Wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika
na wale wa Umoja wa Mataifa watakutana leo Addis Ababa mji mkuu wa
Ethiopia kwenye kikao cha kila mwaka, ambapo mwaka huu ajenda kuu
itakuwa ni kuujadili kwa kina mgogoro wa mpaka kati ya nchi za Sudan na
Sudan Kusini. Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Afrika imeeleza kuwa,
licha ya mgogoro wa Sudan mbili, wajumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja
wa Afrika watajadili pia hali ya mambo katika eneo la Maziwa Makuu ya
Afrika, Pembe ya Afrika, Jamhuri ya Afrika ya Kati na eneo la Sahel.
Sudan Kusini ambayo awali ilikuwa sehemu ya Sudan, ilijitangazia uhuru
wake mwezi Juni 2011. Hata hivyo, nchi hizo mbili zimetumbukia kwenye
mgogoro mkubwa baada ya kila upande kudai haki ya umiliki wa maeneo
matano ya mpakani na hali kadhalika tuhuma za kila upande za kuwaunga
mkono waasi wa upande wa pili. Hadi sasa, Sudan imeshaishitaki Sudan
Kusini mara tano kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa
kuwaunga mkono wapinzani wa serikali ya Khartoum.