Viongozi wa nchi wanachama
wa Umoja wa Afrika AU wanaokutana makao makuu ya umoja huo mjini Addis
Ababa, Ethiopia wameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC
isiwafungulie mashtaka viongozi wa nchi za Afrika wanapokuweko
madarakani. Viongozi hao aidha wameitaka mahakama hiyo iakhirishe kesi
za marais wa Uhuru Kenyatta wa Kenya na Omar al Bashir Sudan. Mkuu wa
Kamisheni ya Umoja wa Afrika Bi Dlamini Zuma, amesema Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai zinapaswa
kuakhirisha haraka usikilizaji wa kesi za viongozi wa Kenya
waliochaguliwa na wananchi. "Baraza la Usalama na ICc zinapaswa
kushirkiana nasi ili kuwezesha uongozi wa Kenya uliochaguliwa na
wananchi uweze kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kwa kulizingatia kwa
haraka suala la uakhirishaji kesi zinazosikilizwa na ICC dhidi ya Rais
na Makamu wa Rais wa Kenya", amesema Zuma. Mbali na Rais, Naibu wa Rais
wa Kenya William Ruto naye pia anakabiliwa na kesi katika Mahakama ya
Kimataifa ya Jinai yenye makao yake the Hague, Uholanzi ya kuhusika na
kuongoza machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2007
yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200…/