Wafanyakazi wasiopungua
milioni moja wa serikali ya shirikisho ya Marekani wamelalamikia hatua
ya nchi hiyo ya kuwapa likizo bila ya mishahara yao. Taarifa zinasema
kuwa, wafanyakazi hao wamelalamikia vikali hatua ya kuendelea kubaki
nyumbani kwa siku ya nne mfululizo bila ya kulipwa mishahara yao na
wanataka warejeshwe kazini haraka iwezekanavyo. Fikra za walio wengi na
wafanyakazi nchini humo wanajihesabu kuwa ni mateka na wahanga wa
mivutano ya kisiasa ndani ya Baraza la Kongresi. Hapo jana, Rais Barack
Obama wa Marekani alisisitiza kuwa kuendelea kusimamishwa idara za
shirikisho ni pigo kubwa kwa nchi na uchumi wa Marekani. Taarifa
zinasema kuwa, thuluthi mbili ya wafanyakazi wa serikali akiwemo Obama
mwenyewe, watalazimika kufanya kazi bila ya malipo hadi mgogoro wa
bajeti kati ya Warepublican na Wademokrat utakapotatuliwa. Wademokrat na
Warepublican wanazozana juu ya miswada iliyopendekezwa na serikali ya
Obama juu ya marekebisho ya bima ya afya.