Mhadhiri mmoja wa kidini nchini
Saudi Arabia amehukumiwa kifungo cha miaka minane jela na kuchapwa
viboko 800 kwa kosa la kumnajisi bintiye mdogo wa miaka mitano na
kumtesa hadi kufariki dunia. Mahakama ya Saudi Arabia Jumatatu hii
ilimuamuru Fayhan al Ghamdi kumlipa mke wake wa zamani yaani mama wa
binti huyo fedha za diya ya damu dola za Kimarekani 270,000. Mke wa pili
wa mahdhiri huyo aliyekutwa na hatia ambaye naye ameshtakiwa kwa
kushiriki kwenye jinai hiyo amehukumiwa kifungo cha miezi kumi jela na
viboko 150. Binti huyo wa Saudia aliyekuwa na umri wa miaka mitano
alilazwa hospitali mwezi Disemba mwaka juzi akiwa na majeraha kadhaa,
michubuko, majeraha ya kuungua moto na kupasuka fuvu la kichwa.
Wanaharakati nchini Saudi Arabia na wa nchi za nje wamelaani vikali
jinai hiyo iliyofanywa na baba huyo kwa bintiye na kuitaja adhabu
iliyotolewa na mahakama ya nchi hiyo kwa mtenda jinai huyo kuwa ya
kiwango cha chini mno. Wanaharakati hao wamesema mtenda jinai huyo
alipaswa kufungwa jela maisha au kunyongwa ili iwe mfano kwa wengine.