Chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini Tanzania (Chadema),
kimesema huenda kikachukua uamuzi mzito wa kujiengua kwenye mchakato wa
kutafuta katiba mpya nchini humo iwapo mambo muhimu na ya kimsingi
hayatapatiwa ufumbuzi wake hadi ifikapo tarehe 30 Aprili mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania
imeeleza kuwa, Chadema kinataka kufutwa uteuzi au uchaguzi wa wajumbe wa
Mabaraza ya Wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata
na badala yake wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya wachaguliwe moja
kwa moja na wanachi wa Kata bila ya kuchujwa na Kamati za Maendeleo za
Kata. Wakati huohuo,
Msikiti mmoja katika kitongoji cha mji mkuu wa Sweden, Stockholm
umeruhusiwa kuadhini kwa kutumia kipaza sauti kilicho kwenye mnara kwa
ajili ya Sala ya Ijumaa. Hii ni mara kwa kwanza kwa nchi hiyo ya
Scandinavia kuruhusu adhana kwa sauti inayosikika nje ya msikiti.
Idara ya polisi mjini Stockholm imesema msikiti huo utaruhusiwa
kuadhini kwa muda wa kati ya dakika tatu na tano katika kipindi cha
baina ya saa sita na saa saba mchana kila Ijumaa. Mkuu wa Jumuiya ya
Utamaduni wa Kiislamu katika eneo la Botkyrka kusini mwa Stockholm Bw.
Ismail Okur ameupongeza uamuzi huo. Ombi la kuadhini kwa sauti inayotoka
nje ya msikiti liliwasilishwa miaka mitano iliyopita. Kuna karibu
Waislamu 7,000 katika eneo hilo na aghalabu wana asili ya Uturuki. Chama
chenye chuki dhidi ya Uislamu cha Sweden Democrats kimepinga uamuzi
huo.














