Sheikh Abdullah Saleh Al Farsy
(February 12, 1912
- November 9, 1982)
Mwanachuoni,
Mshairi, na Mwana historia maarufu kutoka Zanzibar
Imekusanywa
na Muhammad Faraj Salem
Al Saiy
Sifa zake
Alipofariki dunia
mwaka 1982 Sheikh Abdullah Saleh Al Farsy alikuwa bila shaka yoyote mwanachuoni
na mwana historia mkubwa wa Kiislamu na mmojawapo wa washairi wakubwa.
Atakumbukwa
daima kwa uso wake mkunjufu usioacha kutabasamu na kwa mwenenedo na tabia zake
njema. Wakati wote alikuwa akizungukwa na watu wanaotaka kumsalimia au kupata
kutoka kwake mafunzo ya Dini.
Umaarufu
wake ulikuwa si katika kisiwa cha Zanzibar na
nchi za Afrika ya Mashariki peke yake, bali ulienea hadi Somalia ya kusini na ya kaskazini, Cape Town upande wa kusini mpaka kufikia Malawi, mwahali alipokuwa akitoa darsi zake
kabla ya kuhamia Kenya kwa
kuhofia kukamatwa na serikali ya Zanzibar.
Alizaliwa
Zanzibar mwezi wa February mwaka 1912 katika ukoo maarufu, akajifunza Qur-aan
kutoka kwa Fatma Hamid Said (1854-1936), aliyesoma kwa Sheikh Amin bin Ahmed
aliyekuwa akifundisha Qur-aan kijiji cha Jongeani mahali alipozaliwa Sheikh
Abdullah Farsy na kukulia.
Sheikh
Abdullah Saleh Farsy alihifadhi Qur-aan yote pamoja na hadithi nyingi za Mtume
wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) akiwa na umri mdogo sana, na
shauku yake kubwa isiyotoshelezeka ya kujifunza masomo ya Kiislamu na ya
kiulimwengu ilionekana pale wenzake walipokuwa wakijishughulisha na michezo na
anasa za kidunia, wakati yeye alikuwa kila siku akizama katika kusoma kitabu
kipya cha mafunzo ya Kiislamu.
Alikuwa
akipenda sana
kusoma kiasi ambapo maisha yake yote yalifungika ndani ya maktaba 'library'
yake kubwa ya nyumbani.
Alipofariki
dunia, Sheikh Abdullah Saleh al-Farsy alikuwa Aalim mwenye kutambulika na
kuheshimika kupita wote katika nchi zinazotumia lugha ya Kiswahili. Mchango
wake usiokuwa na mfano katika kuelimisha watu dini ya Kiislamu ulifikia kiwango
chake cha juu baada ya kuchapicha tafsiri kamili ya mwanzo ya Qur-aan Takatifu
ya Kiswahili iliyokubaliwa rasmi yenye kurasa 807.
Elimu yake
Alipokuwa
kijana, mwanachuoni huyu mwenye hamasa na uhodari alibahatika wakati ule kuwepo
na kuenea kwa vyuo vikongwe vya Kiislamu vilivyojaa wanafunzi chini ya uongozi
wa Maulamaa weledi mfano wa Sheikh Abu Bakar bin Abdullah bin Bakathir
(1881-1943) aliyekuwa mwanafunzi maarufu wa Sayyid Ahmed bin Abu Bakar
al-Sumait (1961-1925)
Katika mwaka
wa 1922 Sheikh Abdullah Saleh Farsy alijiunga na chuo cha Msikiti Barza baada ya
Maulamaa wawili kumtaka afanya hivyo:
Wa kwanza alikuwa
Sayyid Hamid bin Mansab (1902-1965) aliyemfunza RISALATUL JAMI'A, yenye mafunzo
ya taasisi ya Kiislamu. Imamu huyu wa msikiti wa Forodhani aliyefariki dunia
wakati akitoa darsi ndani ya msikiti Gofu alikuwa mwanafunzi wa Sheikh Muhammad
Abdul Rahman Makhzymy (1877-1946), mmojawapo wa waalimu wa Sheikh Abdullah
Saleh Farsy.
Wa pili alikuwa
Sayyid Alawy bin Abdul Wahab (1902-1960) aliyemsomesha vitabu 12 vya Fiq'hi
katika lugha ya kiarabu pamoja na sharhi ya MARDFIN RABBIYYAH juu ya elimu ya
urithi.
Baada ya
kuwa mjuzi katika elimu ya taasisi ya Kiislamu katika chuo cha Msikiti Barza,
Sheikh Abdullah Saleh Farsy alikuwa mjuzi pia wa elimu ya nahau ya lugha ya
Kiarabu. Na alipokuwa na umri wa miaka 20 alikuwa akiandika mashairi ya
Kiarabu, dalili ya daraja kubwa ya elimu ambayo Maulamaa wa Zanzibar wakati ule waliweza kuieneza.
Sheikh
Abdullah Saleh Farsy alijifunza chini ya Maulamaa wengi wakubwa kama vile
Sheikh Ahmed bin Muhammad al-Mlomry (1873-1936) aliyemfundisha vitabu 25
vikiwemo Tafsiri ya Jalalayn kilichoandikwa na Jalal al-Din Mahali (1389-1450)
kutoka Misri na Jalal al-Din Suyuti (1445-1505), Syria, na hawa ni Maulamaa wakubwa
na maarufu wa madhehebu ya Imam Shafi.
Baada ya
kuhitimu darsi zote katika chuo cha Msikiti Barza, Sheikh Abdullah Saleh Farsy
aliruhusiwa na Sheikh Ahmed bin Muhammad al-Mlomry kusomesha katika chuo hicho
katika mwezi wa Ramadhan chini ya uangalizi wake.
Alijifunza
pia kutoka kwa Sheikh Abu Bakar (1881-1943), mtoto wa Sheikh Abdullah bin Abu
Bakar Bakathir (1860-1925), mwanafunzi wa Sheikh Ahmed bin Abu Bakar al-Sumait.
Sheikh Abu
Bakar bin Abdullah bin Bakathir aliyejifunza kutoka kwake elimu ya Fiq'hi
kupita Maulamaa wengi hapo Zanzibar, alikuwa akihudhuria darsi za Sheikh
Abdullah Saleh Farsy kwa ajili ya kumpa moyo, kisha akamchagua kuwa Imamu wa
Swalah ya Witri kutoka mwaka 1933 mpaka terehe 28 October 1939, alipomruhusu
pia kusoma Qur-aan katika Msikiti Gofu na hatimaye akawa anasalisha Swalah ya
Alfajiri mpaka mwaka 1966 alipochukuwa mahali pake mtoto wa dada yake Saleh bin
Salim bin Zagar.
Sheikh
Abdullah Saleh Farsy alisoma vitabu vingi vya Fiq'hi kutoka kwa Sheikh Muhammad
Abdul Rahman al-Makhzymy vikiwemo vitabu vya Fathul Muin na Iqnai, ambavyo
mwanzo vilikuwa vikisomeshwa na Sheikh Abdullah bin Abu Bakar bin Bakathir hapo
Msikiti Gofu katika mwaka 1917.
Alijifunza
kutoka kwake pia elimu ya kupanga nyakati za Swalah na kuujua upande wa Qiblah.
Juu ya kuwa
hapo mwanzo Sheikh Abdullah Saleh alisoma Minhaaj At Tabiiyn kitabu cha Sheikh
Zakariya Muhyddin Yahya Sharaff ad-Din al-Nawawi (1213-1277) ambaye ni
mwanachuoni mkubwa wa madhehebu ya Kishafi, lakini baadaye alisoma tena kitabu
hicho kwa Sheikh Muhammad Abdul Rahman al-Makhzymy.
Msimamo wa
kisheria wa kitabu hiki hapo Zanzibar umeanzia zama za Imam Abu Hamid bin
Muhammad al-Ghazzali (1058-1111), aliyekuwa mwanafunzi wa Imam wa Haramayn
Ahmed Malik al-Jawayti (1085) kutoka kwa Ayoub al-Buwati (845), mwanafunzi wa
Imam Muhammad Idriys al-Shafi'i (767-820), mwanzilishi wa Madrasa ya Shafi'i,
yenye wafuasi wengi Zanzibar na Misri.
Sheikh
Muhsin bin Ali bin Issa Barwan aliyekuwa mwalimu wake Msikiti Gofu, alikuwa
mwanachuoni wa mwanzo katika mwaka 1944 kumruhusu Sheikh Abdullah Saleh Farsy
kusomesha Jalalayn Msikiti Barza katika mwezi wa Ramadhani. Baadaye Sheikh
Abdullah Saleh Farsy alijifunza kwa Sheikh al-Amin Ali bin Abdullah bin Nafi
al-Mazrui mwaka (1875-1947), aliyeupendezesha kwa watu Uislamu wa kisasa kama ulivyoshereheshwa na Shekh Muhammad Abduh (1845-1905),
aliyemsomesha Sheikh Ahmed Muhammad Mlomry katika chuo kikuu cha al Azhar,
Misri.
Sheikh
Abdullah Saleh Farsy alipewa Ijaza (shahada) na Sheikh ‘Umar bin
Ahmad bin Abu Bakar al-Sumait (1896) aliyemsomesha vitabu vya Fiq'hi, Mantiq (Logic)
na Hadith, pamoja na vitabu vingine. Bahati mbaya mwanachuoni huyu alirudi Yemen katika mwaka wa 1965 kutokana na udikteta
uliokuwepo Zanzibar
chini ya serikali iliyoongozwa na mkiristo Julius Kambarage Nyerere.
Umahiri
aliouonyesha Sheikh Abdullah Saleh Farsy katika elimu ya mambo ya kidunia
ulikuwa mkubwa pia. Alikuwa hodari sana
katika elimu hiyo, na alipokuwa Central Primary School aliyojiunga nayo mwaka
1924, mwalimu wa lugha ya Kiingereza alishindwa kuamua darasa lipi ampeleke.
Sheikh Abdullah Saleh Farsy aliyemaliza miaka minane inayotakiwa katika shule
ya msingi katika muda wa miaka mitano tu.
Miongoni mwa
walimu wake maarufu alikuwa Sheikh Abdullah bin Ahmed bin Seif (1900-1940) na
Sheikh Abdul Bary kutoka chuo kikuu cha Al-Azhar aliyeajiriwa na Sayyid Ali bin
Humoud mwaka (1902-1911).
Qur-aan Takatiku
Aliandika
tafsiri yake ya Qur-aan Takatifu kuanzia mwaka wa 1950 hadi mwaka 1967, wakati
fikra za umoja wa Kiislamu na Uislamu wa kisasa ulipokuwa ukifanyiwa kampeni
kubwa hapo Zanzibar.
Wakati huo
huo Tafsiri hii ilikuwa ni jibu la tafsiri ya Qur-aan Tukufu aliyoiandika Padri
Godfrey Dale kwa ajili ya kuwawepesishia wahubiri wa Kiafrika walioajiriwa na University
Mission to Central Africa (UMCA), iliyoanzishwa mwaka 1873 na Padri
Dr. David Livingston (1813-1873) huko Zanzibar.
Tafsiri ya
Padri Dale iliyoandikwa kwa Kiswahili cha Kiunguja ilikuwa na kurasa 542 pamoja
na kurasa 142 za sharhi, ilipigwa chapa mwaka 1923 huko London na jumuiya ya
kueneza elimu ya Kikristo (Society for Promoting Christian Knowledge).
Kwa vile
tafsiri hiyo iliandikwa kwa njia ya kuutetea Ukristo, jambo lisilokubalika kwa
Waislamu, Sheikh Mubarak bin Ahmed bin Ahmad, mkuu wa Makadiani Afrika
Mashariki (Ahmadiyah Muslim in East Africa) aliamua kuanza kuandika
tafsiri yake mwaka 1936 iliyokubaliwa na kutambuliwa na wamisionari hapo Zanzibar.
Katika mwaka
1942 nakala ya tafsiri ya Makadiani iliyopigwa taipu ilipelekwa mbele ya kamati
ya lugha ya Kiswahili (Inter-Territorial
(Swahili) Language) kwa ajili ya kukubaliwa rasmi kilugha. Na katika
mwezi wa April mwaka 1944, kamati ilijibu kwa kuikubali lugha iliyotumika
ikitaka baadhi ya marekebisho kufanyika. Juu ya kuwa masahihisho yote
hayakufanyika kama ilivyotakiwa, tafsiri hiyo
ikapelekwa mbele ya baadhi ya viongozi wa Makadiani wa Afrika ya Mashariki na
kukubaliwa kuwa lugha iliyotumika ni nzuri na yenye kukubalika.
Sheikh Amri
bin Abeid (1924-1964), aliyejifunza Ukadiani huko Pakistan mwaka (1954-1956)
alijaribu kuitetea tafsiri ya Makadiani, lakini tafsiri hiyo iliyopigwa chapa
kwa mara ya mwanzo mwaka 1953 ilisababisha mgogoro mkubwa kutoka kwa Masunni
waliowatuhumu Makadiani kuwa wamebadilisha na kugeuza baadhi ya maneno kwa
kusudi la kuunga mkono fikra zao.
Ili kupambana
na tafsiri za Wakristo na Makadiani zilizogeuzwa na kubadilishwa ilionekana
kuwepo umuhimu na dharura ya kupatikana tafsiri yenye kutambuliwa rasmi. Jukumu
hilo
akabebeshwa Sheikh Abdullah Saleh Farsy, aliyekuwa akimuomba Mwenyezi Mungu
ampe umri mrefu asife kabla ya kuikamilisha tafsiri hiyo.
Fikra hii
adhimu ilianza baada ya Sheikh kupiga chapa kitabu chake cha mwanzo kiitwacho
'Maisha ya Mtume Muhammad' (Swallah Llahu alayhi wa Sallam)
kilichofuatiliwa na kitabu cha Sura za Swalah na Tafsiri zake mwaka (1950).
Kabla ya
kudhihirisha kutoridhika kwake na tafsiri ya Makadiani katika kijitabu kidogo
‘Upotofu wa Tafsiri ya Makadiani’, Sheikh Abdullah Saleh alikwishawahi kuandika
tafsiri na sharhi ya Surah Yaseen, Al-Waqiah na Al- Mulk kilichopigwa chapa na
A.A. Vasingstake, Uingereza na kutolewa mwaka 1950 Zanzibar.
Tafsiri yake
aliyoiandika kwa kuitegemea zaidi tafsiri ya Jalalayn ilianza kupigwa chapa
juzuu baada ya juzuu, na baina ya mwaka 1956 na 1961 juzuu kumi na mbili
zilikwishapigwa chapa.
Kutokana na
upungufu wa fedha, tafsiri iliyokamilika ilipigwa chapa mwaka 1969 na wadhamini
walikuwa The Islamic Foundation.
Msaada
mkubwa uliotolewa na Sultani wa Qatar, Sheikh Ahmad bin Ali uliwezesha kugawiwa
bure misahafu 4,000 na kuuzwa misahafu mingine 3,000 kwa bei nafuu ya shilingi
kumi tu.
Kuanzia
mwaka 1950 hadi 1960 kampeni kubwa dhidi ya Makadiani ilifanywa na Jamaat al Islam huko Pakistan chini ya uongozi wa Sheikh Maududi
(1903-1979) aliyezikaribisha juhudi kubwa za Sheikh Abdullah Saleh Farsy, juu
ya khitilafu iliyokuwepo baina ya misimamo ya Zanzibar na Pakistani, kwani Sheikh Abdullah
Saleh Farsy hakuwa akiona tofauti yoyote baina ya Makadiani na Ahmadiya
waliojitenga na Makadiyani. (Ahmadiya ni kundi lililojitenga na Makadiani
kutokana na baadhi ya khitilafu baina yao)
Islamic
Foundation ya Nairobi yenye kuunga
mkono Jamaat al Islam ya Pakistan,
ndiyo iliyopiga chapa kwa mara ya mwanzo Tafsiri ya Sheikh Abdullah Saleh
Farsy, aliyeandika kuwa Maududi ameikubali tafsiri yake ya QURANI TAKATIFU. Na
Sheikh Abdullah Saleh Farsy naye alieleza kuikubali kwake tafsiri ya Maududi
inayoitwa 'Qur'an Fahmi Ke Bunyadi Usul' (Msingi wa kuifahamu Qur-aan),
na akaruhusu uandikwa utangulizi wa Tafhim
Al-Qur-aan katika Qurani Takatifu.
Mafundisho yake
Kuanzia
tarehe 7 Januari 1960 hadi 19 Februari 1960
Sheikh Farsy alikuwa safarini Nyasaland 'Malawi' na Rhodesia ya Kusini akitoa
darsa na kuwahutubia Waislamu na kuwanasihi juu ya umuhimu wa kujifunza masomo
ya dini.
Tarehe 11
April 1960 baada ya kurudi kutoka Nyasaland,
Sheikh Farsy aliandika ripoti aliyoeleza ndani yake umuhimu wa mafunzo ya dini.
Aliwataka wanaohusika kutilia nguvu umuhimu wa kuwapatia Waislamu elimu katika
skuli za serikali.
Aliandika: "Kwanza, upeo wa elimu ya watoto wa Kiislamu ni duni
ukilinganisha na wasiokuwa Waislamu katika Nyasaland.
Kuwepo kwa jamii mbili katika nchi, mojawapo imeelimka na nyengine haijaelimika
ni hatari kwa serikali na kwa jamii. Serikali ni baba wa wananchi wote, na kwa
ajili hiyo inapaswa kutopendelea upande mmoja."
Aliendelea
kueleza: "Serikali inatoa misaada mbali mbali kuipa
skuli za wamishionari bila ya kuzilamisha kujiunga na skuli za serikali. Jukumu
la serikali ya Nyasaland lazima liwe
kuinyanyua daraja ya elimu kwa Waisalmu iwe sawa na ile ya jamii nyingine
nchini.”
Matakwa ya
Sheikh Farsy juu ya kuelimishwa Waislamu hayakuwa kutaka wajengewe skuli zao
tu, bali yalikuwa makubwa kuliko hivyo. Alitilia mkazo jambo la kuajiriwa
waalimu wa dini ya Kiislamu katika skuli za serikali pia. Alisema: "Shule
za serikali hazina budi kuwa na walimu watakaosomesha mafunzo ya Kiislamu wenye
kulipwa na serikali. Inashangaza kuona kuwa waalimu wa Kikristo katika shule
hizo wanalipwa na serikali wakati waalimu wa Kiislamu wanalipwa na jamii. Haya
hayafahamiki."
Kupitia darsi
zake za misikitini na kwa njia ya vitabu, Sheikh Farsy alitumia juhudi zake
zote katika kuwaelimisha vijana misingi asili ya Kiislamu. Alihimiza na kutilia
nguvu umuhimu wa kufufua, kufuata na kuyafahamu mafundisho sahihi ya dini kama
yalivyokuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa
Sallam) na Sahaba zake (Radhiya Llahu anhum) pamoja na mafundisho ya
watu wema waliotangulia 'Salafus
Swaalih'.
Mafundisho
haya yalikuwa yakifundishwa kabla yake na Sheikh Al-Amin na Sheikh Muhammad Kassim
hapo Mombasa.
Lengo la
Sheikh Farsy lilikuwa kubwa kupita wadhifa wake wa Kadhi mkuu wa Kenya.
Lengo lake lilikuwa ni kupata jukwaa litakalomwezesha kuifufua na kuieneza
elimu sahihi ya dini kama ilivyokuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa Sallam), na kuwakataza watu kufuata uzushi ‘bid’aah’ na itikadi
zisizo na misingi ya Kiislamu, na mambo yaliyo batili ambayo hao wanaoyaeneza
wanajaribu kuyanasibisha na Uislamu.
Sheikh Farsy
alifanikiwa kiasi kikubwa sana,
na watu wengi waliokuwa wakihudhuria darsa zake walikuwa wakihisi kuwa mafunzo
yake yanaingia moja kwa moja ndani ya nyoyo zao. Kwa juhudi zake, alifanikiwa
kuanzisha kizazi kilichoiendeleza kazi yake hiyo ya kupiga vita uzushi na
ushirikina, na kufanikiwa kuondoa itikadi nyingi ambazo watu wakati huo
walikuwa wakidhani kuwa yamo katika dini.
Safari zake
Baada ya
kukamilisha masosmo yake katika Chuo cha Ualimu 'Teachers Training
College (TTC)', Sheikh Abdullah alisomesha shule za msingi kuanzia mwaka 1932
hadi 1947, na kutokana na jitihada zake kubwa katika kazi, alipewa cheo cha
Mkaguzi mkuu wa shule za msingi za Unguja na Pemba kuanzia mwaka 1949 hadi
mwaka 1952. Kisha akapewa cheo cha Principal wa Muslim Academy Secondary
School kuanzia mwaka 1952 hadi 1956 kabla ya kuchaguliwa kuwa Mwalimu mkuu 'Headmaster' wa Arabic
Medium School kuanzia mwaka 1957 hadi 1960.
Mwezi wa
Machi mwaka 1960, Sheikh alikwenda kuhiji na katika mwaka wa 1967 alijiuzulu
kazi katika Wizara ya Elimu alipokuwa mwalimu katika Chuo cha Ualimu 'Teachers'
Training College.
Katika mwaka
1960, alichaguliwa kuwa Kadhi mkuu wa Zanzibar, na aliendelea na kazi hiyo muda
wa miaka saba, mpaka alipoamua kuiacha na kuhamia Kenya baada ya mapinduzi ya
Januari 12, 1964 yaliyosababisha umwagaji mwingi wa damu huko Zanzibar pamoja
na kukamatwa na kutiwa ndani bila sababu kwa viongozi wengi wa kisiasa na wa
kidini.
Mwenyeji
wake huko Kenya alikuwa
Sheikh Muhammad Kassim al-Mazrui, sahibu yake wa zamani tokea waliposoma pamoja
chini ya mwalimu wao Sheikh al-Amin bin Ali al-Mazrui, aliyekuwa akifundisha
dini huko Zanzibar.
Sheikh
Abdullah Saleh Farsy hakuwa mgeni huko Kenya ambako sifa zake kuwa
mwanachuoni mkubwa zilitangulia kufika kabla yake. Sheikh Muhammad Kassim
al-Mazrui ndiye aliyempendekeza kwa Rais Jomo Kenyatta kupewa cheo cha Kadhi
mkuu wa Kenya,
jambo ambalo Rais Kenyatta alilikubali bila kipingamizi.
Kwa muda wa
miaka 14 alikuwa Kadhi mkuu wa Kenya,
daraja yenye heshima kubwa sana aliyoitumikia
kwa muda wote huo kwa ikhlasi, hekima, uwezo wa hali ya juu, na uerevu mkubwa sana mpaka alipoamua
kustaafu katika mwaka 1980.
Kifo chake
Sheikh
Abdullah Saleh Farsy alifariki dunia tarehe 9 Novemba mwaka 1982 karibu miezi
minane tokea alipoondoka Kenya kuelekea Muscat - Oman kwa ajili ya kuungana na
aila yake.
Huzuni kubwa
iliyoingia nyoyoni mwa Waislamu wa Afrika Mashariki kutokana na kifo chake
itaendelea muda mrefu sana, na pengo lake kamwe
si rahisi kuzibika, na watu wataendelea kufaidika na elimu aliyowarithisha
daima milele.
Wadhifa zake
·
Mwalimu – Shule za msingi (1932 -
1947)
·
Mkaguzi mkuu wa Shule za Msingi - Zanzibar
na Pemba (1949 - 1952)
·
Principal - Muslim Academy
Secondary School (1952 -
1956)
·
Mwalimu mkuu - Arabic Medium
School (1957 - 1960)
·
Kadhi mkuu wa Zanzibar (1960 - 1967)
·
Mwalimu - Teacher Training
College (? - 1967)
·
Kadhi mkuu wa Kenya (1974 - 1980)
Darsi zake
Alipokuwa Mombasa, Kenya
Sheikh Farsy alikuwa akitoa darsa zake katika misikiti ifuatayo:
·
Msikiti Sakina (Majengo) kila
Jumanne
·
Msikiti Al-Azhar (Guraya) kila
Al Khamisi
·
Msikiti Shihab (Mwembe Tayari) kila
Jumatano
·
Msikiti Mlango wa papa (mji wa Kale)
Jumatatu
·
Msikiti Ridhwaan (King’orani) Ijumaa
·
Msikiti Muhammad Rashid (Kaloleni
Mazui) Jumatatu-mara moja kila mwezi
·
Tunah (Majengo) Ijumaa moja
·
Msikiti Nur (Ijumaa moja)
·
Malindi, Kenya
·
Msikiti Sheikh Nassor. (Jumamosi
baada ya Swala ya Magharibi)
Vitabu vyake:
·
Tafsiri ya Qurani Takatifu.
Ilipigwa chapa mara ya mwanzo mwaka 1969
·
Maisha ya Nabii Muhammad
·
Mawaidha ya Dini
·
Tarehe ya Imam Shafi na Wanazuoni
wakubwa wa Afrika ya Mashariki
·
Baadhi ya Wanachuoni wa Kishafi wa
Mashariki ya Afrika.
·
Sayyid Said bin Sultan
·
Urathi
·
Jawabu za Masuala ya dini (sehemu ya
kwanza, pili na tatu)
·
Tafsiri ya Suratul Kahf na hukumu ya
swala ya Ijumaa
·
Sura za
swala na tafisir zake
·
Swala na maamrisho yake
·
Ndoa na maamrisho yake
·
Saumu na maamrisho yake
·
Mambo anayofanyiwa Maiti na Bidaa za
Matanga na hukumu za Eda
·
Bidaa I na II
·
Khitilafu za Madhehebu Nne katika
swala
·
Sifa za
Mtume, mawaidha na Dua
·
Mashairi I-II
·
Maisha ya Sayyidnal Hassan
·
Maisha ya Sayyidnal Hussein
·
Utukufu wa swala na namna ya kusali
·
Mafunzo ya dini
·
Tafsiri ya Maulidi Barzanji neno kwa
neno
·
Wakeze Mtume wakubwa na wanawe
wengine
·
Wakeze Mtume wadogo
·
Tafsiri ya Baadhi ya Sura za Qurani:
Yasin, Waqia na Mulk Sayyidna Khalid bin Al-Walid
·
Vyakula alivokula Mtume
·
Tunda la Quran
·
Upotofu juu ya Tafsiri ya Makadiani
·
Kisa cha Miraji
·
Maisha Ya Mtume Muhammad
Vitabu vya
Kiarabu:
·
Al-Busa’idiyyun hukkam Zinjibar. Muscat: Ministry of National
Heritage and Culture 1982.
Vitabu vyake
visivyopigwa chapa: (kiarabu)
·
1.
Inayatullaahi al-adhym bi al Qurani al-Karim
·
2.
Irfaani al ihsaan bi tarjamati al qarii Hafs bin Suleiman
·
3. Nuru al basira wal al basar fi
taraajimi al quraa al arba’atashar
·
4. Al khulafau al Amawiyin [28]
No comments:
Post a Comment