Wafanya ziara wasiopungua watano wameuliwa leo na wengine
wasiopungua 17 wamejeruhiwa katika eneo la Qahira kaskazini mwa mji mkuu
wa Iraq, Baghdad baada ya gaidi mmoja kujiripua ndani ya msafara wa
wafanya ziara hao waliokuwa wakielekea kwenye haram ya Imam Muhammad Al-
Jawad AS kuomboleza siku aliyouliwa shahidi Imamu huyo wa tisa wa
Waislamu wa madhehebu ya Shia. Wakati huohuo wanafunzi 14 pamoja na
mwalimu wao mkuu wameuliwa katika shambulio jengine la kigaidi
lililofanywa leo pia ndani ya uwanja wa shule moja ya msingi huko
kaskazini mwa Iraq. Lori lililosheheni mada za miripuko liliingizwa na
kuripuka ndani ya uwanja wa kuchezea watoto wa shule moja ya msingi
katika mji wa Tel Afar ulioko kilomita 70 kaskazini magharibi mwa wa
Mosul na kusababisha vifo vya watoto hao pamoja na mwalimu wao mkuu.
Zaidi ya watu elfu sita wameuawa nchini Iraq tangu ulipoanza mwaka huu
wa 2013, elfu moja kati yao wakiwa wamepoteza maisha katika mashambulio
ya kigaidi yaliyofanywa nchini humo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tu
uliopita wa Septemba. Hapo jana watu wasiopungua 60 waliuawa na makumi
ya wengine kujeruhiwa katika milipuko miwili iliyolenga Waislamu wa
madhehebu ya Shia waliokuwa wakienda kuzuru haram tukufu ya Imam Jawad
AS katika viunga vya mji mkuu wa Iraq, Baghdad.