Polisi ya Kenya imetangaza kuwa iko tayari kutoa kitita cha
shilingi laki tano za nchi hiyo ambazo ni sawa na dola 5, 827 kwa mtu
atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa mwenye gari linalosadikiwa
kutegwa mabomu kwenye shambulio lililofanywa zaidi ya wiki mbili
zilizopita kwenye jumba la biashara la Westgate jijini Nairobi, Kenya.
Mkuu wa kikosi maalumu cha kupambana na ugaidi nchini Kenya ameeleza
kuwa, gari hilo linashukiwa lilikuwa limesheheni mada za milipuko na
silaha na kuongeza kuwa kikosi hicho bado kinaendelea kumsaka mmiliki wa
gari hilo. Amesema kuwa, awali mmiliki wa gari hilo alikuwa Mkenya
mwenye asili ya Kisomali. Kundi la al Shabab la nchini Somalia
lilitangaza kuhusika na shambulio hilo lililopelekea watu wasiopungua 67
kuuawa ingawa hadi sasa watu wengine 39 waliokuwepo kwenye eneo hilo
hawajulikani walipo. Kundi la al Shabab limeitaka serikali ya Kenya
kuondoa majeshi yake nchini Somalia, kinyume cha hivyo itakabiliwa na
mashambulio mengine kwenye maeneo nyeti ya nchi hiyo. Rais Uhuru
Kenyatta wa Kenya amesikika akisema kuwa, serikali ya Nairobi
haitayaondoa majeshi yake nchini Somalia hadi pale hali ya amani na
utulivu itakaporejea nchini humo.