Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Tuesday, June 18, 2013

Rais wa Gambia: Magharibi wanaua watu ovyo


Rais wa Gambia: Magharibi wanaua watu ovyo
Rais Yahya Jammeh wa Gambia amezikosoa vikali nchi za Magharibi kwa kufanya mauaji ya raia wasio na hatia katika nchi mbalimbali za dunia kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Rais Jammeh aliyasema hayo wakati akiwahutubia wakazi wa eneo la pwani la magharibi ya nchi hiyo na kuongeza kuwa, vita vya nchi za Magharibi dhidi ya ugaidi ni vita dhidi ya raia wasio na hatia. Akiashiria mauaji ya ndege za Marekani zisizo na rubani na mauaji yanayofanywa dhidi ya watu wanaodhaniwa tu kuwa ni magaidi, Rais Jammeh amesema, kwa hakika Magharibi wanafanya mauaji ya raia wasio na hatia duniani. Aidha amesisitiza kuwa, watu wengi wanaouliwa na ndege hizo za kigaidi zisizo na rubani si magaidi na kwamba, madai ya madola hayo ya kibeberu ya kupambana na ugadi hayana ukweli wowote na yamejaa upotoshaji.

Utata bomu la Arusha


Mlipuko wa bomu uliotokea Arusha na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi 70 limezua utata kutokana na hisia tofauti za viongozi mbalimbali nchini waliozungumzia suala hilo, huku Rais Jakaya Kikwete akisema haamini kama Watanzania sasa wamefikia hatua ya kuanza kuhasimiana kwa misingi ya kisiasa.
Hii ni mara ya pili kwa Jiji la Arusha kushambuliwa kwa bomu baada  ya lile lililorushwa kwenye Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi kwenye Parokia ya Olasiti wakati wa sherehe ya uzinduzi wake Mei 5, mwaka huu na kuua watu watatu na kujeruhi 64. Wakati Rais Kikwete akisema hayo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wamesema tukio hilo ni la kisiasa na lilipangwa.
Kufuatia tukio hilo, uchaguzi wa  kata nne za Arusha mjini umeahirishwa hadi Juni 30.

Sunday, June 16, 2013

Askari watatu wauawa katika mapigano Libya


Askari watatu wauawa katika mapigano Libya
Mapigano kati ya watu wenye silaha na jeshi pamoja na polisi ya Libya yamesababisha kwa uchache askari watatu kuuawa na wengine kujeruhiwa. Mapigano hayo yametokea baada ya watu wenye silaha mjini Bengazi mashariki mwa Libya, kufanya maandamano. Hayo yamethibitishwa na kikosi maalumu cha jeshi la nchi hiyo kinachofahamika kwa jina la ‘Swaiqah’ na kuongeza kuwa, mapigano hayo yamejiri mapema leo asubuhi ambapo katika mapigano hayo, kulitumiwa pia maguruneti na aina nyingine ya silaha nzito. Aidha habari zaidi zinasema kuwa, mapigano yalijiri baada ya waandamanaji waliokuwa na silaha kufanya shambulizi dhidi ya ngome ya kilojestiki ya kikosi hicho cha Saiqah na kwamba, hadi sasa bado milio ya risasi na milipuko inaendelea kusikika karibu na kambi ya kikosi hicho cha Saiqah na askari wa miamvuli hapo mjini Bengazi.

Watu wanne wauawa katika mlipuko Arusha, TZ


Eneo la mlipuko Arusha Juni 15 2013Kwa uchache watu watatu wanahofiwa kuuawa katika mlipuko wa bomu uliotokea mjini Arusha nchini Tanzania Jumamosi jioni katika mkutano wa kampeni wa chama kikuu cha upinzani Chadema.
Hujuma hiyo ya kigaidi ilijiri karibu saa 12 jioni kabla ya mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kumaliza kuhutubia wafuasi wa chama hicho katika Viwanja vya Soweto mjini Arusha. Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania Advera Senso amesema uchunguzi umeanzishwa kuhusu tukio hilo.

Misri yakata uhusiano wa kidiplomasia na Syria


 Misri yakata uhusiano wa kidiplomasia na Syria
Rais Mohammad Mursi wa Misri ametangaza kuwa nchi yake imekata kabisa uhusiano wa kidiplomasia na serikali ya Syria na kwamba ubalozi wa nchi hiyo mjini Cairo utafungwa mara moja. Rais Mursi amekuwa miongoni mwa viongozi wa Kiarabu waliochukua misimamo ya kufurutu mipaka dhidi ya serikali ya Syria. Kwenye hotuba yake hapo jana mjini Cairo, Mursi alisema atamuita nyumbani balozi wa Misri kufuatia uamuzi huo. Weledi wa mambo wanasema hatua ya Misri itazidi kuvuruga hali ya mambo nchini Syria haswa kwa kuzingatia kwamba Misri ilikuwa katika kundi la nchi 4 zilizopewa jukumu la kufuatilia kadhia ya Syria kwa njia za kidiplomasia. Nchi zingine kwenye kundi hilo ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki na Saudi Arabia. Huku hayo yakijiri, habari zinasema jeshi la Syria limezidi kusonga mbele katika mji wa Allepo na kwamba linaendelea kupata mafanikio makubwa. Hii ni katika hali ambayo, Marekani inapanga kuanza kutuma silaha kwa magaidi wa Syria ili kukabiliana na jeshi la nchi hiyo. Wakati huo huo, serikali ya Russia imeionya Marekani dhidi ya kuweka marufuku ya kupaa ndege huko Syria ikisema jambo hilo litakuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa.  

Monday, June 10, 2013

Matokeo ya uchaguzi Madagascar kutotambuliwa


Matokeo ya uchaguzi  Madagascar kutotambuliwa
Serikali ya Ufaransa imetangaza kwamba, haitotambua matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Madagascar iwapo wagombea fulani watashiriki Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, Philippe Lalliot amewataja rais wa sasa Andry Rajoelina, Lalao Ravalomanana; mke wa rais wa zamani aliyepinduliwa na rais wa zamani Didie Ratsiraka na kusema kwamba, kushiriki kwao kwenye uchaguzi ujao kutaendelea kuitumbukiza Madagascar kwenye mgogoro wa kisiasa ulioanza mwaka 2009 kufuatia mapinduzi yaliyomuondoa madarakani, Mark Ravalomanana. Msimamo wa Ufaransa unakwenda sanjari na ule wa Umoja wa Afrika AU na Jumuiya ya SADC ambazo zimetaka wanasiasa hao kuheshimu makubaliano ya Maputo yanayowazuia kuwania urais. Hii ni katika hali ambayo Mahakama ya kilele ya Madagascar imeamua kwamba watatu hao wanaweza kuwania urais kwani hakuna sheria ya nchi yao inayowazuia kufanya hivyo. Uchaguzi wa rais unatarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Askari wa Misri kutoshiriki uchaguzi hadi 2020


Askari wa Misri kutoshiriki uchaguzi hadi 2020
Askari polisi na wanajeshi wa Misri hawatashiriki kwenye uchaguzi wowote hadi mwaka 2020. Bunge la Misri limesitisha hadi mwaka 2020 mpango wa kuwapa wanajeshi na askari polisi wa nchi hiyo haki ya kupiga kura. Awali Naibu Waziri wa Ulinzi anayehusika na masuala ya sheria na katiba wa Misri alitoa pendekezo kwa kamati ya bunge la nchi  hiyo kuandaa mpango wa kuwapatia wanajeshi na askari polisi haki ya kupiga kura kwenye chaguzi mbalimbali zitakazofanyika nchini humo. Mahakama ya Katiba ya Misri mwezi Mei mwaka huu ilitangaza kuwa, kwa mujibu wa katiba mpya ya nchi hiyo, askari polisi na wanajeshi wana haki ya kushiriki kwenye chaguzi nchini humo.

Russia wataka zitumike Hijab mashuleni


Russia wataka zitumike Hijab mashuleniMkuu wa Muungano wa Wanawake wa Kiislamu nchini Russia amesisitiza juu ya kutumiwa vazi la Kiislamu Hijab ya Kiislamu katika maeneo ya umma bila ya kukinzana sheria hiyo ya Kiislamu na ile ya serikali ya Russia. Nailya Ziganshina amesema kuwa, utumiwaji wa vazi la Hijab kwa wanawake wa Kiislamu hakukinzani na sheria za sekta ya elimu nchini humo, yakiwemo mashule. Bi Nailya Ziganshina amesema kuwa, uvaaji huo wa Hijab unakwenda sambamba na mila, desturi na utamaduni wa kidini katika jamii ya nchi hiyo na kusisitiza kuwa, utumiaji wa Hijab haukinzani na mafunzo kwa watoto kwenye shule za nchi hiyo. Inafaa kuashiria hapa kuwa, ni miaka mingi sasa kwa serikali ya Russia kupiga marufuku uvaaji wa Hijab kwenye mikusanyiko ya umma na hasa mashuleni , suala ambalo limesababisha matatizo makubwa kwa wafuasi wa dini ya Kiislamu nchini Russia.

Saturday, June 8, 2013

Dk. Shein: Siitambui Kamati ya Maridhiano Zanzibar




Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema haitambui kamati ya maridhiano inayotetea Zanzibar kuwa na mamlaka kamili kama taifa linalojitegemea na kuwa na kiti katika Umoja wa Mataifa.

Dk. Shein alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume baada ya kukamilisha ziara ya kikazi nchini China juzi.

Alisema kwamba haitambui kamati hiyo lakini alikiri kukutana nayo mara tatu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ilikwenda kumpongeza Ikulu baada ya kuibuka na ushindi, mara ya pili walifika kumpa mkono wa pole kufuatia ajali ya meli ya Spice Islanders kabla ya kukutana nao kwa mara ya mwisho.

Saturday, June 1, 2013

Japan yaahidi msaada wa dola bilioni 32 kwa Afrika


Japan yaahidi msaada wa dola bilioni 32 kwa Afrika
Japan imeahidi kutoa msaada wa dola bilioni 32 kuzisaidia sekta za umma na za binafsi katika nchi za bara la Afrika ili kusaidia ustawi na maendeleo na kuyashajiisha mashirika na makampuni ya Kijapani kuwekeza barani humo katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Ahadi hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo wa Maendeleo ya Afrika (TICAD) na inajumuisha msaada rasmi wa maendeleo wa dola bilioni 14 na dola bilioni 6.5 za kusaidia sekta ya miundombinu. Kwa mujibu wa takwimu rasmi kiwango cha uwekezaji wa moja kwa moja wa Japan barani Afrika katika mwaka 2011 kilikuwa dola milioni 460 kikiwa ni cha chini mno kulinganisha na uwekezaji wa dola bilioni 3.17 uliofanywa na China katika nchi za bara hilo. Tangu achaguliwe kuwa Waziri Mkuu wa Japan mwezi Disemba mwaka uliopita, Shinzo Abe amechukua hatua kubwa katika uga wa diplomasia na amesisitiza kwamba anapanga kufanya safari katika nchi za Kiafrika mapema iwezekanavyo. Inafaa kuashiria kuwa viongozi wapatao 50 wa nchi za bara la Afrika wanashiriki katika mkutano wa siku tatu wa TICAD unaofanyika huko Yokohama karibu na mji mkuu wa Japan, Tokyo unaojadili masuala kadhaa yakiwemo ya maendeleo ya uchumi, kuleta amani na kupambana na uharamia…/

Serikali ya Ghana yaondoa ruzuku ya fueli


Serikali ya Ghana yaondoa ruzuku ya fueliSerikali ya Ghana imeondoa ruzuku ya bidhaa za fueli yakiwemo mafuta ya petroli, mafuta ya dizeli na gesi ili kusaidia kupunguza nakisi katika bajeti yake. Uamuzi huo umetangazwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Taifa ya Bidhaa za Petroli (NPA) Alex Mould ambaye amesisitiza kuwa utekelezaji wa uamuzi huo umeanza rasmi leo. Kutokana na kuchukuliwa hatua hiyo bei ya mafuta ya petroli itapanda kwa asilimia 3 na bei ya mafuta ya dizeli kwa asilimia 2. Ghana imekuwa moja ya nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi duniani tangu ilipoanza kuzalisha mafuta mwaka 2010, lakini serikali imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kudhibiti nakisi ya bajeti ya matumizi yake na uthabiti wa sarafu ya nchi hiyo ya cedi. Nakisi ya bajeti ilifikia kiwango asilimia 12.1katika mwaka uliopita wa 2012 mara mbili zaidi ya lengo lililowekwa la asilimia 6.7. Uamuzi wa kuondoa ruzuku katika bidhaa za fueli ulikuwa utekelezwe tangu mwaka uliopita nchini Ghana lakini ulicheleweshwa kwa sababu ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Disemba kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo John Atta Mills…/