Mabudha wenye misimamo mikali wanaendelea kuwatesa na
kuwanyanyasa Waislamu wa Myanmar huku serikali ya nchi hiyo ya kusini
mashariki mwa Asia ikionekana kuwatelekeza Waislamu hao. Leo Jumapili
vyombo vya habari vimeripoti kuwa, makundi ya Mabudha wenye chuki za
kidini wamevamia nyumba tano za Waislamu katika mji wa Kyaung Gone,
yapata kilomita 50, kaskazini magharibi mwa mji mkuu Yangon na kuzichoma
moto nyumba hizo. Vyombo vya habari vya serikali vimedai kuwa polisi
wamewatia mbaroni Mabudha 40 kwa kushambulia nyumba za Waislamu. Polisi
wanasema kuwa, tarehe 2 mwezi huu wa Oktoba, Waislamu watano wakiwemo
wanaume wanne na mwanamke mmoja waliuliwa kikatili katika kijiji cha
Thabyuchaing baada ya mamia ya Mabudha wenye misimamo mikali kuvamia
kijiji hicho. Wiki iliyopita pia, bikizee mmoja aliuliwa kwenye eneo la
Thandwe, katika jimbo la Rakhine baada ya zaidi ya Mabudha 700
kumiminika mitaani kuwasaka Waislamu na kuchoma moto nyumba zao.
Mashirika ya haki za binaadamu yanailamumu serikali ya Myanmar kwa
kudharau wajibu wake wa kuwalinda Waislamu.