Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Monday, October 7, 2013

PICHA:DALADALA LILILOBEBA WANAFUNZI LAPATA AJALI MBAYA,WANAFUNZI WANUSURIKA


 Askari wa usalama barabarani wakijipanga kutoa huduma baada ya basi la daladala lililokuwa limebeba wanafunzi takriban 50 wa shule ya msingi ya Mgulani kugongana na gari dogo aina ya RAV 4 na kupinduka katika makutano ya Kenyatta Avenue na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es salaam jana  jioni.

 Dereva wa gari dogo akiwa na mtoto wa umri wa takriban miaka mitatu walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali. Wanafunzi wote walinusurika.
 Uharibifu wa miundumbinu baada ya ajali hiyo
 Askari wa usalama barabarani wakiondoa mabegi ya wanafunzi hao ambao walitafutiwa basi lingine kuwapeleka hospitali kwa uchunguzi zaidi
 Wanafunzi wakiwa katika gari walilotafutiwa baada ya ajali hiyo
 Magari ya break-down yakifanya juhudi ya kunyanyua basi hilo

LADY MADONNA AANZA KUJIFUNZA QURANI, NI BAADA YA KUWA NA MAHUSIANO NA KIJANA WA KIISLAMU

Mwanamuziki nyota muziki wa POP duniani Lady madonna
anasema kwa sasa anajifunza kitabu kitukufu cha Qurani na Uislamu.

Madonna ambaye ni mfuasi wa dini ya kiyahudi ya dhehebu la Kabbalah kwa sasa ana mahusiano na mwanaume wa kiislamu Brahim Zaibat ambaye amekuwa chachu ya kuanza kujifunza uislamu.
 

Akizungumza na gazeti la Bazaar Harper alisema Madonna
"Najenga shule kwa ajili ya wasichana katika nchi za kiislamu na nasoma Qurani. Nadhani ni muhimu kusoma vitabu vitakatifu". Madonna amekuwa mfuasi wa dhehebu la Kabbalah tangu mwaka 1996 wakati alipoolewa na mwingereza Guy Ritchie. 


Imeripotiwa kwamba Madonna mwenye umri wa miaka 55, ameanza kujifunza kuhusu uislamu kwa sababu ya mahusiano yake na Brahim Zaibat mwenye umri wa miaka 25. Madonna ambaye amebadilika mno kitabia wengi wanaamini huenda baadae akasilimu.

RIPOTI KAMILI YA WALIOKAMATWA WAKIJIFUNZA UGAIDI HII LEO,MAJINA YAO NA VYOTE WALIVYOKAMATWA NAVYO HIVI HAPA

Kamanda Zellothe Stephen akionesha CD za mafunzo ya kijeshi zilizokuwa zinatumiwa na kundi hilo.

Na Abdallah Bakari, Mtwara — POLISI mkoani Mtwara inawashikilia watu 11 kwa tuhuma za kupata mafunzo ya kijeshi msituni kwa kutumia CDs za al-Shabaab.
Tukio hilo la aina yake limetokea katika mlima Makolionga wilaya ya Nanyumbu mkoani hapa ambapo pia CDs zenye mafunzo mbalimbali ya kijeshi 25 zimekamatwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen ameuambia “mtandao wa Kusini Leo” kuwa watuhumiwa hao
walikamatwa wiki moja iliyopita baada ya jeshi lake kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema: “CD hizo zilikuwa zinatoa mafunzo ya Al-Shabaab ya kuchinja watu, Mauaji wa Osama Bin Laden, Zindukeni Zanzibar, Kuandaa Majeshi, Mauaji wa Idd Amin na Mogadishu Sniper,” alisema Stephen.
Alisema watuhumiwa wote ni wakazi wa wilaya ya Nanyumbu mkoani hapa na kwamba walikuwa wakiongoza na Mohamed Makande 39, mkazi wa kijiji cha Sengenya ambaye pia anashikiliwa na jeshi hilo.
Aliwataja wengine waliokamatwa kuwani Hassan Omary (39) mkazi wa kijiji cha Nanyulu, Rashid Ismail (27). Abdallah Y. Hamisi (32), Salum Wadi (38), Fadhili Rajabu (20), Abbas Muhidini (32), Ismail Chande (18), Said Mawazo, Issa Abeid (21), na Ramadhani Issa (26) wote wakazi wa kijiji cha Likokona.
Kuhusu vitu watuhumiwa walivyokamatwa navyo, Kamanda Zelothe alisema, “Tumekamata mapanga mawili, Deki ya DVD, Solar, Visu, Tochi, Betri, Simu za kiganjani 5, Vyombo mbalimbali vya kulia chakula, Baiskeli tatu, Vitabu mbalimbali wa dini ya Kiislam, Unga wa mahindi kilo 50, Mahidi kilo 150 na virago vya kulalia. Vingine ni mfuko wa kijani unaosadikiwa ni wa kijeshi wenye nembo ya nanga ya meli yenye mistari kulia na kushoto na nyoka katikati.”
Alisema jeshi lake licha ya kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, linaendelea na uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na Polisi Makao Makuu kwa lengo la kufanikisha kuunasa mtandao mzima.

Sunday, October 6, 2013

Magaidi waendelea kumwaga damu za raia nchini Iraq


Magaidi waendelea kumwaga damu za raia nchini Iraq
Wafanya ziara wasiopungua watano wameuliwa leo na wengine wasiopungua 17 wamejeruhiwa katika eneo la Qahira kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad baada ya gaidi mmoja kujiripua ndani ya msafara wa wafanya ziara hao waliokuwa wakielekea kwenye haram ya Imam Muhammad Al- Jawad AS kuomboleza siku aliyouliwa shahidi Imamu huyo wa tisa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Wakati huohuo wanafunzi 14 pamoja na mwalimu wao mkuu wameuliwa katika shambulio jengine la kigaidi lililofanywa leo pia ndani ya uwanja wa shule moja ya msingi huko kaskazini mwa Iraq. Lori lililosheheni mada za miripuko liliingizwa na kuripuka ndani ya uwanja wa kuchezea watoto wa shule moja ya msingi katika mji wa Tel Afar ulioko kilomita 70 kaskazini magharibi mwa wa Mosul na kusababisha vifo vya watoto hao pamoja na mwalimu wao mkuu. Zaidi ya watu elfu sita wameuawa nchini Iraq tangu ulipoanza mwaka huu wa 2013, elfu moja kati yao wakiwa wamepoteza maisha katika mashambulio ya kigaidi yaliyofanywa nchini humo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tu uliopita wa Septemba. Hapo jana watu wasiopungua 60 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika milipuko miwili iliyolenga Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa wakienda kuzuru haram tukufu ya Imam Jawad AS katika viunga vya mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Mabudha waendelea kuwatesa Waislamu Myanmar


Mabudha waendelea kuwatesa Waislamu Myanmar
Mabudha wenye misimamo mikali wanaendelea kuwatesa na kuwanyanyasa Waislamu wa Myanmar huku serikali ya nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia ikionekana kuwatelekeza Waislamu hao. Leo Jumapili vyombo vya habari vimeripoti kuwa, makundi ya Mabudha wenye chuki za kidini wamevamia nyumba tano za Waislamu katika mji wa Kyaung Gone, yapata kilomita 50, kaskazini magharibi mwa mji mkuu Yangon na kuzichoma moto nyumba hizo. Vyombo vya habari vya serikali vimedai kuwa polisi wamewatia mbaroni Mabudha 40 kwa kushambulia nyumba za Waislamu. Polisi wanasema kuwa, tarehe 2 mwezi huu wa Oktoba, Waislamu watano wakiwemo wanaume wanne na mwanamke mmoja waliuliwa kikatili katika kijiji cha Thabyuchaing baada ya mamia ya Mabudha wenye misimamo mikali kuvamia kijiji hicho. Wiki iliyopita pia, bikizee mmoja aliuliwa kwenye eneo la Thandwe, katika jimbo la Rakhine baada ya zaidi ya Mabudha 700 kumiminika mitaani kuwasaka Waislamu na kuchoma moto nyumba zao. Mashirika ya haki za binaadamu yanailamumu serikali ya Myanmar kwa kudharau wajibu wake wa kuwalinda Waislamu.

15 wauawa 85 wajeruhiwa katika machafuko Misri


15 wauawa  85 wajeruhiwa katika machafuko Misri
Watu wasiopungua 15 wameuawa katika machafuko yaliyotokea leo nchini Misri katika maadhimisho ya mwaka wa 40 wa tangu yalipoanza mashambulizi ya Misri dhidi ya vikosi vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vya mwaka 1973.
Khaled al Khatib, mmoja wa maafisa wa Wizara ya Afya ya Misri amethibitisha habari hiyo. Saba kati ya watu hao wameuawa katika Medani ya Ramses mjini Cairo. Watu wengine 85 wamejeruhiwa katika machafuko yaliyotokea kwenye maeneo tofauti ya Misri.
Polisi wamewafyatulia risasi na mabomu ya kutoa machozi makundi ya watu waliokuwa wanaandamana huku wengine wakijaribu kuingia kwenye Medani ya Tahrir ambako maelfu ya watu wanaounga mkono jeshi la Misri walikuwa wamekusanyika kuadhimisha siku hiyo.
Huko Delga, kusini mwa Cairo, duru za hospitali zimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba polisi walifyatua risasi hai katikati ya kundi la watu waliokuwa wanarusha mawe, na kumuua mtu mmoja.
Watu wengine wameuliwa katika maeneo mengine yaliyoshuhudia machafuko nchini Misri.

BABA NA WANAWE WAWILI WAPIGWA RISASI WAKITOKA KUSALI MSIKITINI


Watu watatu inaoaminika ni baba na wanawe wawili wamepigwa risasi wakati wanatoka kusali swala ya ijumaa
katika msikiti wa Villiers-le-Bel commune, kaskazini mwa jiji
la paris kilomita 17.4 kutoka katikati ya mji huo, limeripoti gazeti la lugha ya kifaransa la La Parisien.
 

Uchunguzi wa awali unaonesha kwamba risasi nne ziliwapata watu hao na mshambulizii wa tukio hilo alifanikiwa kukimbia eneo la bila kujulikana.
 

Baba na mmoja wa watoto wake walijeruhiwa vibaya
kwa risasi na walikimbizwa katika hospitali ya Beaujon huko Clichy ambapo mwanawe mwingine alijeruhiwa kidogo na kupelekwa Hospitali ya jirani ya Gonesse commune kilomita moja na nusu toka msikitini hapo.

 
Polisi wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na bado wanamtafuta mshambulizi huyo.

 
Kwa miaka ya karibuni waislamu katika nchi za Ulaya wamekuwa katika kipindi kigumu cha kunyanyaswa, kupigwa, kuuliwa pamoja na kubaguliwa.


polisi wakiwa katika tukio hilo

MAREKANI YAISHAMBULIA AL SHABAB, YAMKAMATA KIONGOZI WA AL QAIDA LIBYA


Kundi la askari wa Jeshi la Majini la Marekani limefanya shambulizi katika pwani ya mji wa kusini mwa Somalia dhidi ya wapiganaji wa Al Shabab jana.

Shambulizi hilo limelenga kamanda wa ngazi za juu wa wanamgambo wa kundi hilo la Al Shabab aliyetajwa kwa jina la Abu Siyad katika mji wa Baraawe. Afisa mmoja wa jeshi la Marekani amesema kundi hilo la wanamaji wa Marekani halikufanikiwa katika shambulizi hilo.

Maafisa wa Marekani wamesema kuwa shambulizi hilo lilipangwa wiki moja na nusu iliyopita na kwamba lilichochewa na hujuma iliyofanywa na wanamgambo wa Al Shabab dhidi ya jengo lenye maduka la Wastgate jijini Nairobi mwezi uliopita.

Msemaji wa kundi la al Shabab Abdulaziz Abu Musab amesema makomando wa kigeni wamevamia pwani ya mji wa Baraawe kwa kutumia boti mbili za kasi kubwa na kwamba hawakufanikiwa kufikia malengo yao. Amesema askari wa Marekani walilazimika kukimbia baada ya kukabiliwa na mashambulizi makali ya al Shabab.


Habari zinasema mji huo  unaolindwa na wapiganaji wa al-Shabaab ulishambuliwa kutoka baharini katika mapambano yaliyodumu zaidi ya saa moja. Radio ya Mogadishu imesema shambulizi hilo lilitekelezwa jana usiku kwa ndege za kigeni. 

Mji wa Barawe ambao uko kilomita 250 kusini mwa mji wa Mogadishu, umekuwa ukidhibitiwa na wapiganaji wa al-Shabaab kwa miaka kadhaa na umekuwa ukishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa vikosi vya kigeni.

Marekani imepanga kufanya mashambulizi katika pwani ya Afrika mashariki na Libya kwa madai ya kuwatafuta vinara wa ugaidi.Wakati huo huo taarifa zinasema shambulizi la Libya wamefanikiwa kumkamata kiongozi wa Al qaida nchini humo Abu Anas al Liby (أبو أنس الليبي) ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa tuhuma za kuhusika na ulipuaji wa mabomu mwaka 1998 katika nchi za Tanzania na Kenya ambapo watu 224 walikufa.

Marekani iliweka zawadi ya dola milioni 5 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa za kukamatwa kwake.





Friday, October 4, 2013

Mauaji Ya Mhubiri Ibrahim Rogo Yazua Tandabelua

VIDEO:MSIKILIZE SHEKH SALIM ABD ALIYENUSULIKA KWENYE TUKIO LA MAUAJI YA IBRAHIM ROGO PAMOJA NA WENZAKE

Sheikh Ibrahim Rogo na wenzake 3 wauawa Kenya


Sheikh Ibrahim Rogo na wenzake 3 wauawa Kenya
Polisi ya Kenya imetangaza kuwa, watu wanne akiwemo Sheikh Ibrahim Ismail Rogo wameuawa baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana ndani ya gari dogo jana usiku huko mjini Mombasa. Taarifa ya Polisi  ya Kenya imeeleza,  Sheikh Ibrahim Rogo alikuwa mrithi wa Sheikh Aboud Rogo ambaye  naye aliuawa na familia yake kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwezi Agosti 2012. Mauaji ya Sheikh Ibrahim Rogo ambayo yameutikisa mji wa Mombasa, yametokea  baada ya kupita takriban wiki mbili tokea kundi la al Shabab lilipovamia  na kuua  watu wasiopungua 63 na kujeruhi mamia ya wengine kwenye jengo la maduka ya biashara la Westgate jijini Nairobi. Baadhi ya wananchi wa Mombasa wanakituhumu kikosi  maalumu cha kupambana na ugaidi kuwa ndicho kilichotekeleza  mauaji hayo. Sheikh Ibrahim Rogo ambaye alikuwa akitoa mihadhara kwenye Msikiti wa Musa mjini Mombasa alituhumiwa na jeshi la polisi kuwa anawachochea vijana wa Kiislamu kujitumbukiza kwenye makundi  ya kigaidi. Polisi ya Kenya imesema kuwa, Gaddafi Mohammad, Issa Abdallah  na Omar Abu Rumeisa ni miongoni mwa waliouawa, naye Salim Aboud alinusurika kwenye shambulio hilo.

Wamarekani walalamikia likizo zisizo na malipo


Wamarekani walalamikia likizo zisizo na malipo
Wafanyakazi wasiopungua milioni moja wa serikali ya shirikisho ya Marekani wamelalamikia hatua ya nchi hiyo ya kuwapa likizo bila ya mishahara yao. Taarifa zinasema kuwa, wafanyakazi hao wamelalamikia vikali hatua ya kuendelea kubaki  nyumbani kwa siku ya nne mfululizo bila ya kulipwa mishahara yao na wanataka warejeshwe kazini haraka iwezekanavyo. Fikra za walio wengi na wafanyakazi nchini humo wanajihesabu kuwa ni mateka na wahanga wa mivutano ya kisiasa ndani ya Baraza la Kongresi. Hapo jana, Rais Barack Obama wa Marekani alisisitiza kuwa kuendelea kusimamishwa idara za shirikisho ni pigo kubwa kwa nchi na uchumi wa Marekani. Taarifa zinasema kuwa, thuluthi mbili ya wafanyakazi wa serikali akiwemo Obama mwenyewe, watalazimika kufanya kazi bila ya malipo hadi mgogoro wa bajeti kati ya Warepublican na Wademokrat utakapotatuliwa. Wademokrat na Warepublican wanazozana juu ya miswada iliyopendekezwa  na serikali ya Obama juu ya marekebisho ya bima ya afya.