Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa,
watoto 362 walio chini ya umri wa miaka mitano wamefariki dunia kutokana
na lishe duni nchini Niger. Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa,
watoto hao wamefariki dunia katika eneo la Zinder mashariki mwa Niger
kati ya mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu. Taarifa hiyo imeeleza
kuwa, asilimia 90 ya vifo katika maeneo ya Zinder, Magaria na Mirriah
inatokana na lishe duni kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Zinder ni mji wa pili kwa wingi wa watu nchini Niger, na eneo hilo
hukabiliwa mara kwa mara na ukosefu wa chakula unaosababishwa na ukame,
huku watoto na wanawake wakiwa wahanga wakubwa wa balaa hilo.