Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Tuesday, November 20, 2012

TUHUMA ZA UAMSHO KUNYOLEWA NDEVU WAKIWA GEREZANI, MAHAKAMA KUU YAWASHAURIWA WAFUNGUE KESI MADAI


Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
 Mahakama Kuu ya Vuga mjini Zanzibar imetoa ushauri kwa Viongozi wa Jumuiya mbili za Kiislam Zanzibar wanaotuhumiwa kwa makosa ya kuhatarisha usalama wa Taifa ya kutotendewa haki wakiwa Gerezani wafungue kesi ya madai.
Ushauri huo umetolewa na Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mh. George Kazi mara baada ya kupitia kwa makini maombi ya watuhumiwa hao yaliyofikishwa mbele yake Novemba 8, mwaka huu kupitia kwa mawakili wa watuhumiwa hao.
Kesi hiyo inawakabili watu wanane akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar
na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uamsho Sheikhe Mselem Ali Mselem.
Wengine katika kesi hiyo ni Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Azan Khalid Hamdan, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman na  Ghalib Ahmada Omar.
Akitoa uwamuzi huo, Mh. Kazi amesema watuhumiwa wana haki ya kufungua kesi mahakama kuu ya kile wanachokilalamikia na kwamba mahakama kuu itakuwa na uwamuzi wa kuyasikiliza madai yao tofauti na kesi ya msingi kwa watuhumiwa.

Kwa kupitia kwa Mawakili wao, watuhumiwa hao walidai kuwa wananyimwa uhuru na haki zao za msiki ikiwa ni pamoja na kupigwa marufuku yfugaji wa ngevu wakiwa rumande chuo cha Mafunzo (magereza). 
Watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa mashta manne yakiwemo ya kutoa lugha za uchochezi, kufanya vurugu na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara mjini Zanzibar.
Wakizungumzia kesi ya msingi kwa watuhumiwa hao, Waendesha Mashtaka wa Serikali walidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamili na kwamba wanaomba siku nyingine ya kutajwa.
Mrajisi huyo wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, ameiahirisha kesi hiyo hadi Alhamisi Novemba 29, mwaka huu itakapotajwa tena.
Kama kawaida, Jeshi la Polisi lilifunga barabara zote za kuingia na kutoka mahakamani na kuimarisha ulinzi ndani na nje ya mahakama hiyo ambapo kila pembe walionekana Makachero wa Polisi na Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia.
 Nao baadhi ya wananchi waliofika makahakamani hapo waliwataka waandishi wa habari kuandika ukweli kuhusiana na kesi hiyo ili kuinusuru nchi yetu kukumbwa na machafuko.
 Watuhumiwa hao wanatetewa na Mawakili wa kujitegemea Bw. Salum Toufik na Bw. Abdallah Juma Kaka huku kwa upande wa Serikali ikiwakilishwa na Bw. Ramadhani Nassibu na wenzake wawili kama Waendesha Mashtaka.

No comments:

Post a Comment