Taasisi mbalimbali za Palestina
zimelaani njama ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kutaka kujenga
hekalu katika eneo la mashariki ya msikiti mtukufu wa al Aqsa. Baraza
Kuu la Kiislamu, Baraza la Waqfu na Masuala ya Kiislamu na Baraza la
Fatwa la Quds tukufu yametoa taarifa ya pamoja leo ambapo mbali na
kufichua, yamelaani pia njama hiyo ya utawala wa Kizayuni dhidi ya kibla
cha kwanza cha Waislamu. Taarifa hiyo imeashiria kubadilishwa sura ya
sehemu ya msikiti huo ya al Buraq na vilevile kujengwa njia ya mabasi
yaendayo kwa kasi katika eneo la kati ya Jabalu-turi na Babul-asbat, na
kueleza kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa lengo la kuyayahudisha maeneo
matakatifu na kufuta athari za Kiislamu, kitu ambacho hakikubaliki.
Taarifa ya taasisi hizo za Palestina imeashiria mpango wa Israel wa
kujenga hekalu katika eneo la sehemu moja ya tano ya msikiti wa Alqsa na
kusisitiza kwamba msikiti huo kidini, kisiasa na kimamlaka hauna
uhusiano wowote na Mayahudi na kwamba eneo hilo takatifu la Baitul
Muqaddas ni milki ya Waislamu wote duniani. Sambamba na kutoa indhari
kwa utawala wa Kizayuni juu ya mas-ulia utakayobeba kwa hatua yoyote ya
kuuvunjia heshima msikiti mtukufu wa al Aqsa, taarifa hiyo imetoa wito
pia kwa Ulimwengu wa Kiislamu na wa Kiarabu kutimiza wajibu walionao juu
ya msikiti huo mtakatifu pamoja na Quds tukufu…/