Jumanne tarehe 27 Novemba ilikuwa siku ya umwagaji damu mkubwa
kwa Iraq na Wairaqi. Milipuko minane iliitikisa miji mbalimbali ya ya
nchi hiyo na kwa akali watu 29 walipoteza maisha yao na zaidi ya mia
moja na ishirini kujeruhiwa. Miji ya Kirkuk, Al Anbar na Baghdad ndiyo
iliyolengwa na magaidi hapo jana. Polisi ya Iraq imelinyooshea kidole
cha tuhuma kundi la mtandao wa al-Qaeda. Hata hivyo al-Qaeda ambalo ni
kundi lililolelewa na Marekani, ni moja tu kati ya makumi ya makundi ya
kigaidi ambayo yanaendesha harakati zao nchini Iraq. Inapaswa pia
kuongeza katika majimui hiyo, harakati za kisiasa zinazoipinga serikali
ya Baghdad na Noury al-Maliki mwenyewe, Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Ushirikiano wa makundi na harakati hizi za kisiasa na magaidi, hadi sasa
umeandaa uwanja wa kutokea milipuko na operesheni kadhaa za kigaidi
nchini humo. Ni jambo linaloeleweka wazi kuwa, mrengo wa al-Iraqiya
unaoongozwa na Iyad Allawi, una uhusiano wa karibu na makundi amilifu ya
kigaidi nchini Iraq. Nchi kama Saudi Arabia, Qatar na Jordan ambazo
hazifurahishwi na muundo wa kisiasa wa Iraq na hata Waziri Mkuu Noury
al-Maliki, daima zimekuwa zikiuunga mkono mrengo wa al-Iraqiya na
makundi amilifu ya kigaidi katika nchi hiyo na kuyapatia misaada ya kila
upande. Nchi hizo, zimekuwa zikiutumia mrengo huo kama wenzo wa
mashinikizo dhidi ya al-Maliki na ikilazimu walitumie kundi hilo kutoa
pigo kwa serikali ya Baghdad na hivyo kuutilia alama ya swali utendaji
wa al-Maliki. Hadi sasa makumi ya magaidi ambao ni raia wa Saudia,
Imarati na Jordan wametiwa mbaroni. Huu ni ushahidi kwamba, Iraq
inakabiliwa na njama kali pia kutoka kwa baadhi ya nchi za Kiarabu.
Nchi hizi za Kiarabu ambazo aghlabu zina uhusiano baridi na Iraq
daima zimekuwa zikihesabiwa kuwa tishio kwa uthabiti wa kisiasa na
kiusalama wa nchi hiyo. Pamoja na hayo, akthari ya weledi wa masuala ya
kisiasa wanaamini kwamba, kuibuka wimbi jipya la machafuko huko Iraq
bila shaka kutakuwa na uhusiano wa namna fulani na matukio ya Mashariki
ya Kati yakiwemo ya Syria. Jumanne ya jana magari manane yaliyotegwa
mabomu ndani yake yaliripuka katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. Syria
nayo ilikuwa na hali kama hiyo hiyo. Hii inaonesha kuwa, kuna njama za
pamoja ambazo zinatekelezwa dhidi ya nchi hizo. Inaonekana kuwa, mamluki
wa nchi za Kiarabu na makundi ya kigaidi ambayo yanapatiwa misaada ya
kifedha na silaha na mhimili wa pamoja wa Kimagharibi-Kiarabu ulio dhidi
ya Syria unataka kuishughulisha Iraq na Syria kwa migogoro ili uweze
kunufaika na anga hiyo kwa maslahi yake. Iraq ni miongoni mwa nchi za
eneo la Mashariki ya Kati ambazo hadi sasa zimekataa kuungana na mhimili
ulio dhidi ya Syria. Hapana shaka kuwa, jambo hilo limeikasirisha mno
Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu ambazo ziko pamoja na Washington
katika kadhia ya Syria. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa,
moja ya sababu za kuzusha machafuko na sokomoko nchini Iraq ni kutaka
kuilazimisha nchi hiyo ikubaliane na matakwa ya nchi za Magharibi
kuhusiana na migogoro ya Mashariki ya Kati.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment