Ripoti iliyotolewa na Umoja wa
Mataifa inaonesha kuwa, Watanzania ni miongoni mwa watu wasio na furaha
na waliokata tamaa hapa duniani. Ripoti hiyo imeitaja Tanzania kuwa ni
miongoni mwa nchi 10 za mwisho duniani kati ya nchi 156 zilizofanyiwa
utafiti huo. Upatikanaji wa huduma za jamii, mtazamo wa watu kuhusu
rushwa, umri wa kuishi, ukosefu wa kazi, pato la taifa na ukarimu wa
watu katika nchi husika, ni baadhi ya vigezo vilivyoangaliwa wakati wa
kuandaa ripoti hiyo. Taarifa hiyo imezitaja nchi tano za Denmark,
Norway, Uswisi, Uholanzi na Sweden kuwa ndizo zinazoongoza kwa watu wake
kuwa na furaha zaidi duniani, huku Angola ikishika nafasi ya kwanza
Afrika na ya 61 duniani. Kwa upande wa Afrika Mashariki, wananchi wa
Uganda ndio walionekana kuwa na furaha zaidi katika ripoti hiyo kwani
nchi hiyo imeshika nafasi ya 120 wakifuatiwa na Kenya iliyoshika nafasi
ya 123, Tanzania nafasi ya 151, Rwanda nafasi ya 152 na Burundi ni ya
mwisho Afrika Mashariki huku ikiwa inashikilia nafasi ya 153 duniani.
Hata hivyo, Waziri wa Kazi na Ajira wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Gaudensia Kabaka ameeleza kushtushwa na ripoti hiyo akisema kuwa ni
asilimia 11.7 tu ya Watanzania wasio na ajira na kwamba, wale wanaofanya
kazi, wanapata huduma zote za msingi, ikiwa ni pamoja na kwenda likizo
na mishahara inayolingana na taaluma zao na kusisitiza kwamba, hafahamu
ni vigezo vipi vimetumika katika ripoti hiyo.