Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imechukua uamuzi wa kumsamehe
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya asihudhurie vikao vya kesi inayomkabili
huko Hague nchini Uholanzi. Taarifa iliyotolewa jana na mahakama hiyo
imeeleza kuwa, Rais Kenyatta atahudhuria kikao cha ufunguzi wa
kusikiliza kesi yake na kikao cha mwisho cha kutolewa hukumu ya kesi
inayomkabili. Awali, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilimtaka Rais
Kenyatta ahudhurie mwenyewe kwenye kwenye vikao vyote ya kesi
inayomkabili, ambayo imepangwa kuanza kusikilizwa tarehe 12 Novemba
mwaka huu. Hivi karibuni, Umoja wa Afrika uliitaka Mahakama ya Kimataifa
ya Jinai kusitisha zoezi la kusikiliza kesi za Rais Kenyatta na Naibu
wake William Ruto, hadi pale viongozi hao watakapoondoka madarakani.
Viongozi hao wa Kenya wanatuhumiwa kwa kufanya uchochezi na kusababisha
mauaji ya watu wasiopungua 1,500 katika machafuko yaliyojiri Kenya mara
baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.