisheni na kusikiliza muziki jambo ambalo ni haramu ni bora utazame na kusikiliza mawaidha ujipatie manufaa, thawabu na kuongeza elimu yako. Kumbuka kwamba kama vile mwili unavyohitajia chakula, hali kadhalika Moyo na Nafsi zinahitaji chakula chake nacho ni kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى  kwa kila aina ya ukumbusho, na mawaidha na darsa za dini ni mojawapo ya chakula kizuri kabisa cha kutakasa Moyo na Nafsi kwa kuzijaza iymaan na mapenzi ya Mola Wako Mtukufu.

Sunday, July 8, 2012


Bismillahi naanza, salaamu zipokeeni,
Mungu Atatuongoza, Atutoe mashakani,
Azidi Kutuongoza, Atunawiri machoni,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Viumbe tuwe tayari, inakuja Ramadhani,
Tukae tukifikiri, ikija tufanye nini?
Tufanye mengi ya kheri, na tusome Qur-ani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Tusipoteze wakati, kuzurura mitaani,
Au kusoma gazeti, asubuhi na jioni,
Au nyumbani kuketi, kuona televisheni,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Tusibaki kukoroma, kujibwaga vitandani,
Au kwenda kwenye ngoma, mchezo wa mashetani,
Au kwenye masenema, kwenye picha za kigeni,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Mwezi huo mtukufu, tayari upo njiani,
Kula chakula khafifu, acha nafasi tumboni,
Hapana ubadhirifu, Anaupinga Manani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Omba dua omba sana, mwezi huu wa imani,
Fursa kupata tena, hiyo haijulikani,
Leo upo twakuona, kesho upo kaburini,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Kwenda kucheza karata, ni madhambi ikhwani,
Faida hautopata, ni upuuzi kwa yakini,
Mwisho wake ni matata, na ugomvi barazani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Kwenda kufuata mpira, mpaka kule uwanjani,
Jambo hili linakera, zindukeni Waumini,
Wakati unatupora, majuto huja mwishoni,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Tusigombane na watu, kwa matusi hadharani,
Tazama Mtume wetu, ifikapo Ramadhani,
Huwa mpole wa watu, na mwingi wa ihsani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Mwezi mmoja sio mwingi, ndugu zangu kumbukeni,
Mema tufanye kwa wingi, iwe akiba mbeleni,
Tarawihi ni msingi, wa mwezi wa Ramadhani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Mungu Atupe subira, asitushinde shetani,
Mungu Atupe sitara, akhera na duniani,
Tunaomba maghfira, na ridha Za Rahmani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.

Thursday, July 5, 2012

MATATIZA YA ZANZIBAR YANATOKANA NA WAZANZIBAR WENYEWE

Najua kama kukanusha ndio tabia ya binaadamu kwani aambiwae ukweli huwa si rahisi kuukubali ukweli huo kama viongozi wa zanzibar ndio chimbuko la migogoro yote yanayojitokeza katika muungano.
Wamezoeya kupiga kofi japo kwamba jambo linawakandamiza ilimradi posho inaingia mifukoni mwao ni muhali kulipinga.
Leo tumefika hapa waliorithi wapiga kofi nao sasa wanajaribu kutaka kukanusha lakini wapi ,farasi ameshakimbia ndio tamko linatoka “funga banda funga banda’ iko haja gani ya kufunga banda huku wakilaumiana kisiri siri .
Mwalimu nyerere katika mkutano wake mmoja nakumbuka alisema”wazanzibari tunawabembeleza angalau waseme jambo katika vikao lakini hakuna anaesema ,basi nyinyi wazanzibari hamna shida na hapa katika kikao ndipo pa kusema matatizo yenu?”
Wazanzibari wakiwa bungeni hawajui kusema ni mabubu lakini wakirudi nyumbani zanzibar ni mahodari kupanga mbinu za kuwadhoufisha wananchi,sasa tusemeje ?si ndio wao wenye matatizo?.
Kadhia hii haitaisha kwa wazanzibari matapeli ,ni mahodari kuomba ridhaa za wazanzibari lakini wakeshapewa huwa wadodosaji wakubwa katika bunge na hata wawakilishi.
Lengine ni kwamba wanaojichukulia ridhaa kwa nguvu ,wizi na hadaa kutoka kwa wananchi huwa si watu wema,wasomi au wenye kujua jambo ila ukereketwa ambao hautaisaidia zanzibar kuendelea mbele ila kurudi nyuma nyuma nyuma mpaka tugubikwe na kiza na kweli giza limeshatugubika.
Sidhani kama tunaweza kuondokana na aina hii ya wapiga kofi,wasinzilizi mpaka kuangukwa na udenda kikaoni,wachochezi wa kudhoufisha na kuwakandamiza wananchi wa chini hata ikibidi kuwapandikizia kesi zisizo kichwa wala miguu.alimradi dhulma juu ya dhulma nasi hatutambui na hatutatambua mpaka laana na ghadhabu za Mola wetu zitumalize ,yote ni nani ? ni wazanzibari wenyewe.
Tusipate taabu ya kumtafuta mchawi ,wachawi ni sisi wenyewe wazanzibari na hatutafika pahali mpaka wachawi wote wadhibitiwe na allah na inshaalla atawadhibiti.
Wachawi wengi wameshapita na hawa tulionao sasa inshaalla Mola atawadhibiti kisha atuangazie nuru itokayo kwake kwa umoja wetu wazanzibari.
Tumebaki kuwasifu ,kiongozi huyu hodari,kiongozi huyu hivi ,hakuna hata mmoja wote wachawi wa nafsi nyingine .
Kama ni kweli viongozi wazuri wangeliagiza wananchi wapigwe mabomu kama yaliyotokezea mahonda na donge? ila matatizo ni wazanzibari wenyewe ,hata kama serikali ya tanzania imetoa agizo hilo ,ina mamlaka gani ndani ya zanzibar ikiwa viongozi wa zanzibari wenyewe hawataki

Sunday, July 1, 2012

TARTIBU ZA KULALA


Muislamu hukuona kulala kwa jicho la kuwa ni miongoni mwa neema ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaneemesha waja wake kwa maslahi na manufaa yao ya kimwili, kiakili na kiroho. Tusome na tutafakari : "NA KWA REHEMA ZAKE AMEKUFANYIENI USIKU NA MCHANA ILI MPUMUE NA MTAFUTE FADHILA ZAKE (hapo mchana) NA ILI MPATE KUSHUKURU" [28:73].Na tusome tena : "NA TUKAUFANYA USINGIZI WENU KAMA KUFA (ili mpate kupumzika)" [78:9].
Hii ni kwa sababu kupumzika mtu usiku baada ya harakati za kuchosha za maisha za mchana kutwa, huusaidia mwili wa binadamu kuendelea kukua na kuwa mchangamfu, wenye nguvu ili mwanadamu aweze kutekeleza majukumu yake aliyopewa na Mola wake. Sasa ili mwanadamu aweze kuishukuru neema hii ya kupata muda wa kupumzika (kulala) hana budi kuzichunga na kuzifuata adabu na taratibu zifuatazo katika kulala kwake :
  1. Asichelewe kulala baada ya swalatil-Ishaa ila kwa dharura muhimu, kama vile kudurusi elimu (kusoma), au kuzungumza na mgeni. Muongozo huu unapatikana katika hadithi iliyopokelewa na Abu Barzah kwamba Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa akichukia kulala kabla ya Swalatil Ishaa na kuzungumza baada yake. Bukhaariy na Muslim. Muislamu anatakiwa alale mapema ili aweze kuamka usiku kuswali.
  2. Ajitahidi kulala akiwa na udhu. Hili ni kwa kuitekeleza kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipomwambia Baraai bin Azib – Allah amuwie Radhi – "Unapotaka kulala, tawadha udhu wako wa swala" Bukhariy na Muslim.
  3. Anapopanda kitandani aanzie kulalia upande wake wa kulia na alalie mto. Hapana ubaya wowote ikiwa baada ya kushikwa na usingizi atageukia upande wa kushoto. Maelekezo na mafundisho haya tunayapata katika kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipomwambia Baraai bin Aazib "Unapotaka kulala, tawadha udhu wako wa swala, kisha lalia upande wako wa kulia". Na pia katika neno lake : "Unapokiendea kitanda chako il-hali ukiwa twahara basi litegemezee mto taya/shavu lako lako la kulia"
  4. Asilalie tumbo lake (asilale kifudifudi) mchana au usiku. Haya ni kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa iliyopokelewa kwa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kwamba amesema : "Huo ni ulalaji wa watu wa motoni" Na amesema tena : "Huo ni ulalaji asioupenda Mwenyezi Mungu Mtukufu"
  5. Alete dua na dhikri zilizopokelewa kutoka kwa Bwana Mtume. Miongoni mwa dhikri hizo ni hizi zifuatazo :
    1. Aseme SUBHANALLAH WALHAMDU LILLAH WALLAHU AKBAR *33, Kisha aseme LAA ILAHA ILLA LLAH WAHDAHU LA SHARIKA LAHU LAHUL MULK WALAHUL-HAMD WAHUWA ALAA KULLI SHAY-IN QADIR. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipomwambia Aliy na Bintiye Fatmah – Allah awawie radhi – walipomtaka Bwana Mtume awapatie mtumishi wa kuwasaidia shughuli za nyumbani : "Je nisikufundisheni lililo bora kuliko hili mliloliomba ? Mnapotaka kulala semeni SUBHANALLAH mara 33, AL-HAMDULILLAH mara 33 na ALLAHU AKBAR mara 34, haya ni bora zaidi kuliko mtumishi." Muslim
    2. Asome Suratil Fatiha (Al-Hamdu) na mwanzo wa Suratil Baqarah mpaka kwenye neno MUFLIHUUN, na ayatil Kursiy na aya za mwisho wa sura. Haya ni kwa mujibu wa riwaya zilizopokelewa katika kulipondokesha jambo hili.
    3. Dua yake ya mwisho kabisa kabla ya kulala iwe ni dua hii iliyopokelewa kutoka kwa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
      {kiarabu}
  6. Akiamka asubuhi alete dhikri zifuatazo :
    1. Aseme atakapoamka kabla hajainuka kitandani : ALHAMDU LILLAHI-LLADHIY AHYAANAA BAA’DA MAA AMAATANAA WA ILAYHIN NUSHUUR.
    2. Ainue macho yake juu na asome : INNA FII KHALQIS-SAMAAWATI WAL-ARDHI -> aya kumi za mwisho za suratil Aali Imraan. Azisome aya hizo atakapoamka kwa ajili ya tahajjud (swala ya usiku) kwa kuifuata kauli ya Ibn Abbaas –Allah awaridhie – "Nilipolala kwa ndugu wa mama yangu Maymuna, mkewe Mtume – Rehema na Amani zimshukie – Mtume alilala mpaka nusu ya usiku au kabla yake kidogo au baada yake kidogo. Halafu aliamka na akawa anaupangusa usingizi usoni mwake kwa mkono wake, kisha akazisoma zile aya kumi za mwisho wa Suratil Aali Imran halafu akaenda akatawadha vema na akaswali" Bukhaariy.
    3. Aseme mara nne : ALLAHUMMA INNIY ASBAHTU BIHAMDIKA USH-HIDUKA WA USH-HIDU HAMALATA ARSHIKA, WAMALAAIKATAKA, WAJAMII KHALQIKA ANNAKA ANTAL-LAHU LAA ILAHA ILLA ANTA WA ANNA MUHAMMADAN ABDUKA WARASULUKA" Dua hii ni zao la kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – "Atakayesema maneno hayo mara moja, Allah ataiwacha huru roho ya (mwili) wake na (adhabu ya) moto, na atakayesema mara tatu, Allah ataiwacha huru robo tatu yake na moto na akiyasema mara nne, Allah atamuacha huru yeye mzima na moto" Abu Dawoud.
    4. Aseme anapouweka mguu wake kwenye kizingiti cha mlango hali akitoka nje : BISMILLAH TAWAKKALTU ALAL-LAH LAA HAWLA WALAA QUWWATA ILLA BILLAH. Amesema Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – "Mja atakapoyasema maneno haya, huambiwa umeongozwa na umetoshezwa" Tirmidhiy.
    5. Akivuka kizingiti cha mlango aseme : ALLAHUMMA INNI AUDHUBIKA AN ADHWILLA AU UDHWALLA, AU AZILLA AU UZALLA, AU ADHLIMA AU UDHLAMA, AU AJ-HALA AU YUJHALA ALAYYA" Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Ummu Salamah : Hakupatapo kutoka nyumbani kwangu Mtume – Rehema na Amani zimshukie – katu ila aliyainua macho yake mbinguni/juu na kusema "ALLAHUMMA INNIY AUDHUBIKA AN ADHWILLA AU UDHWALLA …" Abu Dawoud.

POLISI INAWATAKA NINI WAZANZIBARI?


KAMA wapo Watanzania waliobisha ushiriki kamili wa Jeshi la Polisi katika kufanya uhalifu dhidi ya binadamu Zanzibar , kwa matukio ya 26-27 Mei, basi watafakari matukio mapya ya 17 Juni. Katika matukio yale, askari wa polisi walipewa silaha na kusukumiza risasi za mipira na mabomu ya kutoa machozi. Wakashambulia ofisi za mawakili, gari za wananchi na nyumba za viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI).
Ni matukio ambayo hadi leo, polisi haijayatolea taarifa licha ya kupokea malalamiko mbalimbali ya wananchi.
Wananchi walipoteza mali zao: gari zilizoharibiwa kwa mabomu; na Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS) wanaolalamikia kitendo cha polisi kuteketeza kwa mabomu ofisi za wanachama wao zilizoko Amani.
Bado Polisi haijaeleza chochote kuhusu vitendo vyao hivyo vilivyoonyesha dhahiri kuwageuka wananchi ambao kwa mujibu wa sheria na utendaji wa jeshi hilo , wanapaswa kuwalinda wao kama binadamu pamoja na mali zao.
Mpaka hapo, picha iliyojengwa kuhusu matukio hayo, ni kwamba Uamsho ndio walihusika kuhujumu mali za wananchi. Ni Uamsho pia wanaotajwa kuchoma makanisa wawili, lile la Assemblies of God (TAG) la Kariakoo na jingine la Mwanakwerekwe.
Ni aibu kuwa Polisi walichosema katika kadhia yote ile, ni hicho tu. Kwa bahati mbaya wanaoelewa dhamira mbaya za jeshi hili wanajua upi mchele wa kuchukua, na zipi pumba za kupuuza.
Kwa kuwa ni wao waliolikoroga, wataendelea kulinywa wao wenyewe. Wanasubiriwa wakatoe ushahidi wa tuhuma zao dhidi ya Uamsho.
Lakini, kama vile matukio hayo ni madogo na ya kuzua na ambayo wanaamini hayathibitishi vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu, Jeshi la Polisi likaingia tena katika utendaji wa ovyo wiki tatu tu baadaye – tarehe 17 Juni.
Polisi wake wenye silaha walikatiza msafara mrefu wa gari, pikipiki na vespa wa wafuasi wa Uamsho waliokuwa wakienda kijiji cha Donge ambako taasisi hiyo iliandaa mhadhara wa kutoa elimu kwa umma kuhusu Muungano.
Mhadhara huo uliokuwa umeruhusiwa kwa mujibu wa sheria, ulisimamishwa eneo la Mahonda, Msikiti wa Ijumaa, mita 100 hivi kutoka kilipo kituo cha Polisi Mahonda.
Mpaka wanafanikiwa kutawanya wafuasi wa Uamsho kwa mabomu ya machozi, risasi za mipira na marungu, watu kadhaa waliachwa wameumia na mali nyingi kuharibiwa.
Polisi, wakijua kuwa Uamsho wana vibali vyote vya kufanya mhadhara msikitini Donge Pwani, walijipanga baina ya msikiti wa Ijumaa na kituo cha polisi, wakataka wana Uamsho warudi mjini.
Mhadhara umekusudiwa kufanyika Donge, Polisi wanazuia msafara Mahonda, mwanzo wa jimbo la Donge, ambalo wanasiasa wanaojifanya wafalme, wanataka jimbo hilo liwe bikira kisiasa pamoja na mfumo wa vyama vingi kuishi kwa mwaka wa 20 sasa.
Polisi wanajua Uamsho hawajavunja sheria, wana umma mkubwa wa watu unawafuata nyuma na kila waendako kuhadhir, kuwazuia katikati ya safari yao ni kuwachochea wakasirike.
Wana Uamsho wakasita. Wakashuka kwenye gari zao na vyombo vyao vingine. Wakabaki hapo kusubiri viongozi wao waje kutoa uamuzi. Kwa kuwa pale waliposimamishwa na polisi, pembeni kuna msikiti mkubwa, wakaamua baadhi yao kuingia msikitini kwa ajili ya sala na dua.
Viongozi walipofika Mahonda, na kupata taarifa ya kilichotokea na kinachoendelea, nao wakaamua kushuka. Wakawafuata viongozi wa polisi ili kujadiliana nao. Ndipo wanapewa taarifa ya amri ya mkuu wa mkoa kuzuia mhadhara Donge.
Lahaula, kufa hakuna breki. Palepale milio ya risasi za mipira na mabomu ya machozi ikaanza kurindima. Askari wakaingia msikitini bila ya kuvua viatu – hatua ya kunajisi msikiti. Wakapiga watu na kuwatupia matusi.
Mtu mmoja waliyemkuta chooni akijisaidia, alitukanwa kwa matusi ya nguoni. Akalazimishwa kutoka na kupita katikati ya msikiti bila ya kunawa au kusafisha miguu yake; huku akisindikizwa na askari ambaye naye hakuvua viatu vyake ambavyo wakati huu vilikuwa vimenasa uchafu.
Polisi wakaingia upande wa wanawake na kuwapiga huku wakiwavua nguo na kuwatusi na kuwadhalilisha. Ni matendo yaliyoonyesha uchokozi wa dhahiri dhidi ya dini.
Kuthibitisha kuwa polisi walishapanga ubaya, walisasambua mitaa ya Mahonda wanamokaa raia na kupita wakipiga wanaume huku wakiwavua nguo wanawake.
Hawakuchoka. Polisi wengine walitumwa kwenda hadi Donge ambako mhadhara ungefanyika na kupiga watu hata wale ambao walikutwa wakizungumza barazani kwao. Watu wazima nao hawakusalimika. Walipigwa na kutukanwa.
Polisi hawakuchoka. Walizunguka miji Mkokotoni, Kivunge, Mkwajuni, Gamba na Chaani. Mote humo wakipiga risasi za mipira na mabomu ya machozi. Wakitukana watu wazima wanaume na wanawake.
Sasa mhadhara ulikuwa umepangwa kufanyika Donge, vyereje polisi washambulie wananchi hata vijiji vingine hivyo? Ndio kule kupanga ubaya na uhalifu dhidi ya binadamu.
Leo, idadi ya watu wapatao 40 wanatajwa kuwa wanauguza majeraha ya risasi, mabomu na marungu. Wengi wengine wameumizwa kwa mateke.
Haji Khatib Ali wa Mahonda amechakazwa mguu kwa risasi na mzee Thabit Shaka wa Fukuchani amechakazwa tako kwa bomu.
Askari walimpiga mtu mwingine lakini risasi ikaduru ilipokutana na simu iliyokuwa kwenye mfuko wa suruali na kunusuru kumchakaza paja. Simu hiyo ilipasuka na kusambaratika.
Huu ni uhalifu dhidi ya binadamu. Ni uchokozi na uchochezi dhidi ya akili za wananchi wema wanaoipenda amani, wanaotii viongozi wa serikali yao ya umoja wa kitaifa.
Vitendo vya polisi vinasikitisha. Na athari zake ni kupandikiza uhasama kati ya askari na raia. Kuna askari hawajarudi makwao tangu hapo kwa kuhofia kushughulikiwa na wananchi kwa kuwa wameonekana wakipiga watu na kuripua kwa mabomu vespa na pikipiki zao.
Pia walipondaponda baiskeli za wananchi wanaoishi Mahonda waliokuwa wakisubiri nao kuondoka na msafara kutoka Mahonda kwenda Donge. Huko ni kuzikufuru neema za Mwenyezi Mungu. Hawi radhi kwa mambo haya.
Tatizo kubwa la Jeshi la Polisi sasa ni kujichukulia sheria mkononi na kushambulia raia na kuharibu mali zao. Tatizo jingine ni kule kufanya yote hayo, halafu wakaeneza uongo kwa ulimwengu kuwa wanadhibiti wakorofi.
Katika matendo hayo, ni nani hasa mkorofi? Polisi wameamua kuasi raia.
Sasa watu wa Donge wanauliza: Wao ni nchi gani? Inatumia sheria zilizo tofauti na sehemu nyingine ya nchi yao au wao wana taifa jingine?
Wanayauliza maswali haya kwa viongozi wao – mwakilishi Ali Juma Shamhuna, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Polisi wanalia sasa maana shutuma zote zimewaelekea.

UAMSHO NI SAWA NA WAAMSHA DAKU

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Amani Abeid Karume, akiwahutubia Wanachama wa CCM wa Jimbo la Rahaleo katika ukumbi wa Tawi la CCM Gulioni
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dk Amani Abeid Karume amewafananisha Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar (JUMIKI) kuwa sawa na waamsha daku wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na kuwataka Wana CCM kubakia na misimamo yao katika suala la Muungano.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika Jimbo la Rahaleo Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Dk Karume alisema kwamba CCM haijalala hivyo wanachama wa CCM hawana sababu ya kuwa na hofu na Uamsho kwani wao hawakulala na wenye kuamshwa ni wale waliolala.
“Kwani nyie mmelala mpaka muamshwe, nyie mko macho eti…hao ni kama wale wanaoamsha daku utakasirika, lakini ukiamka unasema ahaa kumbe muda wa kula daku tena hofu ya nini” Alisema Dk Karume na kuwachekesha waliohudhuria mkutano huo.
Makamu huyo Mwenyekiti alilazimika kutoa maelezo hayo baada ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mjini Unguja, Borafia Silima Juma kueleza wasiwasi wa wanachama wa CCM kuhusu vurugu zilizotokea mwezi Mei mwaka huu na harakati kundi la Uamsho.
Dk Karume akijibu hilo, alisema juhudi za kuiweka Zanzibar katika hali ya maelewano ilifanywa na Jumuiya za Kimataifa na Mataifa kutoka nje, lakini hawakuweza kusuluhisha migororo ya kisiasa iliyodumu kwa takriban miongo mitatu, lakini baada ya Wazanzibari wenyewe kuamua kuacha tofauti zao maridhiano yalifikiwa mwaka 2009.
Akitoa historia feru na miafaka na maridhiano Dk Karume alisema wakati wa utawala wake walihakikisha kabla ya kumaliza kipindi cha utawala wake anaiwacha Zanzibar ikiwa salama, yenye umoja na mshikamano na isiyokuwa ya vipande vipande ambapo hali hiyo ilifanikishwa baada ya kufikiwa kwa maridhiano ya kisiasa baina ya Chama ch Wananchi(CUF) na Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Mimi na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad tulikutana Ikulu na kukazungumza kwa nini kumaliza tofauti zetu maana sisi sote ni wamoja na leo mafanikio yake ndio haya ya Zanzibar imetulia kwa hivyo natoa wito wa kuendeleza umoja huu” Alisema Dk. Karume.
Akizungumzia suala la maoni kuhusu Muungano, Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM alisema watu wote wanaotoa maoni kimsingi wanatumia haki ya kikatiba na kidemokrasia hivyo wana CCM wanachotakiwa ni kuendelea kusimamia azma ya ujenzi wa chama chao huku wakiendelea kuheshimu misimamo yao bila ya kuyumbishwa.
Dk Karume alisema hoja ya Muungano wako baadhi ya watu amewasikia wakitaka Muungano uendelee, wengine wakishauri ufanyiwe marekebisho na mabadiliko huku wengine wakitaka uvunjike.
“Msipatwe na homa, ondoeni hofu na wasiwasi , waacheni masheikh wajibishane na masheikh wenzao na sisi wanasiasa tutafute majibu mjarab yatakayofaa ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha vijana wetu kutambua mahali tulikotoka, tulipo sasa na kule tuendako”Alisema.
Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alitamka bayana kuwa katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi njia pekee ni kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura ili kushinda katika kila uchaguzi na si kinyume chake.
Mkutano huo uliofanyika katika Tawi la Gulioni ambako alizungumza na wanachama wa matawi mawili la Gulioni na Mwembeladu ni wanachama wachache waliohudhuria tofauti na matarajio ya watu wengi ambapo kuliwekwa mabomba nje ya tawi hilo lakini wasikilizaji walikuwa kidogo mno.
Viongozi walioambatana na Dk Karume ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini, Yussuf Mohammed, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mjini Borafya Silima, Mbunge wa Rahaleo,  Abdallah Juma Abdallah (Maabodi), na Mwakilishi wake Salim Nassor (Aljazira), Mwakilishi wa Chumbuni Machano Othman Said, Isa Haji Gavu Mwakilishi wa kuteuliwa, Mussa Perera Silima mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi CCM. na wanachama wachache wa chama hicho.