“Kifua
changu kilifunguka baada ya kuujua Uislamu”
“Nilikuwa na
masuali mengi sana ndani ya nafsi yangu juu ya dini yangu ya Ukristo, lakini
sikuweza kupata majibu ya kuniridhisha, nikaamua kujiunga na shule ya upadri ili
niweze kusoma na kuijuwa vizuri. Nikasoma mpaka nikafikia cheo cha Upadri,
nikawa mlinganiaji mkubwa wa dini yangu, na pia baba
yangu alikuwa mlinganiaji wa dini ya ukristo juu ya kuwa biashara yetu kubwa
ilikuwa ni kuuza vyombo vya muziki ambavyo sehemu kubwa ya vyombo hivyo
tulikuwa tukiyauzia makanisa.
Nilikuwa nikiuchukia sana Uislamu na
Waislamu na hii inatokana na sura mbaya niliyokuwa nayo juu ya Uislamu kuwa wao
ni watu wasiokuwa na imani juu ya Mwenyezi Mungu, wenye kuliabudu sanduku jeusi
liliopo jangwani na kwamba ni watu wajinga, magaidi wenye
kuua kila asiyefuata dini yao.
Lakini alipokuja kuishi nyumbani
kwetu Muislamu mmoja kutoka nchi ya Misri kwa muda wa
miezi miwili, nilibahatika kugundua mengi juu ya Uislamu na hii ilitokana na
maisha na nidhamu yake mtu huyo, na baada ya kujadiliana naye tuligundua mambo
mengi mepya juu ya Uislamu hatukuwa tukiyafahamu hapo mwanzo
Siku moja baba yangu aliniambia kuwa
atakuja mtu mmoja kutoka nchi ya Misri na kwamba huenda
tukafanya naye biashara ya ala za muziki, jambo lililonifurahisha sana kwani tukifanikiwa
biashara yetu itaenea na kufika hadi nchi ile kubwa ya Pyramids (Misri). Kisha
baba yangu akaniambia: “Lakini sina budi kukuambia
kuwa mtu huyo atakayekuja ni Muislamu na ni mfanya
biashara maarufu.”
Nikamuuliza huku nikiwa nimeudhika sana: “Muislamu! Hapana, siwezi
kukubali kuzungumza naye”
Baba yangu akaniambia: “Huna
budi kukubali.”
Nikajibu: “La abadan siwezi
kukubali.”
Baba yangu akashikilia kuwa lazima
nimpokee vizuri Muislamu huyo kutoka nchi ya Misri, na
mimi nilikubali kwa sababu nilikuwa naishi katika nyumba yake asije
akanifukuza.
Hata hivyo, siku aliyowasili mgeni
huyo nilikwenda kumpokea nikiwa nimevaa kofia yenye msalaba mkubwa na kidani chenye msalaba na pia nilifunga msalaba mkubwa juu
ya mkanda wangu huku nikiwa nimebeba Biblia mkononi mwangu.
Nilikwenda kumpokea nikiwa hali
hiyo, na jambo la mwanzo nililofanya baada ya kuonana
naye ni kuishambulia dini ya Kiislamu pamoja na Waislamu kama nilivyokuwa nikiijuwa
mimi kutokana na sura mbaya niliyokuwa nayo. Na wakati wote huo yeye alikuwa
mtulivu sana akipokea kwa utulivu mkubwa maneno yangu
yaliyojaa hamasa na ghadhabu.
Tulipowasili nyumbani, baba yangu
akamkaribisha vizuri na kumtaka afikie nyumbani kwetu
na kukaa hapo kwa muda, na nyumbani kwetu tulikuwa tukiishi mimi na mke wangu
na baba yangu.
Mmisri yule akakubali kuwa mgeni
wetu na wakati ule pia tulikuwa na mgeni mwengine
aliyekuwa Mkristo mwenye kufuata madhehebu ya Kikatholiki
Idadi yetu ikawa
watu watano.
Wane kati yetu ni walinganiaji wa dini ya Kikristo,
mimi na baba yangu tulikuwa wafuasi wa madhehebu ya Kiprotestanti na yule
Mkristo mgeni wetu alikuwa akifuata madhehebu ya Kikatoliki, na mke wangu pia
alikuwa mlinganiaji mwenye kufuata madhehebu ya chuki yaliyokuwa karibu sana na
itikadi za Kiyahudi (Zionist). Baba yangu aliisoma Injili tokea alipokuwa na umri mdogo akawa mlinganiaji maarufu. Yule askofu wa
Kikatoliki alikuwa na ujuzi mkubwa baada ya kufanya kazi ya kulingania katika
bara zote mbili za Amerika (Amerika ya kusini ya Kaskazini) kwa muda wa miaka
12, na mke wangu alikuwa akifuata madhehebu ya ‘Burinjin’ yenye kuunga mkono
itikadi za Kiyahudi, na mimi binafsi nilidurusu Injili pamoja na madhehebu
mbali mbali ya Kikristo na kupata shahada ya ‘Doctorate’ katika elimu ya
itikadi za Kikristo.
Tukawa sisi Wakristo kila mmoja wetu
anayo Biblia yake yenye kuhitalifiana na ya wenzake,
tunakaa tukiwa tumeizunguka meza ya duara na kujadiliana juu ya hitilafu zilizokuwepo
katika itikadi za Kikristo na hitilafu zilizokuwepo katika Biblia zetu tofauti
huku yule Muislamu akistaajabu juu ya khitilafu za Biblia zetu. Na wakati ule
baba yangu alikuwa na Biblia ya Mfalme James na mimi
nilikuwa na Biblia ya Revised Edition inayosema kuwa ndani ya Biblia ya Mfalme
James mna makosa mengi na dhambi kubwa kubwa, na hii ndiyo sababu iliyowafanya
Wakristo baada ya kuona makosa mengi yaliyomo iliwabidi kukiandika upya na
kusahihisha yale waliyoona kuwa ni makosa makubwa. Na Biblia ya tatu aliyonayo
mke wangu ni copy ya mlinganiaji wa siku hizi aitawe
James Swagart, na kinachochekesha ni kuwa James Swagart huyu alipokuwa
akijadiliana na Sheikh Ahmed Deedat mbele ya watu alisema: “Mimi sina elimu ya Biblia!!” Inakuwaje basi mtu aandike Biblia kamili kwa jina lake wakati hana elimu ya Biblia, kisha adai kuwa
inatoka kwa Mwenyezi Mungu.
Yule askofu wa Kikatholiki, yeye anayo Biblia nyengine yenye milango 73,
wakati Biblia niliyonayo mimi ina milango 66, na Biblia zote hizo zinahitilafiana
hata yaliyomo ndani yake na hitilafu hizo ni kubwa na nyingi sana.
Tukamuuliza yule Muislamu kutoka
Misri ambaye jina lake lilikuwa Muhammad: “Zipo
Qurani ngapi kwenu zenye
kuhitalifiana?”
Akanijibu: “Sisi
hatuna isipokuwa Qurani moja tu nayo ni ile ile
iliyoteremshwa kwa lugha ya Kiarabu na wala haijabadilishwa wala kuongezwa hata
herufi moja ndani yake tokea ilipoteremshwa miaka 1400 iliyopita.”
Na yule askofu wa
Kikatoliki alikuwa haamini mengi yaliyomo ndani ya Biblia yake, jambo
lililomfanya awe na ugomvi mkubwa na viongozi wa Kanisa lake, kwani juu ya kuwa
ni mlinganiaji wa Kanisa hilo kiasi cha miaka 12 hivi sasa, lakini hakuwa
akiamini mengi katika mambo ya itikadi yaliyo muhimu sana.
Na baba yangu alikuwa akiamini kuwa
Biblia hizi zimeandikwa na watu na kwamba si wahyi
utokao kwa Mwenyezi Mungu, isipokuwa wameandika wakidhani kuwa huo ni wahyi
utokao kwa Mwenyezi Mungu. Na mke wangu pia alikuwa akiamini kuwa katika Biblia
yake mna makosa mengi sana, isipokuwa yeye pia alikuwa
akiona kuwa asili ya maneno yaliyomo yanatoka kwa Mwenyezi Mungu.
Ama mimi sikuwa nikiayasadiki mengi
yaliyomo ndani ya Biblia zetu, kwani nilikuwa nikiona kuwa maneno yake
yanagongana na hayakubaliani, na miongoni mwa mambo hayo nilikuwa siku zote
nikijiuliza nafsi yangu na nikiwauliza wengine pia kuwa itakuwaje Mwenyezi
Mungu awe mmoja kisha wakati huo huo awe watatu? Na niliwahi
kuwauliza Maaskofu wakubwa, tena mashuhuri ulimwenguni wakati ule, wakanipa
majibu yasiyokubalika akilini. Nikawauliza vipi nitaweza kuwa
mlinganiaji na kuwafundisha watu kuwa Mwenyezi Mungu
ni mmoja na wakati huo huo ni watatu, kisha niwafanye waamini wakati mimi
mwenyewe sijaamini.
Wengine wakaniambia: “Usiwabainishie watu, wewe waambie tu kuwa jambo hili ni katika yale ambayo mtu analazimika kuamini bila ya
kuuliza”. Na wengine wakaniambia: "Unaweza
kuwaambia watu kuwa Utatu wa Mwenyezi Mungu ni mfano
wa tunda la tufaha, juu ya kuwa ni moja lakini nje yake mna ganda na ndani yake
mna nyama na kokwa.” Nikawaambia: ‘Mfano huu
hauwezi kupigiwa Mwenyezi Mungu, kwani ndani ya tufaha mna kokwa nyingi kwa hivyo miungu inaweza kuwa mingi, na pia huenda ndani
yake akawepo mdudu, na kwa njia hiyo miungu itaongezeka, na huenda tufaa
likaoza na mimi simpendi mungu wa aina hiyo.”
Na wengine wakanipigia mfano wa mtu
na mkewe na mwanawe, nikawaambia kuwa mke anaweza kuwa na mimba na idadi
ikaongezeka, na anaweza kutalikiwa kisha miungu ikafarikiana, na anaweza kufa
mmoja wao na mimi sipendi mungu wa aina hiyo.
Sijapata hata siku moja kuamini juu
ya Utatu wa Mwenyezi Mungu na wala sijapata kumuona
mwenye kuweza kumshawishi mwenye akili zake akaamini hayo tokea nilipozaliwa
nikabatizwa na hatimaye nikawa Padri na mlinganiaji.
Hata hivyo tulipokuwa sisi Wakristo
wane tumekaa kuizunguka meza yetu nyumbani tukijadiliana, tulikuwa tukijaribu
kumuita Muislamu huyu katika Ukristo, lakini yeye alikuwa akitujibu kuwa yeye
atakubali kutufuata ikiwa tunayo yaliyo bora kuliko yaliyomo katika dini yake.
Tukamuambia: “Bila shaka yamo mengi.”
Muislamu akasema: “Mimi nipo tayari kama mtaweza
kunipa uthibitisho na dalili ya maneno yenu.”
Nikamuambia: “Dini kwetu haina
uhusiano na dalili wala akili, bali unatakiwa lazima usalimu amri na kuyakubali
yote unayoambiwa. Itakuwaje sasa wewe unataka tukupe
uthibitisho na dalili?”
Muislamu akasema: “Lakini Uislamu ni dini ya
Itikadi na uthibitisho na dalili na akili na Wahyi utokao mbinguni.”
Nikamuambia: “Ikiwa kwenu mnategemea uthibitisho na dalili
basi mimi ningependa kufaidika na kusoma kutoka kwako.” Na tulipoanza
kujadiliana juu ya Utatu, kila mmoja wetu akatoa Biblia yake na
kuanza kusoma, lakini hatukuweza kupata dalili yoyote iliyo wazi. Kisha
tukamuuliza Muhammad: “Nini itikadi yenu juu ya
Mwenyezi Mungu katika Uislamu?” Akasema:
1-
قُلْ هُوَ اللهُ أَحَدٌ
2- اللهُ الصَّمَدُ
3-
لَمْ يَلِدْ وَلَمْ
يُولَدْ
4- وَلَمْ يَكُن لَّهُ
كُفُوًا أَحَدٌ".
|
1. Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee.
2.
Mwenyezi Mungu Mkusudiwa.
3. Hakuzaa wala hakuzaliwa.
4. Wala hana anaye fanana naye hata mmoja
|
ِAlisoma kwa
Kiarabu kisha akatufasiria, na sauti yake pale alipokuwa akisoma kwa lugha ya
Kiarabu iliingia ndani ya moyo wangu na hata hivi sasa kama kwamba bado
inaendelea kuingia sikioni mwangu na bado ningali ninaikumbuka. Ama kuhusu tafisiri
yake; sijapata kuona maneno yaliyo wazi na bora, tena
yenye nguvu na kufahamika na kukubalika akilini yenye kubeba maana yote kwa
ukamilifu kupita hayo.
Tukio hili
kwetu lilikuwa mfano wa mshangao mkubwa uliotuamsha
katika usingizi wetu na kughafilika kwetu tuliokuwa tukiishi ndani yake pamoja
na upotovu.
Yule askofu wa Kikatoliki akamuomba Muhammad ampeleke msikitini ili
apate kuona namna Waislamu wanavyoswali, akaenda naye mara mbili katika
mojawapo ya makao ya Jumuiya ya Kiislamu, na huko akaona namna Waislamu
wanavyotawadha na kuswali, kisha akarudi nyumbani. Na sisi tukamuuliza yule
Askofu: “Muziki gani wanapiga Waislamu katika Swala
zao?”
Akasema: “Hawapigi muziki kabisa.”
Tukasema kwa mshangao: “Wanamuabudu Mola
wao na kuswali bila ya muziki!?”
Askofu
akasema: “Ndiyo, na mimi natamka: ( أشهد أن لا إله إلا الله
وأن محمدًا رسول الله) Nashuhudia kuwa hapana anayestahiki
kuabudiwa isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.”
Tukamuuliza:
“Kwa nini ukasilimu, wewe unayo hakika juu ya haya
unayotenda?”
Nilimuuliza
hayo huku mimi mwenye naungulika moyoni mwangu
nikitamani kuwa ningelislimu kabla yake ili asiwe bora kupita mimi.
Kisha baba
yangu akasilimu, na mimi na mke wangu tukapanda juu
nyumbani kwetu, na mke wangu akaniambia: “Nadhani
uhusiani ulio baina yetu hautoweza tena kuendelea.”
Nikamuuliza:
“Kwa nini! Unadhani kuwa na
mimi pia nimeingia katika dini ya Kiislamu?”
Akaniambia: “Si hivyo, bali mimi ndiye
nitakayeingia katika dini ya Kiislamu.”
Nikamuambia:
“Kusema kweli hata mimi
pia nataka kusilimu.”
Nikatoka nje
ya nyumba yetu na kusujudu huku nikielekea kibla,
nikasema: “Mola wangu niongoze.” Nikauhisi
moyo wangu kuufungukia Uislamu, kisha nikaingia nyumbani na
kuwajulisha kuwa nishasilimu.
Kuingia
kwetu katika dini ya Kiislamu kunatokana na neema
kubwa iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu, kisha kutokana na mwenenedo na tabia njema
ya yule Muislamu aliyekuwa mlinganiaji mwema mwenye tabia njema. Upo msemo
kwetu usemao: “Usiniambie, bali nionyeshe"
No comments:
Post a Comment