Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Wednesday, November 27, 2013

WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR IMESHAURIWA KUWEKA MIONGOZO ITAKAOWAFANYA WAMILIKI WA VYUO VYA UALIMU KUSAJILI VYUO VYAO.



WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR IMESHAURIWA KUWEKA MIONGOZO ITAKAOWAFANYA WAMILIKI WA VYUO VYA UALIMU KUSAJILI VYUO VYAO.

MWENYEKITI WA JUMUIYA YA MAENDELEO YA ELIMU ZANZIBAR ZEDO BWANA USSI SAID SULEIMAN, AMEISHAURI SERIKALI KUPITIA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR KUWEKA MIONGOZO ITAKAYOWAWEZESHA WAMILIKI WA VYUO VYA UALIMU VYA BINAFSI KUSAJILI VYUO VYAO.
USHAURI HUO AMEUTOA ALIPOKUWA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI HUKO OFISINI KWAKE JADIDA WETE MKOA WA KASKAZINI PEMBA.
MWENYEKITI HUYO AMESEMA UAMUZI WA HIVI KARIBUNI WA WIZARA YA ELIMU KUFUNGA VYUO VYOTE VYA BINAFSI VINAVYOENDESHA MAFUNZO YA UALIMU WA MAANDALIZI HAUKUWA SAHIHI KWANI VYUO NA TAASISI ZA BINAFSI NCHINI ZINASAIDIA SANA KUTOA FURSA MBALI MBALI ZA AJIRA KWA VIJANA.
KUFANYA HIVYO ITAPELEKEA VIJANA WENGI KUTEGEMEA AJIRA SERIKALINI.
MWENYEKITI USSI AMBAE PIA NI MKUU WA CHUO CHA ZANZIBAR EDUCATION COLLEGE AMESEMA NI VYEMA KWA SERIKALI KULIANGALIA KWA KINA SUALA HILO KWANI LINAWEZA KULETA ATHARI KUBWA KWA TAIFA LETU.
TAASISI ZA BINAFSI ZIMEKUWA ZIKITOA MCHANGO MKUBWA KWA SERIKALI HIVYO WIZARA YA ELIMU INAPASWA KUWEKA MIONGOZO MAALUM ITAKAYOWAFANYA WAMILIKI WA VYUO VYA BINAFSI KUSAJILI VYUO VYAO.
NDUGU USSI AKIFAFANUA SABABU ZINAZOWAFANYA VIJANA KUJIINGIZA KATIKA WIMBI LA MADAWA YA KULEVYA, WIZI NA UASHARATI NI UKOSEFU WA AJIRA HIVYO VIJANA HUAMUA KUJIINGIZA KATIKA MATENDO MAOVU.
KUENDELEA KUWA NA CHUO KIMOJA TU AMBACHO KINATOA MAFUNZO YA UALIMU HAPA ZANZIBAR NI KUDUMAZA MAENDELEO YA VIJANA WETU NA TAIFA KWA UJUMLA.
KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU WAKATI UMEFIKA SASA KWA WIZARA KUTOA VIBALI KWA TAASISI BINAFSI KUENDESHA MAFUNZO YA UALIMU HAPA NCHINI.
AIDHA NDUGU USSI SAID SULEIMAN AMEWAPONGEZA SANA MHESHIMIWA WAZIRI WA ELIMU NA NAIBU WAKE MHESHIMIWA ZAHRA KWA KAZI NZITO YA KUTAKA KULETA MABADILIKO MAKUBWA YA ELIMU NCHINI INGAWA VIONGOZI HAO WANAKABILIWA NA CHANGAMOTO NYINGI SANA.

Wednesday, November 20, 2013

OIC yaunga mkono natija ya kikao cha Kuwait


OIC yaunga mkono natija ya kikao cha KuwaitNaibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amesema kuwa jumuia hiyo inaunga mkono maamuzi na maazimio yaliyofikiwa katika kikao cha wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiafrika huko Kuwait. Samir Bakr Diab ameeleza kuwa OIC inaunga mkono maamuzi na maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho cha Kuwait khususan katika uwanja wa mapatano ya kibiashara kati ya nchi za Kiarabu na Kiafrika na kuondolewa vizuizi vilivyopo katika uwanja huo.
Akizungumza katika kikao cha tatu cha wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiafrika huko Kuwait kwa niaba ya Ikmaluddin Ehsanoghlo Katibu Mkuu wa OIC, Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Samir Bakr Diab amesema kuwa taasisi hiyo imeanzisha mfuko wa maendeleo ya mshikamano wa Kiislamu wenye mtaji wa dola bilioni kumi ili kuzisaidia taasisi mbalimbali za kibiashara za nchi wanachama wa jumuiya hiyo.  

Wairani 6 wauawa katika mlipuko wa Beirut


Wairani 6 wauawa katika mlipuko wa BeirutUbalozi wa Iran nchini Lebanon umetangaza kwamba raia 6 wa Kiirani ni miongoni mwa watu waliouawa katika milipuko iliyotokea nje ya jengo la ubalozi wa Iran mjini Beirut hapo jana. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Wairani hao ni Hojatulaislam Ibrahim Ansari afisa wa Kitengo cha Utamaduni cha Iran, mke wa mwanadiplomasia wa Iran pamoja na maafisa wanne wa usalama kwenye ubalozi huo.
Milipuko hiyo miwili iliyotokea nje ya ubalozi wa Iran mjini Beirut imepelekea watu wasiopungua 23 kuuawa na wengine 140 kujeruhiwa. Kundi la kigaidi la brigedia ya Abdullah Azzam lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limetangaza kuhusika na milipuko hiyo. Rais Michel Suleiman wa Lebanon amelaani milipuko hiyo na kusema kuwa serikali yake itafanya kila iwezalo kuwasaka waliohusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

Sultani Makenga kupewa hifadhi nchini Uganda


Sultani Makenga kupewa hifadhi nchini Uganda
Afisa mmoja wa vyombo vya usalama vya Uganda amearifu kuwa Sultani Makenga mmoja wa makamanda wa waasi wa M23 aliyekimbilia nchini humo atapewa hifadhi. Afisa huyo ameeleza kwamba, kamanda huyo alikimbilia Uganda baada ya kushindwa waasi hao huko mashariki mwa Kongo na kwamba kwa sasa anashikiliwa na jeshi la UPDF. Ameongeza kuwa, kutokana na sababu za kiuslama serikali ya Kampala haitotangaza mahali alipo Sultani Makenga. Makenga anatuhumiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufanya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Serikali ya Kampala imetangaza kuwa waasi 1,000 wameingia nchini humo kupitia mipaka ya magharibi mwa Uganda baada ya kushindwa katika mapigano na vikosi vya Kongo vilivyokuwa vikisaidiwa na askari wa Umoja wa Mataifa. Uganda inayotuhumiwa na Kongo kuwaunga mkono waasi wa M23 imesema kuwa, haiko tayari kuwarejesha nyumbani waasi hao.

Mugabe asema Zimbabwe si koloni la Uingereza


Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe 
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amesema kuwa, nchi ya Zimbabwe si koloni la Uingereza. Akiwahutubia wanachuo wa vyuo vikuu katika mji Mkuu Harare hapo jana, Mugabe alieleza kuwa wananchi wa Zimbabwe ijapokuwa wanazungumza vizuri na kwa ufasaha lugha ya Kiingereza lakini hawakoloniwi tena na Waingereza.
Huku akiwabeza wazungu na wakoloni wa zamani wa nchi hiyo Mugabe amesema kwamba, hawapaswi kuwapumbaza wananchi wa Zimbabwe ili kwa njia hiyo waweze kupora kikamilifu utajiri wa nchi hiyo. Aidha  sambamba na kueleza kuwa utamaduni wa kikoloni wa nchi za Magharibi umeingiza tamaduni za nje katika bara la Afrika Mugabe ameongeza kuwa, wazawa wa bara la Afrika wanatambua haki zao na kwamba wanastafidi vyema na mali asili na utajiri wao ambao kwa karne nyingi umekuwa ukiporwa na wakoloni.

Tuesday, November 19, 2013

Arab League yalaani machafuko nchini Libya


Arab League yalaani machafuko nchini Libya
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) amelaani vikali vitendo vya ukatili vilivyotokea Tripoli, mji mkuu wa Libya dhidi ya waandamanaji wasio na silaha. Mbali na Nabil al-Arab kulaani machafuko hayo ya hivi karibuni ya mjini Tripoli ambapo makumi ya waandamanaji waliuliwa na kujeruhiwa, amezitaka pande zote kuunga mkono juhudi za serikali na baraza la kongresi ya kitaifa nchini humo za kuikwamua nchi hiyo na hali mbaya iliyo nayo hivi sasa. Aidha al-Arab ameonyesha kusikitishwa kwake na matukio hayo na akaongeza kuwa, vitendo vya utumiaji mabavu nchini Libya vimefikia kiwango cha kutisha. Hii ni katika hali ambayo jana baadhi ya duru za habari ziliripoti kujiri mapigano yaliyowahusisha wakazi wa eneo la al-Shawkh huko Swalahu al-Din katika viunga vya mji mkuu Tripoli, na wanamgambo wenye silaha. Watu 47 waliuawa na wengine 500 kujeruhiwa baada ya makundi ya watu wenye silaha kuwamiminia risasi waandamanaji waliokuwa wakipinga vitendo vya utumiaji mabavu nchini humo.

Wanawake wa Ikhwan Muslimin kizimbani Misri


Wanawake wa Ikhwan Muslimin kizimbani MisriDuru za habari nchini Misri zimeripoti kuwa, kwa akali wanawake 15 na wasichana 7 wenye mahusiano na kundi la Ikhwanul Muslimiin, wanatazamiwa kupandishwa kizimbani, kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya kikatili katika maandamano yaliyopita nchini humo. Habari zinasema kuwa wanachama hao watapandishwa kizimbazi hapo kesho. Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu nchini Misri imetangaza kuwa, itawafikisha mahakamani wanawake hao ambao pia wanatajwa kuwa miongoni mwa wafuasi wa rais aliyeuzuliwa madarakani, Muhammad Mursi, kesho Jumatano, Novemba 20, ili kujibu tuhuma dhidi yao. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, wanawake hao walitiwa nguvuni mwishoni mwa mwezi uliopita wakituhumiwa kuhusika na machafuko yaliyotokea katika eneo la Rushdi mkoani Alexandria. Wasichana 7 kati ya watuhumiwa hao wanatajwa kuwa na umri kati ya miaka 18 na kuendelea na kwamba, wanaendelea kushikiliwa na vyombo vya dola nchini Misri.

Ash Shabab wahujumu kituo cha polisi Somalia


Ash Shabab wahujumu kituo cha polisi Somalia
Wanamgambo wa ash Shabab wamekishambulia kituo kimoja cha polisi katika mji wa Baladweyne kaskazini mwa Mogadishu mji mkuu wa Somalia na kuwafyatulia risasi maafisa na raia waliokuwemo ndani ya kituo hicho cha polsi na kusababisha vifo vya watu wasiopungua kumi. Kundi la ash Shabab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limedai kuhusika na mashambulizi hayo. 
Ufyatuaji risasi uliendelea nje ya kituo cha polisi cha Baladweyne karibu na mpaka na Ethiopia kwa masaa kadhaa.
Vikosi vya Somalia vikishirikiana na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa baadaye vilikizingira kituo hicho cha polisi na kuopambana na wanamgambo hao wa ash Shabab.
Abdiasis Abu Mus’ab, msemaji wa masuala ya kijeshi wa kundi la ash Shabab amedai kuwa wanamgambo wao wameua polisi 25 wa Somalia na wanajeshi 18 wa kulinda amani wa Djibouti katika shambulio hilo la leo huko Baladweyne.

'Hujuma ya kigaidi ya Beirut ni njama za Wazayuni'


'Hujuma ya kigaidi ya Beirut ni njama za Wazayuni'Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea mkabala na ubalozi wa Iran huko Beirut mji mkuu wa Lebanon ni njama za Wazyuni na vibaraka wao. Bi Marzieh Afkham amelaani mashambulizi hayo ya kigaidi yaliyotokea leo asubuhi huko Beirut mkabala na ubalozi wa Iran mjini humo na kusisitiza kuwa, jinai hiyo ni kitendo cha chuki na uadui kilichofanywa na Wazayuni na vibaraka wao.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kusikitishwa na kuuliwa shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa wa Lebanon na wa nchi za nje katika mashambulizi hayo ya kigaidi na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa mashambulizi hayo. Bi Afkham ameongeza kuwa kwa kuzingatia kwamba mripuko huo umetokea karibu na ubalozi wa Iran huko Beirut, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran inafuatilia suala hilo kwa makini na kwa juhudi maalumu na kwamba itatoa taarifa kamili katika uwanja huo. Watu wasiopungua 26 wameuliwa na wengine 150 kujeruhiwa katika mripuko huo.
Wakati huo huo mkuu wa idara ya utamaduni katika ubalozi wa Iran mjini Beirut Sheikh Ibrahim Ansari ameuawa shahidi katika mripuko huo. Habari hiyo imethibitishwa na kaimu waziri wa afya nchini Lebanon.

Monday, November 18, 2013

Naibu Mkuu wa shirika la ujasusi Libya atekwa nyara


Naibu Mkuu wa shirika la ujasusi Libya atekwa nyaraNaibu wa Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Libya ametekwa nyara akiwa pamoja na mmoja wa viongozi waliooongoza mapinduzi dhidi ya Kanali Muammar Gadafi nchini humo. Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, maafisa hao waandamizi wa Libya wametekwa nyara leo mjini Tripoli. Huku hayo yakiripotiwa, habari kutoka Tripoli, mji mkuu wa Libya zinasema kuwa, hali ya wasiwasi imerejea mjini humo baada ya kutulia kwa muda mfupi. Kwa siku mbili mfululizo mji huo umeshuhudia mapigano kati ya pande hasimu yaliyopelekea zaidi ya watu 40 kuuawa na karibu laki tano wengine kujeruhiwa. Leo wananchi wa Libya wameendelea kuwazika watu waliouawa, maziko ambayo yameambatana na maandamano ambapo wakazi wa mji huo wameitaka serikali dhaifu ya nchi hiyo ikabiliane vilivyo na wanamgambo wenye silaha. Wananchi hao wametishia kufanya uasi wa nchi nzima kama serikali na makundi yenye silaha yatashindwa kufikia makubaliano ya kurejesha amani katika nchi hiyo tajiri kwa mafuta ya kaskazini mwa Afrika. 

Wamisri wachoma moto picha za Erdogan na Qatar



Wamisri wachoma moto picha za Erdogan na Qatar
Waandamanaji wanaomuunga mkono Abdulfatah al Sisi, Waziri wa Ulinzi wa Misri wamezichoma moto picha za Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan na bendera ya nchi ya Qatar mjini Cairo, Misri. Waandamanaji hao waliokuwa wamekusanyika mbele ya ubalozi wa Uturuki mjini Cairo, wametaka pia kufukuzwa balozi wa Uturuki nchini kwao. Kabla ya hapo na katika kulalamikia matamshi ya viongozi wa Ankara, Cairo ilimuita balozi wa Uturuki nchini humo Hussein Own Butsali sambamba na kumuondoa balozi wake mjini Ankara. Mbali na hapo serikali ya Cairo ilitangaza kuwa, itachunguza uhusiano wake na Uturuki lakini ikatangaza kuwa, katika hali ya sasa haitamrejesha balozi wake nchini Uturuki. Nivyema kuashiria hapa kuwa, baada ya kuuzuliwa madarakani rais Muhammad Mursi wa Misri, Uturuki ambayo ilikuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa hatua hiyo, ilitangazi wazi wazi kwamba, inamtambua Mursi kuwa ndiye rais pekee wa kisheria wa nchi hiyo. Aidha mbali na hapo Ankara iliendelea kulaani hatua ya kuwekwa kizuizini mteja wao huyo sanjari na kusisitiza kutaka kurejeshwa kwake madarakani nchini Misri, suala ambalo lilizidi kupigilia msumari wa moto kwenye siasa za nchi mbili. Inasemekana pia kwamba, Qatar ambayo ni muungaji mkubwa wa Harakati ya Ikhwanul Muslimiin nchini Misri, ilikata misaada yake ya kifedha kwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika baada ya kung’olewa madarakani rais Muhammad Mursi.

Wahamiaji haramu 61 wakamatwa Italia


Wahamiaji haramu 61 wakamatwa Italia
Maafisa wa Italia wamewatia nguvuni wahamiaji haramu 61 katika kisiwa cha kusini mwa nchi hiyo. Kikosi cha ulinzi cha pwani ya Italia leo Jumatatu kimewatia mbaroni wahamiaji haramu 61 waliokuwa na lengo la kuingia katika kisiwa cha Lampedusa kusini mwa nchi hiyo. Kisiwa cha Lampedusa kinachopatikana kati ya kisiwa cha Sicily na Tunisia hutumiwa na makumi ya wahamiaji haramu  kutoka kaskazini mwa Afrika na eneo la Mashariki ya Kati kama njia ya kufika nchini Italia na katika nchi nyingine za Ulaya.
Wahamiaji haramu zaidi ya elfu 36 mwaka huu wameingia Italia wakitafuta hifadhi.