Marekani imeitaka serikali ya Rwanda
kutoa ushirikiano utakaosaidia kukomeshwa mapigano huko Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo. Samantha Power, mwakilishi wa Marekani katika
Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Rwanda ikiwa ni nchi jirani na Kongo
inapaswa kuwa na nafasi ya moja kwa moja katika mchakato wa kuleta amani
na utulivu nchini Kongo. Bi. Power amesisitiza kwamba nchi zote za eneo
la Maziwa Makuu ya Afrika zinapaswa kufanya juhudi maradufu za
kuwatokomeza waasi walioko mashariki mwa nchi hiyo. Hapo jana ujumbe wa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliyataka makundi ya waasi
mashariki mwa Kongo kuacha kuendeleza machafuko katika eneo hilo. Inafaa
kuashiria hapa kuwa, mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Kongo na
waasi wa M23 kwa upatanishi wa Uganda bado yanaendelea, lakini hadi sasa
hayajakuwa na natija yoyote ile.