MTAFARUKU mkubwa umezuka kati ya familia na wanafunzi
wa Mwanachuoni Mkubwa wa Dini ya Kiislamu wa Afrika Mashariki, Sheikh
Nassor Abdallah Bachu aliyefariki dunia jana mchana huko Chukwani Mjini
Zanzibar.
Mtafaruku huo umekuja baada ya wanafamilia kuchimba
kaburi mbele ya kibla cha Msikiti ambayo amesaliwa huku wanafunzi wa
Sheikh huyo wakisema hawezi kuzikwa katika kibla cha Msikiti kwa kuwa ni
kinyume na mafundisho ya dini ya kiislamu.
Kamati ya maandalizi ya mazishi hayo imesema kitendo
kilichofanywa na wanafamilia kuchimba kaburi mbele ya msikini ni kinyume
mafundisho ya dini na ni tofauti na alivyokuwa akihubiri wakati wa uhai
wake ambapo mara zote alikuwa akikataza waumini wa dini ya kiislamu
kuzikwa ndani ya msikiti au mbele ya msikiti.
Akiongozwa kamati hiyo, Sheikh Nurdin Kishki
aliwatangazia waumini kuwa na subra wakati kamati ya maandalizi ya
Sheikh huyo ikiwa ikifanya mazungumzo na wanafamilia ili kufikia mwafaka
wa wapi lichimbwe kaburi lake, huku kila mmoja aliyekuwepo katika
mkuanyiko huo wakisomeshana namna ya kuzikana maiti za kiislamu.
Wakati waumini hao wakitakiwa kuwa na subra baadhi ya
waumini wamekwenda kulifukia kaburi la awali lililochimbwa na kusema
haitowezekana kuzikwa katika eneo hilo na kutafutwa eneo jengine kwa
ajili ya kuulaza mwili huo.
“Waumini tunakuombeni jamani muwe na subra lakini
tunasema daima mwenyewe Marehemu Sheikh Nassor wakati wa uhai wake
alikuwa akipinga suala la kuzikwa ndani ya msikiti au mbele ya msikiti
lakini kaburi tunaliona limechimbwa mbele ya msikiti huku ni kwenda
kinyume na mafundisho ya dini ya kiislamu na pia ni kinyume na kile
alichokuwa akikihubiri na kukisomesha, hatuwezi kuwaingilia wanafamilia
kwa kuwa sisi ni wanafunzi wake tu Sheikh lakini wao ndio wenye maiti na
wao ndio wenye haki lakini tunawaomba sana katika hili tusende kinyume
na dini” alisema Kishki mbele ya umati mkubwa.
Baada ya vuta ni kuvute hizo wanafamilia waliingia
ndani ya msikiti na kujifungia na hatimae kutoa tamko la kuuliza ni
masafa gani ambayo wanataka likachimbwe kaburi na mwili wa marehemu
ulazwe.
Akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari, Said
Masoud Gwiji ambaye ni miongoni mwa wanafunzi wake Sheikh Nassor na pia
ni mwana kamati ya maandalizi ya mazishi alisema kwamba ni vizuri wana
familia wakafahamu kwamba alichokuwa akikihubiri Sheikh Nassor kiendane
na kile kinachotekelzewa mwisho wa uhai wake.
Alisema sio busara kuvutana lakini kwa kuwa
mafundisho ya dini ya kiislamu yanakataza kaburi kuchimbwa karibu na
msikiti ni vyema likazingatiwa hilo na mazishi hayo kaburi likachimbwa
kando na msikiti.
Hatimae wanafamilia na wanafunzi wa Sheikh Naassor
wakakubaliana kuchimba kaburi mbali na msikiti na mazishi yakafanyika
huku umati mkubwa ukiwa unashuhudia huku kila mmoja akitaka kushika
maiti hiyo jambo ambalo limezusha ahama kubwa kutokana na umati mkubwa.
Naye Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim
Seif Sharif Hamad ameungana na melfu ya waumini wa dini ya Kiislamu jana
katika mazishi ya Mwameanachuoni na Mhadhiri Mkubwa wa Dini ya Kiislamu
Zanzibar, Sheikh Nassor Abdallah Bachu amefariki dunia juzi Chukwani
Mjini Unguja.
Sheikh Nassor Bachu amefariki majira ya saa 5 mchana
juzi baada ya kuugua kwa muda mrefu akisumbuliwa na kiharusi ambapo
alisafirishwa kwa matibabu nchini India na katika hospitali mbali mbali
za Dar es Salaam na Zanzibar kabla ya kufikwa na mauti.
Mwili wa Marehemu Sheikh Nassor ulilazimika kusaliwa
katika viwanja vya Mnazi Mmoja kutokana na kuwa hakuna Msikiti mkubwa
ambao ungeweza kuhimili maelfu hayo ya watu waliofika kwa ajili ya
kushindikiza mwili huyo.
Hii ni mara ya kwanza kwa ummati mkubwa kama huo
kushiriki mazishi ya Mwanachuoni huyo ambapo awali alitakiwa kusaliwa
katika Msikiti wa Kikwajuni aliokuwa akiendesha darsa wakati wa uhai
wake lakini kutokana na umati mkubwa ilishindikana na kuamuliwa kusaliwa
katika viwanja vya Mnazi Mmoja, na baadae magari yamefuata msafara
kuanzia Skuli ya Haile Sellasie na kuelekea Donge kwa kuzikwa ambapo
kuanzia Mjini hadi Donge barabara imejaa wananchi wakisubiri njiani
kuona msafara uliobeba maiti hiyo.
Mazishi ya Sheikh Nassor hayajawahi kutokea ambapo
mbali ya ummati mkubwa kuja kushuhudia mazishi hayo wanawake na wanaume
walioanzia Chukwani alipomalizikia uhai wake, na baadae kuletwa katika
uwanja na Mnazi Mmoja na kupekelekwa huko Donge maelfu ya waumini
wameonekana kusubiri maiti njiani na kushuhudia msafara mkubwa uliokuwa
ukiongozwa na gari ya Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja
na Waziri wa Ofisi ya Makamo wa Pili, Mahammed Aboud Mohammed, Mufti
Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar,
Sheikh Khamis Haji, Katibu Mtendaji wa Wakfu na Mali ya Amani Sheikh
Abdallah Talib na Masheikh mbali mbali kutoka Nairobi, Mikoa ya Tanzania
Bara, na wenyeji wao Zanzibar.
Sheikh Nassor alinza kufundisha mafunzo ya dini ya
Kiislamu kwa kuendesha darsa mbali mbali katika Misikiti ya Kikwajuni na
Rahaleo mnamo mwaka 1978 baada ya Mwalimu wake Sheikh Said Njugu kuanza
kuumwa na kushindwa kuendesha darsa hizo ambapo majina ya wanafunzi wa
Sheikh huyo yalipendekezwa matatu akiwemo Sheikh Ali Ahmad, Sheikh
Othman Ali na yeye Sheikh Nassor Bachu.
Mwalimu wake Sheikh Nassor pia aliwahi kupigwa
marufuku kufanya mihadhara na kuendesha darsa na Mzee Aboud Jumbe Mwinyi
aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo jambo ambalo linelezwa kwamba
kabla ya kifo chake Sheikh Said Njugu alikwenda kuombwa radhi na Mzee
Aboud Jumbe.
Wanafunzi wa mwanzo ambayo amewasomesha Sheikh Nassor
alivyoanza kuendesha darsa ambapo alianzia na wanafunzi wachache
akiwemo Abdulghani Msoma ambaye ni Katibu Ofisi ya Utawala Bora,
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Rashid na Ali Juma
Shamhuna ambaye ni waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Sheikh Nassor Bachu alianza kuvuma katika miaka 80
ambapo alikuwa na upinzani mkubwa kati yake na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar iliyokuwa ikiongozwa na Rais wa wakati huo Dk Salmin Amour Juma
ambapo alionekana kuhimiza wajibu na maadili ya kiislamu kufuatwa jambo
ambalo lilikuwa likionekana ni geni kwa wakati huo.
Mbali kupingwa na viongozi wa serikali lakini pia
Sheikh Nassor alipata upinzani mkali kutoka kwa Maulamaa na Masheikh
mbali mbali wa dini ya Kiislamu kutokana na kutangaza kwake msimamo wa
kufuata Sunnah -Mila za Mtume Muhammad (s.a.w) ambapo waislamu
walionekana kupingana naye.
Msimamo wa Sheikh Nassor Bachu ulikuwa ni kukataza
kuadhimishwa kwa kuzaliwa kwa Mtume Muhammaa (s.a.w) kwa kusomwa maulid
na akitaka maadhimisho hayo yawe ni kufuata matendo yake badala ya
kukusanyika, pamoja na suala la muandamo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani
kufuatwa popote unapoonekana jambo ambalo lilikuwa likipingwa na baadhi
ya Maulamaa hapa nchini wakitaka lazima Mwezi uonekane nchini na
utangazwe na serikali.
Changamoto alizokumbana nazo Sheikh Nassor katika
uhai wake ni nyingi ikiwemo kutengwa na baadhi ya jamii yake, kuzuwiwa
kuendesha darsa, kufungiwa misikiti asisalishe na mara kadhaa kupigwa
mabomu ya machozi wakitawanywa baada ya kusali sana la Eid El Hajj
ambapo hali hiyo ilianzia wakati wa utawala wa Dk Salmin na kumalizikia
kwa Rais Mstaafu Amani Karume.
No comments:
Post a Comment