Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Friday, September 13, 2013

Jeshi la Mali lapambana na waasi wa Tuareg


Jeshi la Mali lapambana na waasi wa Tuareg
Habari kutoka Mali zinasema kuwa, mapambano makali yameshuhudiwa kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa Tuareg katika mji wa Lere katikati mwa nchi hiyo. Duru za habari zinaripoti kuwa, waasi hao ndio walioanza kuwashambulia wanajeshi wa serikali kuanzia jana Jumatano ingawa wao wamedai jeshi ndilo lililoanza kuwafyatulia risasi na makombora ya mizinga. Makabiliano hayo yamepelekea waasi kadhaa kuuawa huku wanajeshi 3 wa serikali wakijeruhiwa vibaya. Hii ni mara ya kwanza kwa vita kama hivyo kutokea tangu pande mbili hizo kusaini makubaliano ya amani mwezi Juni mwaka huu. Vita hivyo aidha vinatokea ikiwa imepita wiki moja tu tangu rais mpya, Ibrahim Keita ashike rasmi hatamu za uongozi wa nchi hiyo ya mgharibi mwa Afrika; jambo linaloashiria kibarua kigumu kinachomsubiri kiongozi huyo katika juhudi zake za kutafuta maridhiano ya kitaifa.

UNHCR: Tanzania imewafukuza Warundi 30,000


UNHCR: Tanzania imewafukuza Warundi 30,000
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema kuwa maelfu ya Warundi waliokuwa wakiishi katika nchi jirani ya Tanzania wamerejeshwa nchi kwao kwa nguvu katika siku 30 zilizopita. Catherine Huck, Kamishna wa UNHCR amesema kwamba, ni vigumu kujua idadi ya Warundi waliofukuzwa kutoka Tanzania lakini kwa uchache ni watu kati ya elfu 20 hadi elfu 30.
Karibu Warundi milioni moja walivuka mpaka na kuingia Tanzania wakati wa vita vya ndani vya mwaka 1993. Ingawa wakimbizi wengi wa Burundi walirejea nchini kwao baada ya vita hivyo kuisha mwaka 2006 lakini baadhi yao bado wanaishi  nje ya nchi ikiwemo Tanzania.

Saturday, September 7, 2013

WAANDAMANA KUPINGA MISS WORLD,INDONESIA

Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza mwanzoni mwa wiki hii kupinga  mashindano ya Miss World yanayotarajia kuanza jumapili ya kesho nchini Indonesia .Waandamanaji hao wametaka shindano hilo lifutwe kwani linadhalilisha utu wa mwanamke na ni kinyume na mafundisho ya kiislamu.
Upinzani mkubwa toka kwa waandamanaji hao umezidi, katika taifa hilo lenye  Waislamu wengi zaidi duniani,licha ya waandaaji kudai wameondosha vazi la ufukweni (bikini)

Baadhi ya wanaume na wanawake 800 kutoka kundi la Hizbut Tahrir la Indonesia wamekusanyika katika mji wa Jakarta nje ya wizara ya ustawi wa jamii, wakitoa wito kwa serikali wa kufuta shindano hilo.
Aidha waliandamana hadi makao makuu ya shirika la habari la Indonesia MNC kwamba liache kutangaza habari za shindano hilo lililopotoka. "Je, tunataka nchi yetu kuonekana kama ya watu wa ngono?" mmoja wa waandamaji alisema kwa sauti kubwa .

"Sisi tutaendelea kuandamana na kuwaambia watu jinsi ya udhalilishaji wanawake kwa kufanyika shindano hili," alisema mratibu wa maandamano hayo,  Zikra ASRI,huku akiwa amezungukwa na wanawake  waliovaa hijabu nyeupe na baibui nyeusi.

Mjini Medani katika kisiwa cha Sumatra,  wanachama 500 wa Hizbut Tahrir waliandamana hadi majengo ya serikali, na kudai kuwa shindano hilo lifutwe.Licha ya upinzani kuongezeka , waandaaji wamesema kuwa  shindano hilo lazima lifanyike na halita athiri heshima na utamaduni wa indonesia
Shindano la Miss Dunia linatarajiwa kuanza Jumapili katika kisiwa cha Bali, na mshindi anatarajiwa kupatikana  katika jiji la Jakarta Septemba 28.

Nchi hiyo yenye watu milioni 240,June mwaka jana mwanamuziki Lady Gaga alilazimika kufuta onesho lake,baada ya viongozi wa dini ya kiislamu kutishia kuchoma moto ukumbi ambao atafanyia onesho hilo,baada ya mwanamuziki huyo kuonesha mavazi yake ya ndani.
waandamanaji nchini indonesia

MSIKITI WAWAKA MOTO MKOANI DODOMA

Msikiti wa Answar Sunna ulipo mjini DODOMA wateketea kwa moto mchana huu.


Msikiti mkubwa wa Answar Sunna  uliopo  barabara ya saba mjini Dodoma  umewaka  moto  mchana  huu  ikiwa  ni  muda  mfupi  baada  ya  swala  ya  mchana  kumalizika....


Akiongea  kwa  njia  ya  simu  na  Mpekuzi wetu, mmoja  wa  mashuhuda  walioshuhudia  tukio  hilo  amedai  kuwa  chanzo  cha  moto  huo  ni  moto wa  JIKO  la  wakazi  wa    ghorofa ya  juu  ya  jengo  la  msikiti  huo...

Hata  hivyo, shuhuda  mwingine  aliyeongea  na  mtandao  huu  amedai    kuwa  chanzo  cha  moto  huo  ni  hitilafu  ya  umeme  iliyoanzia  ghorofa  ya  juu  ya  jengo  hilo. 

 
Kwa  mujibu  wa  mashuhuda  hao, moto  huo  umefanikiwa  kudhibitiwa  na  jeshi  la  zima  moto  na  kwamba  hakuna  mtu  aliyepoteza  maisha  kutokana  na  moto  huo.

Tunaendelea  kufuatilia  undani  wa  tukio  hili.
source:ndotoblog

Friday, September 6, 2013

DAKTARI FEKI AKAMATWA HOSPITALI YA KCMC, MOSHI

HALI ya wasiwasi imetanda kwa baadhi ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi baada ya uongozi wa hospitali hiyo kumkamata mtu mmoja anayedaiwa kujifanya ni daktari wa watoto akiwa kwenye wodi ya upasuaji.

Daktari huyo feki aliyefahamika kwa jina la , Alex Sumni Massawe alikamatwa jana majira ya saa 5 asubuhi na kuwekwa chini ya ulinzi mkali wa makachero wa Jeshi la Polisi waliokuwa wamevalia nguo za kiraia baada ya kukutana na mmoja wa wagonjwa ambaye alimuahidi kumfanyia mwanae wa kiume upasuaji wa ngozi.
Kabla ya kukamatwa kwa Alex, mama mzazi wa kijana aliyekuwa akitakiwa kufanyiwa upasuaji, Pamvelina Shirima alikutana na daktari huyo katika baa moja maarufu mjini hapa iliyopo eneo la Dar Street (jina limehifadhiwa) na kumtoza sh.200,000 akidai zitatumika kuharakisha mwanae afanyiwe vipimo vya upasuaji.
Alex anadaiwa alitaka kumfanyia upasuaji kijana, Makasi Tipesa, mkazi wa Manispaa ya Moshi ambaye amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi kwa muda mrefu sasa.
Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya KCMC, Bw. Gabriel Chisseo alisema daktari huyo aliwekewa mtego na uongozi wa hospitali ya KCMC kutokana na baadhi ya wagonjwa kuripoti kutapeliwa na mmoja wa madaktari ambaye amekuwa akijinasibu kwamba anafanya huduma hiyo kutokana na wito alionao katika fani hiyo.
“Leo asubuhi(jana) mteja wetu ambaye amekuwa akitibiwa hapa alitapeliwa na huyu Alex , tulimkamata akiwa wodi ya upasuaji baada ya kupokea kiasi cha sh.200,000 kutoka kwa Pamvelina Shirima ambaye alimleta mwanae afanyiwe upasuaji wa ngozi", alisema Chisseo.
Uongozi wa Hospitali ya KCMC umethibitisha kwamba mtu huyo aliyekamatwa ndani ya Hospitali hiyo, si mwajiriwa wao na wala hakukutwa na sare wala kitambulisho kinachomtambulisha kitengo chake cha kazi.
Hivi karibu kumeibuka matukio ya watu kadhaa kujivika kuwa na taaluma mbalimbali ambazo si za kweli huku jeshi la polisi likifanikiwa kuwakamata wengine wakijifanya kuwa ni maofisa wa jeshi hilo ,wengine usalama wa taifa huku wengine wakijifanya asakri wa kikosi cha usalama barabarani.

Afisa uhusiano wa hosptali ya Rufaa ya KCMC,Gabriel Chisseo akimwonesha anayedaiwa kujifanya daktari katika hosptali hiyo (Daktari Feki) aliyetambulika kwa jina la Alex Massawe. Daktari Feki Masawe akisindikizwa na baadhi ya wafanyakazi wa hosptali ya KCMC kutoka katika moja ya wodi ambayo alikuwa 'akihudumia'.
Daktari feki akiwa katika gari la polisi tayari kupelekwa kituo cha polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe
 



Aliyejidai kuwa ni Daktari katika hosptali ya KCMC(Daktari Feki) aliyetambulika kwa jina la Alex Massawe akiwa amefungwa pingu mikononi mwake katika eneo la hosptali hiyo.

Thursday, September 5, 2013

UN: Mgogoro wa Syria ni mkubwa mno


UN: Mgogoro wa Syria ni mkubwa mnoUmoja wa Mataifa umesema kuwa watu elfu sita wanaikimbia Syria kila siku kutokana na kushadidi mapigano nchini humo. Hayo yalisemwa jana katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani. Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa Masuala ya Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa amesema katika kikao hicho kuwa kamisheni yake haijawahi kuona idadi ya wakimbizi ikiongezeka kwa kiwango cha kutisha namna yote hiyo tangu miaka 20 iliyopita. Ivan Simonovic, Naibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya haki za binadamu amedai kuwa, watu wasiopungua 92,901 waliuawa huko Syria kati ya mwezi Machi mwaka juzi hadi mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, miongoni mwao wakiwemo watoto zaidi ya 6,500. Amesema, inakadiriwa kuwa watu elfu tano wanauawa huko Syria kila mwezi. Serikali ya Damascus inasema kuwa, madola ya kigeni ambayo hayaitakii kheri Syria yamepeleka makundi ya kigaidi na kuyasaidia kwa kila hali ili yafanye mauaji ya raia na maafisa wa serikali nchini humo.

Wito watolewa kusitisha mashambulio dhidi ya M23


Wito watolewa kusitisha mashambulio dhidi ya M23
Mawaziri wa Mambo ya Nje waEneo la Maziwa Makuu Barani Afrika wametaka kusitishwa mashambulio dhidi ya waasi wa M23 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kutoa mwanya kwa mazungumzo ya amani ya Kampala, Uganda.
Aidha wametaka kikosi cha uingiliaji cha Umoja wa Mataifa kuwashambulia waasi kutoka Uganda, Rwanda na Burundi ambao wanaendesha shughuli zao huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kati ya waasi hao ni wale wa FDLR, FNL na ADF.
Hayo yamebainika katika kikao cha faragha cha wakuu wa ulinzi na mawaziri wa mambo ya nje wa Eneo la Maziwa Makuu Barani Afrika waliokutana Kampala Jumatano usiku. Akizungumza baada ya kikao hicho Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Uganda Balozi James Mugune amesema machafuko katika eneo yanapaswa kutatuliwa kwa njia za amani. Leo Alkhamisi Viongozi wa Eneo la Maziwa Makuu Barani Afrika wanatazamiwa kukutana nchini Uganda kujadili hali ya Mashariki mwa Kongo. Nchi wanachama wa Kongamano la Kimataifa la Maziwa Makuu ni pamoja na Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Uganda, Rwanda, Sudan, Tanzania na Zambia.

Picha 12 za mama wa kinigeria aliyekamatwa na madawa ya kulevya katika uwanja wetu wa ndege



Jitihada za kurejesha heshima kwa viwanja vya ndege nchini zilizoanzishwa na waziri wa uchukuzu Dk. Harisson Mwakyembe zinaonekana kuzaa matunda baada ya mwanadada kutoka nchini Nigeria Anthonia Ojo (25) kukamatwa na kete 99 za madawa ya kulevya dar es salaam .
 
Mwanamke  huyo amekamatwa  akieleke Roma Italia kupitia Paris Ufaransa kwa ndege ya Ethiopian Airways  na  aliingia hapa nchini Agosti 30 akitokea Nigeria. 

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Viwanja vya Ndege, Renatus Chalya, Ojo ataendelea kubaki chini ya ulinzi wa polisi kwa uchunguzi zaidi, wakati madawa hayo yamepelekwa kwenye  ofisi ya mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini aina ya dawa hizo  na   thamani yake...

Zifuatazo ni picha mbalimbali za tukio zima la kunaswa kwa mtuhumiwa huyo .












Wednesday, September 4, 2013

Rais wa Somalia anusurika kuuawa


 
Rais Hassan Sheikh Mahmoud wa Somalia
Rais Hassan Sheikh Mahmoud wa Somalia amenusurika kuuawa leo katika shambulizi lililodaiwa kufanywa na wanamgambo wenye uhusiano na mtandao wa al Qaida dhidi ya msafara wake uliokuwa ukisindikizwa na vikosi vya jeshi. Rais wa Somalia alikuwa akikaribia kuwasili katika mji wa bandari wa Marka kusini mwa Mogadishu mji mkuu wa Somalia wakati wanagambo wa al Shabab walipourushia msafara wake maguruneti. Abdikadir Mohamed, Kamanda wa polisi ya Somalia   amethibitisha kutokea shambulio hilo na kueleza kuwa Rais Hassan Sheikh Mahmoud amewasili salama salimini humo Marka umbali wa kilomita 90 kutoka Mogadishu.
Wanamgambo wa al Shabab wamesema wamewaua wanajeshi kadhaa na kuharibu magari mawili ya kijeshi yaliyokuwa kwenye msafara wa Rais wa Somalia  ambao ulikuwa ukisindikizwa na askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika na wa serikali ya nchi hiyo

'Kenya inajiondoa ICC kuzuia ungiliaji wa kigeni'


Kiongozi wa Walio Wengi katika Bunge la Kenya Aden Duale
Kiongozi wa Walio Wengi katika Bunge la Kenya Aden Duale
Nchini Kenya Muungano wa Jubilee umesema mkakati wake wa kuiondoa nchi hiyo katika mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ni jambo ambalo litaiwezesha nchi hiyo kushughulikia migogoro yake pasina uingiliaji wa kigeni.
Kiongozi wa Walio Wengi katika Bunge la Kenya Aden Duale amesema muungano wa Jubilee unaamini kuwa ICC si mahakama huru na ya kujitegemea kama ilivyokuwa na hivyo kuna haja ya hatua za dharura kuchukuliwa kuiondoa Kenya katika mkataba ulioanzisha mahakama hiyo. Duale amesema asilimia 80 ya watu wote duniani si wanachama wa mahakama hiyo. Ametoa mfano na kusema nchi kama vile India, China na Marekani si wanachama wa ICC. Mbunge huyo mwandamizi wa Kenya amesema ICC inaweza kutumiwa vibaya na haina uwezo wa kutoa maamuzi huru.
Muungano wa Jubilee ambao una wajumbe wengi katika Bunge la Taifa na Baraza la Senate umesema utaongoza mjadala wa Alkhamisi wa kutaka Kenya ijiondoe ICC. Mswada huo umewasilishwa bungeni kabla ya kuanza kesi ya jinai dhidi ya binadamu inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta itakayoanza mwezi Novemba na ile ya Naibu wake, William Ruto inayotarajiwa kuanza mwezi huu wa Septemba.

Oman na Zanzibar kuendelea kushikamana na kushirikiana

Waziri wa Habari wa Oman Dkt. Abdulmuumin Mansour Bin Said Al- Hasan akiagana  na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya ujumbe wake kuzungumza yane hapo Ofisini kwake  Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Waziri wa Habari wa Oman Dkt. Abdulmuumin Mansour Bin Said Al- Hasan akiagana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya ujumbe wake kuzungumza yane hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Uhusiano wa  kubadilishana nyaraka za Kihistoria kati  ya Oman na Zanzibar  unaweza kuwasaidia wananchi  wa pande  mbili  pamoja na watafiti wa masuala ya Kihistoria kuelewa kwa kina maingiliano ya muda mrefu yaliyopo kati ya  Wazanzibar na Waoman ambayo yanafanana  Kisilka na Kiutamaduni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa Viongozi sita wa Serikali ya Oman ulioongozwa na Waziri wa Habari wa Nchi hiyo Dr. Abdulmumin Mansour Bin Said Al- Hasani aliokutana nao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema Zanzibar na Oman zimekuwa na uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu tokea karne ya 18 ambao umethibitishwa na wataalamu pamoja na watafiti wa mambo ya Kihistoria kutoka vyuo vikuu tofauti Duniani.
Alielezea haja kwa Viongozi na Wananchi wa Oman na Zanzibar kuendelea kushikamana na kushirikiana katika masuala mbali mbali ya maendeleo yatakayosaidia ustawi wa vizazi vya sehemu zote mbili rafiki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Serikali ya Oman  kupitia ushirikiano wa mamlaka  ya kumbu kumbu na nyaraka ya Oman na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } kwa kuandaa Kongamano la Kimataifa la Ustaarabu wa Kiiislamu kwa Nchi za Mashariki mwa Bara la Afrika.
Balozi Seif alisema  uamuzi huo wa kufanywa kwa kongamano hilo  hapa Zanzibar umekuja wakati muwafaka kwa wataalamu wa mambo ya Kale kubainisha kwamba  Historia ya Uislamu imeanzia hapa Zanzibar.
“ Nimefurahi kusikia kwamba Historia ya Uislamu imeanza Zanzibar. Inaonyesha watafiti wameliona hili kutokana na asilimia kubwa ya wakaazi wa Visiwa vya zanzibar  kuwa  waumini wa Dini ya Kiislamu sambamba na Utamaduni wake “. Alieleza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishauri tafiti za Wataalamu wa masuala ya Historia ambazo zitaibuka katika Kongamano hilo  zielekezwe zaidi kunufaisha wananchi  na waislamu wa ukanda wote wa Afrika Mashariki.
“ Tafiti hizi za Wataalamu wetu wa Kihistoria itapendeza kama zitaendelea kubakishwa katika maktaba zetu ili zisaidie wananchi, waislamu na hata wasomi wetu wa vyuo vikuu vya ukanda wetu wa Afrika Mashariki “. Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Serikali ya Oman ukiongozwa na Waziri wa Habari wa Nchi Hiyo Dr. Abdulmun Mansour Bin Said Al- Hasani hapo Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Serikali ya Oman ukiongozwa na Waziri wa Habari wa Nchi Hiyo Dr. Abdulmun Mansour Bin Said Al- Hasani hapo Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Naye Kiongozi wa Ujumbe huo wa Serikali ya Oman Waziri wa Habari wa Nchi hiyo   Dr. Abdulmumin Mansour Bin Said Al- Hasani alisema ipo haja ya kuendelea kuhifadhiwa kwa Historia iliyopo ya Zanzibar na Oman kwa faida ya vizazi vijavyo.
Dr. Abdulmumin alieleza kwamba upeo wa tabia za watu wa Oman na Zanzibar unaolingana ndio unaochangia na kushawishi wageni na watalii wa mataifa mbali mbali  duniani  kupendelea kuzitembelea nchi hizi zinazofanana kiutamaduni.
Waziri huyo wa Habari wa Oman alifahamisha kwamba Kongamano  hilo la ustarabu wa Kiislamu linalofanyika hapa Zanzibar  mbali ya utafiti uliopatikana lakini pia litafungua uhusiano katika Nyanja nyengine za maendeleo kwa nchi shiriki.
Dr. Abdulmumin alielezea faraja yake kutokana na umuhimu wa udugu uliopo  kati ya watu wa Oman na Zanzibar ambao umepelekea waoman wengi  kujitokeza kushiriki kwenye kongamano hilo.
Alifahamisha kwamba ipo ishara ya kuendelea kwa ziara za mara kwa mara kati ya watu wa pande hizo mbili.
Kongamano hilo la siku tatu linalofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya La Gemma Della East Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na kushirikisha Mataifa yapatayo 17 lina lengo la kuitangaza Zanzibar katika Nyanja za utafiti na Taaluma Kimataifa.
Hilo ni kongamano la Pili la Kimataifa la Ustarabu wa Kiislamu  kufanyika likitanguliuwa na lile la mwaka 2012 lililofanyika Nchini Uganda na kutolewa uamuzi wa kongomano linalofuata kufanyika hapa Zanzibar kutokana na  Historia yake  iliyopo  sambamba na uhusiano  wa karibu iliyonayo na Mataifa ya Kiarabu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Ujumbe wa Serikali ya Oman ambao pia upo Zanzibar kushiriki Kongamano la Kimataifa la Ustaarabu wa Kiislamu. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Habari wa Nchi Hiyo Dr. Abdulmun Mansour Bin Said Al- Hasani  na kushoto yake ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar  Said Ali Mb arouk.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Ujumbe wa Serikali ya Oman ambao pia upo Zanzibar kushiriki Kongamano la Kimataifa la Ustaarabu wa Kiislamu.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Habari wa Nchi Hiyo Dr. Abdulmun Mansour Bin Said Al- Hasani na kushoto yake ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mb arouk.

BREAKING NEWS...!!! MAJAMBAZI WAPORA NA KUJERUHI TEGETA.....



Kundi la watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na bunduki, wamefunga mtaa na kupora fedha na simu za kiganjani katika maduka 11 eneo la Mvumoni Madale, kata ya Wazo na Tegeta Kibaoni, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mashuhuda wa tukio hilo, wakizungumza jana na NIPASHE, walisema tukio hilo lilitokea juzi Jumapili, majira ya saa 1:30 usiku.
Hata hivyo, kumekuwa na taarifa za kukanganya kati ya wananchi walioathirika kutokana na mkasa huo ambao wanadai wameporwa simu na fedha kwa viwango tofauti katika maduka 11 huku Jeshi la Polisi likisema kuwa maduka matatu pekee ndiyo yamevamiwa na kuporwa kiasi cha Sh. 300,000. 
Katika eneo la Mivumoni Madale kwenye maduka yanayofahamika kama maduka 11, majambazi hao walivamia na kupora kwenye maduka sita.
Neema Charles, muuzaji wa Super Market, alisema akiwa anahudumia wateja alishangaa baada ya watu watatu kuingia na kumrudisha mteja aliyekuwa anatoka ndani na kutoa amri ya watu wote kulala chini na kutoa fedha na simu.
“Kati ya watu watatu walioingia ndani mmoja alivaa kininja akaficha sura, alikuwa na bunduki aliyotumia kupiga watu, walipora simu, pochi, fedha za mauzo na fedha zetu binafsi…nilikuwa na Sh. 250,000 kwenye pochi zimekwenda,” alisema.
Alisema walipekua kila mahali na kupora fedha, simu na pochi huku wakiwatolea lugha ya matusi na kuwataka kila mmoja kunyamaza kimya.
Alisema wakati wanaendelea na kupekua, aliwaangalia na ndipo alichomwa na kitu chenye ncha kali karibu na bega la mkono wa kulia na baada ya kupora walikwenda kwenye maduka mengine na tukio hilo lililochukua dakika 20.
Poni Abdalah, mmiliki wa saluni ya kike, alisema alikuwa anahudumia wateja sita na watoto wanne, mara aliingia mtu mmoja na kuwataka kukaa kimya na kutotoka nje. 
“Wakati anatoa amri hiyo mmoja wa wateja alikuwa na mwanaye aliyetoka nje akatoka kumfuata, alivutwa na kusukumwa ndani na tulikaa kimya baada ya kujua tumevamiwa,” alisema.
Alisema jirani yake kuna maduka ya M -pesa na Tigo-pesa nayo yaliporwa kiasi cha Sh. milioni 1.5, na kuwafungia ndani na kuondoka na funguo. Alifafanua kuwa baada ya majambazi kuondoka iliwabidi wavunje mlango ili kumtoa muuzaji aliyefungiwa ndani. 
“Baada ya kuona bibi aliyekuwa mteja kwenye duka langu kaporwa simu, nilizima taa ya dukani na kukaa kimya ikawa pona yangu, baada ya dakika 20 nikatoka nje nikakutana na dada mmoja ambaye alikuwa mteja kwenye duka la dawa amenyang’anywa funguo wa gari yake na watu hao,” alisema Amos Joseph.
Katika eneo la Tegeta, mtaa wa Tegeta Ndevu, Mariamu William, alisema majambazi hayo yalifika dukani humo kama wateja na kumtaka kaka yake, Emmanuel William, muuzaji kutoa fedha huku wakiwa wamemshikia bunduki.
“Kabla ya kuamuru wenye maduka kuwapa fedha walipiga risasi mbili hewani, alivyokuwa anachelewa kuwapa walichotaka walimpiga na kitako cha bunduki,” alisema. 
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema kuwa maduka yaliyoporwa ni matatu katika eneo la Madale mawili na moja ni eneo la Tegeta Kibaoni ambayo yaliporwa kiasi cha Sh. 300,000.
Wambura alisema hana taarifa za kuporwa maduka 11 na kuongeza kuwa polisi wanaendelea kuwasaka majambazi hayo.
MWANAMKE ABAMBWA NA SARE ZA JESHI JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata mwanamke aliyefahamika kwa jina la Saida Mohamed (30), mkazi wa Mwasonga Kigamboni akiwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Kamanda wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema jana kuwa mwanamke huyo alikamatwa juzi saa 4:00 asubuhi eneo la Mwasonga Kigamboni, wilayani Temeke.
Kova alisema, mwanamke huyo alikuwa na sare za jeshi hilo ambazo ni suruali saba za kombati, mashati saba ya kombati, kofia 10 za kombati, mashati mawili mepesi, fulana mbili, kofia aina ya bereti moja, viatu jozi tatu, ponjoo moja, koti moja, begi moja la kuwekea nguo za kipolisi pamoja na mikanda miwili ya kijeshi.
Aidha, Kamanda Kova alisema mwanamke huyo anaendelea kushikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano.
Katika tukio lingine, watu wawili wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kukutwa na mihuri 27 na nyaraka mbalimbali za serikali pamoja na za taasisi binafsi wakizitumia kufanyia utapeli kwa wananchi.
Kova aliwataja watu hao kuwa ni Sadraki Mwangwi (27), mkazi wa Mbagala Sabasaba na Samuel Mwangwi (38), mkazi wa Kimara Baruti.
Alisema, waliwakamata watu hao wakiwa na nyaraka hizo wakizitumia kuwatapeli wananchi wa sehemu mbalimbali jijini wakiwa wanakata risiti za serikali kama vile bima za magari, risiti za benki, manispaa na halimashauri. Aliongeza kuwa watu hao walikuwa kama mawakala wa kutoa risiti ambazo wananchi walizihitaji kwa bei yoyote ile. 
Kova alisema katika msako huo walifanikiwa kuwakamata watu 120 kwa makosa mbalimbali na kusema msako huo ni endelevu.
CHANZO: NIPASHE