Mufti wa Oman amesema kuwa umma wa Kiislamu unapaswa kuwa na
urafiki, upendo na amani kuliko nyuma nyinginezo, kwani huo ndio ujumbe
wa umma huu. Akizungumza na vyombo vya habari pamoja na mwenyeji wake
Ayatullah Muhsin Araqi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya
Kuyakurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu mjini Tehran, Sheikh Ahmad
bin Hamad al Khalili amesema kuwa, umma wa Kiislamu unapita katika
kipindi nyeti mno na kusisitiza kuwa, hivi sasa umma huo unahitajia
kurejea haraka kwenye umoja na mshikamano. Akielezea mazungumzo yake
aliyoyafanya na viongozi wa kidini hapa nchini, Mufti Sheikh al Khalili
wa Oman amesema kuwa, maulamaa wakubwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
wametoa mapendekezo kadhaa ambayo yanahitajia kushughulikiwa kivitendo.
Ameongeza kuwa, mapendekezo hayo yanahitaji kuwekewa mikakati na hata
kuundwa kamati za kuyashughulikia ipasavyo. Mufti wa Oman amesisitiza
kuwa, kuna ulazima wa kufanyika mazungumzo hata kama na wapinzani kwa
lengo la kuondoa hitilafu zilizopo, kwani mazungumzo ndio njia pekee
inayoweza kumkinaisha mwanadamu na hatimaye kufuata njia ya saada.