Gazeti la Los Angeles Times
linalochapishwa nchini Marekani limeandika kuwa waasi wa M23 walioko
mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hujipatia takribani dola
milioni 500 kila mwaka kutokana na magendo ya dhahabu nchini humo.
Uchunguzi uliofanywa na taasisi ya kutetea haki za binadamu ya Enough
ya Washington nchini Marekani unaonyesha kuwa, waasi wa M23
waliojizatiti mashariki mwa nchi hiyo hufanya magendo ya madini ya
dhahabu na kujipatia mamilioni ya dola kila mwaka, pesa ambazo hutumiwa
kununulia silaha na kufanya jinai na mauaji ya halaiki katika eneo
hilo. Taasisi hiyo imeeleza kuwa, licha ya kinara wa kundi hilo Bosco
Ntaganda kupelekwa kwenye mahakama ya ICC kwa tuhuma za kutenda jinai za
kivita, lakini wasaidizi wake wamefanikiwa kutorosha kwa njia za
magendo dhahabu za Kongo na kuziuza nchini Imarati, kupitia nchi jirani
za Burundi na Uganda. Uchunguzi huo umeeleza kuwa, kila mwaka tani 12 za
magendo ya madini ya dhahabu yenye thamani ya dola milioni 500
hupelekwa nje ya nchi hiyo kinyume cha sheria.