Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Friday, November 16, 2012

Kamanda wa Boko Haram auawa Nigeria



Kamanda wa Boko Haram auawa NigeriaKamanda mmoja wa wapiganaji wa kundi la Boko Haram ameuawa katika shambulizi lililofanywa na jeshi la serikali ya Nigeria.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Nigeria imesema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kumuua Ibn Saleh Ibrahim aliyekuwa mmoja wa makamanda wa kundi la Boko Haram katika shambulizi lililofanyika kwenye mji wa Maiduguri. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa watu wengine kadhaa waliokuwa pamoja na Bin Saleh Ibrahim pia wameuawa katika operesheni hiyo.
Jeshi la Nigeria limesema kuwa Saleh Ibrahim alihusika na mauaji ya jenerali mstaafu Mamman Shuwa ambaye alikuwa mmoja wa mashujaa wa vita vya ndani nchini Nigeria katika miaka ya 60. Kiwango kikubwa cha silaha pia kimekamatwa katika operesheni hiyo.
Kundi la Boko Haram linahusika na machafuko ya sasa ya Nigeria hususan katika majimbo ya kaskazini mwa nchi hiyo na limetuhumiwa kuhusika na mauaji ya mamia ya watu tangu mwezi Julai mwaka 2009.

Thursday, November 15, 2012

Pillay: Waasi wa Kongo waua watoto 83


Pillay: Waasi wa Kongo waua watoto 83Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, makundi yanayobeba silaha katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamewaua karibu watu 300 wakiwemo watoto 83 kati ya mwezi Aprili na Septemba mwaka huu kinyume cha sheria katika jimbo la Kivu Kaskazini. Navanethem "Navi" Pillay Mkuu wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema kuwa, makundi hayo yamefanya zaidi ya mashambulio 75 kwenye vijiji mbalimbali vya jimbo hilo lililogubikwa na machafuko na kuwaua watu 264 wakiwemo watoto 83. Pillay ameongeza kuwa, kumeshuhudiwa vitendo vya ukiukaji haki za binadamu na mauaji ya makumi ya wananchi wa eneo hilo katika miezi ya hivi karibuni. Mkuu wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ameitaka serikali ya Kongo kuchukua hatua za haraka za kuwalinda raia wa eneo hilo na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wote ili kuzuia kuendelezwa jinai katika eneo hilo.

Wabunge wapinga kupelekwa jeshi Samburu



Wabunge wapinga kupelekwa jeshi Samburu
Wabunge kadhaa nchini Kenya wamesema kuwa, hatua ya Rais Mwai Kibaki ya kuamuru kupelekwa jeshi katika eneo la Samburu ni kinyume cha sharia na ni ukiukaji wa katiba. Wabunge John Munyes, Josephat Nanok na Ekwe Ethuro wamesema kuwa Rais Kibaki hakuomba ridhaa ya bunge kabla ya kuamuru jeshi kupelekwa Samburu kukabiliana na majangili waliowaua maafisa 40 wa polisi mwanzoni mwa wiki hii. Wabunge hao wamesema tayari agizo hilo la rais limesababisha kuweko kwa hali ya wasiwasi na huenda zoezi la kuwaandikisha wapiga kura linalotarajiwa kuanza wiki ijayo likaathiriwa pakubwa.

Ugonjwa wa Ebola waripuka tena Uganda



Ugonjwa wa Ebola waripuka tena Uganda
Waziri wa Afya wa Uganda, Christine Ondoa ametangaza kuwa, watu 2 wamefariki dunia baada ya kutokea mripuko mpya wa ugonjwa wa Ebola katika eneo la Luweero, nje kidogo ya mji mkuu Kampala. Waziri Ondoa amesema kuwa hatua za tahadhari zimechukuliwa ili kukabiliana na hali hiyo. Amewataka wananchi kuepuka mikusanyiko ya watu wengi kutokana na ukweli kwamba ugonjwa huo unaenea kwa kasi hususan katika maeneo yenye watu wengi.

Helkopta ya kijeshi yaanguka nchini Morocco

Helkopta ya kijeshi yaanguka nchini  Morocco Habari kutoka Guelmim kusini mwa Morocco zinasema kuwa, helikopta moja ya kijeshi imeanguka katika eneo hilo na kusababisha vifo vya wanajeshi 9. Habari zaidi zinasema wanajeshi wengine 2 wamejeruhiwa vibaya na wanaendelea kupata matibabu katika hospitali za karibu na eneo hilo. Wizara ya Ulinzi ya Morocco imesema huenda hali mbaya ya hewa ndiyo iliyosababisha ajali hiyo ingawa uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo chake. Mwaka uliopita takribani wanajeshi 80 walipoteza maisha yao katika eneo hilo la Guelmim  katika ajali mbaya ya ndege. Morocco ina kambi kubwa ya jeshi la wanaanga katika eneo hilo la kusini mwa nchi hiyo.

'Mashambulio ya Israel hayatadhoofisha irada ya Gaza'

'Mashambulio ya Israel hayatadhoofisha irada ya Gaza' Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina huko Ghaza amesema kuwa wakazi wa Ukanda wa Ghaza wako tayari kukabiliana na mashambulizi ya jeshi la utawala haramu wa Kizayuni. Ismail Hania amesema kuwa kushadidi mashambulizi ya utawala ghasibu wa Kizayuni huko Ghaza hakutadhoofisha azma na irada ya wakazi wa eneo hilo.

Hamas yasema Israel imejifungulia milango ya jahanam

Hamas yasema Israel imejifungulia milango ya jahanam
Brigedi ya Izzedin Qassam imetangaza kuwa utawala haramu wa Israel umejifungulia milango ya jahanam kwa kumuua shahidi kamanda wa brigedi hiyo Ahmed al Jabari katika hujuma huko Ukanda wa Ghaza. Jibril ambaye alikuwa kamanda wa Brigedi ya Izzedin Qassam Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu Palestina, Hamas ameuawa shahidi Jumatano ya leo katika hujuma zinazoendelezwa na utawala haramu wa Israel huko Ghaza.

Wednesday, November 14, 2012

Kiongozi Muadhamu akosoa uhuru wa Kimagharibi



Kiongozi Muadhamu akosoa uhuru wa KimagharibiKiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amekosoa mfumo wa uhuru wa Kimagharibi ambao umepelekea kuibuka ubaguzi, utumizi mabavu na sera za kivita.
Ayatullah Khamenei amefafanua zaidi kuhusu kesi za uhuru wa Kimagharibi na kusema kwa mfano 'uhuru wa kiuchumi' huko Magharibi unapelekea kuibuka mfumo unaowapa faida watu wachache. Pia ameashiria 'uhuru wa kisiasa' katika nchi za Magharibi' ambao umepelekea kuhodhiwa madaraka na makundi mawili ya kisiasa. Halikadhalika ameashiria 'uhuru katika masuala ya kimaadili' huko Magharibi jambo ambalo limepelekea kudhihiri ufisadi wa kimagharibi.

Misri yasisitiza kutatuliwa kadhia ya Palestina



Misri yasisitiza kutatuliwa kadhia ya Palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesisitizia udharura wa kutafutwa suluhisho la mwisho la mgogoro wa Palestina. Muhammad Kamal Amru amesema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa kwanza kati ya kundi la Misri na Ulaya mjini Cairo.
Amesisitiza kadhia ya Palestina kutafutiwa suluhisho la mwisho, suala la kwanza likiwa kurejea wakimbizi wa Palestina katika ardhi yao ukiwemo mji wa Quds na katika maeneo ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri aidha ametaka kuheshimiwa dini, uhuru wa kutoa maoni na pia kukabiliana na vitendo vya kuvunjia heshima viongozi na dini za mbinguni.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina amesema, viongozi wa Misri walioingia madarakani baada ya mapinduzi ya wananchi wanapinga mashambulizi mapya dhidi ya Gaza.
Haniya ameongeza kuwa, iwapo Israel isingeungwa mkono na Marekani na nchi za Kiarabu na kama nchi hizo zisingenyamazia kimya jinai za utawala huo huko Ghaza, basi Tel Aviv isingethubutu kuushambulia ukanda huo.

UN yataka kusitishwa machafuko Myanmar



UN yataka kusitishwa machafuko Myanmar
Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Myanmar kusitisha mara moja machafuko nchini humo. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kutiwa wasiwasi na kuendelea machafuko huko Myanmar na kuitaka serikali ya nchi hiyo kukomesha haraka iwezekanavyo mashambulizi dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. Martin Nisirky msemaji wa Ban Ki Moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameashiria hali ngumu inayowakabili wakimbizi wa Kiislamu wa Myanmar na kueleza kuwa Umoja wa Mataifa unaitaka serikali ya nchi hiyo kusitisha mara moja mashambulizi dhidi ya Waislamu na kuzingatia hali ya Waislamu wa nchi hiyo. Nisirky amesema hali ni ya kutia wasiwasi huko katika mkoa wa Rakhine na maelfu ya watu wameamua kuukimbia mkoa huo kupitia njia ya majini na kwamba wamepata ripoti mbaya kuhusu hali za watu hao.

107 wafariki kwa homa ya manjano Darfur, Sudan



107 wafariki kwa homa ya manjano Darfur, Sudan
Mripuko wa homa ya manjano huko katika jimbo la Darfur nchini Sudan umeua watu 107 katika kipindi cha wiki sita zilizopita. Hayo yameripotiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kutahadharisha kwamba ugonjwa huo huenda ukaenea kote nchini Sudan. WHO imesema kuwa homa hiyo ya manjano inazidi kuua watu wengi na kwamba Sudan hivi sasa inafanya juhudi za kupata chanjo ya dharura ya maradhi hayo. Maafisa wa WHO waliripoti kuwa jumla ya watu 67 wamefariki dunia kwa maradhi hayo ya homa ya manjano. Hakuna dawa maalumu kwa ugonjwa wa homa ya manjano inayoenezwa na mbu, bali daktari humhudumia mgonjwa kulingana na dalili kuu anazokuwa nazo kama vile  kuwa na upungufu wa maji mwilini, homa, kuvuja damu na kutapika. Dakta Ansu Banerjee wa Ofisi ya WHO huko Sudan amesema kuwa jumla ya dozi milioni 2.4 za chanjo ya homa ya manjano zinatazamiwa kuwasili Khartoum mji mkuu wa Sudan wiki ijayo.

Mauritania yaonya athari za uingiliaji kijeshi Mali



Mauritania yaonya athari za uingiliaji kijeshi Mali
Spika wa bunge la Mauritania amesema kuwa uingiliaji kijeshi huko Mali kwa ajili ya kukabiliana na makundi yanayobeba silaha  huko kaskazini mwa nchi utakuwa na mripuko mkubwa wa volcano kwa eneo zima la  sawa Sahel la Afrika. Masoud Ould Bilkhair Spika wa bunge la Mauritania amesema kuwa vita dhidi ya makundi  yenye silaha huko kaskazini mwa Mali vitakuwa na atahari mbaya kwa nchi jirani na Mali. Spika wa bunge la Mauritania amesisitiza kuwa viongozi wa Bamako wanapasa kwanza kufanya juhudi ili kuutatua kwa amani mgogoro wa kaskazini mwa nchi hiyo ilikuweza kulinda umoja wa ardhi nzima  ya Mali na kudumisha demokrasia nchini humo.