Kundi la wanamgambo wa ash Shabab la Somalia limetishia kufanya
mashambulizi mengine makali nchini Kenya ikiwa ni siku chache tu baada
ya kundi hilo kuua makumi ya watu katika jumba la biashara la Westgate,
mjini Nairobi. Wanamgambo hao wamedai kama tunavyonukuu taarifa yao
kwamba: "Tutawashambulia Wakenya katika sehemu ambazo zitawaumiza zaidi,
na tutaigeuza miji yao kuwa makaburi, na mito ya damu itatiririka mjini
Nairobi." Vitisho hivyo vya ash Shabab vimekuja baada ya Kenya kukataa
kuondoa wanajeshi wake nchini Somalia. Katika taarifa yake hiyo,
wanamgambo wa ash Shabab aidha wamesema kama ninavyowanukuu: "Uamuzi wa
serikali ya Kenya wa kuendelea kuweka vikosi vyake nchini Somalia ni
dalili kuwa hawakupata somo linalotakiwa katika mashambulizi ya
Westgate." Hivi karibuni, karibu watu 70 waliuliwa na wanamgambo wa ash
Shabab wakati wanamgambo hao walipovamia jumba la biashara la Westgate
mjini Nairobi na hadi hivi sasa hatima ya makumi ya watu wengine
haijajulikana. Hivi sasa kuna wanajeshi 4,000 wa Kenya kusini mwa
Somalia ambako wanapambana na wanamgambo wa ash Shabab wenye mfungamano
na mtandao wa al Qaida. Wanajeshi wa Kenya wako nchini Somalia kama
sehemu ya kikosi cha Umoja wa Afrika kinacholinda amani nchini humo.