Polisi ya Kenya imetangaza kuwa,
watu wanne akiwemo Sheikh Ibrahim Ismail Rogo wameuawa baada ya kupigwa
risasi na watu wasiojulikana ndani ya gari dogo jana usiku huko mjini
Mombasa. Taarifa ya Polisi ya Kenya imeeleza, Sheikh Ibrahim Rogo
alikuwa mrithi wa Sheikh Aboud Rogo ambaye naye aliuawa na familia yake
kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwezi Agosti 2012. Mauaji ya
Sheikh Ibrahim Rogo ambayo yameutikisa mji wa Mombasa, yametokea baada
ya kupita takriban wiki mbili tokea kundi la al Shabab lilipovamia na
kuua watu wasiopungua 63 na kujeruhi mamia ya wengine kwenye jengo la
maduka ya biashara la Westgate jijini Nairobi. Baadhi ya wananchi wa
Mombasa wanakituhumu kikosi maalumu cha kupambana na ugaidi kuwa ndicho
kilichotekeleza mauaji hayo. Sheikh Ibrahim Rogo ambaye alikuwa akitoa
mihadhara kwenye Msikiti wa Musa mjini Mombasa alituhumiwa na jeshi la
polisi kuwa anawachochea vijana wa Kiislamu kujitumbukiza kwenye
makundi ya kigaidi. Polisi ya Kenya imesema kuwa, Gaddafi Mohammad,
Issa Abdallah na Omar Abu Rumeisa ni miongoni mwa waliouawa, naye Salim
Aboud alinusurika kwenye shambulio hilo.