Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Tuesday, November 6, 2012

Mradi wa kueneza chuki dhidi ya Iran, ni sababu ya kuuzwa silaha za mabilioni ya dola kwa nchi za Kiarabu


Mradi wa kueneza chuki dhidi ya Iran, ni sababu ya kuuzwa silaha za mabilioni ya dola kwa nchi za Kiarabu
Katika toleo lake la hivi karibuni kabisa, gazeti la Independent la nchini Uingereza limenukuu duru moja ya ngazi za juu ya Uingereza ikisema kuwa, London inachunguza namna ya kutuma ndege zake za kisasa za kivita aina ya Typhoon katika eneo la Ghuba ya Uajemi kwa ajili ya eti kuzilinda nchi za eneo hili zisishambuliwe na Iran. Gazeti hilo limefichua pia kuwa, ndege hizo za kivita za Uingereza huenda zikatumwa katika eneo la Ghuba ya Uajemi kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusiana na suala la kutia nguvu
uwepo wa kijeshi wa Britani katika eneo hili. Gazeti hilo la Independent la Uingereza pia limenukuu duru za ngazi za juu za kijeshi na kisiasa zikithibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, huenda ndege hizo zikapelekwa kwenye kambi ya jeshi la anga ya adh Dhafar, kusini mwa Abu Dhabi ambayo hivi sasa ina ndege za kivita za Ufaransa na Marekani. Uuzaji wa silaha kubwa na ndogo kwa nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi ulianza tangu miongo miwili iliyopita na hivi sasa umegeuka kuwa mashindano ya uuzaji wa silaha kati ya madola makubwa duniani. Mtandao wa Intaneti wa gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post hivi karibuni uliripoti kuwa, Marekani ina nia ya kuziuzia silaha nchi za Saudi Arabia, Kuwait, Oman, Imarati na Qatar zenye thamani ya dola bilioni sitini. Ripoti hiyo ilisema kuwa, Marekani imekusudia kuuza ndege 82 za kijeshi aina ya F-15 zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 30 kwa Saudi Arabia pekee. Wakati huo huo Kuwait nayo ina nia ya kuimarisha jeshi lake la anga kwa kununua ndege za aina hiyo hiyo kutoka kwa Marekani. Kuwait aidha imekusudia kununua ndege nyingine kumi za kutilia mafuta angani kutoka kwa Marekani. Yote hayo yanafanyika kwa madai ya kuweko hatari ya kushambuliwa na Iran. Uenezaji chuki dhidi ya Iran ni mradi unaopigiwa chapuo sana na vyombo vya habari vya Magharibi ili iwe rahisi kuchota mabilioni ya dola za wananchi wa nchi za Kiarabu zinazotokana na utajiri wa mafuta wa nchi zao. Taasisi ya Amani ya Kimataifa ya Uswisi imesema kuhusu ushindani wa kuziuzia silaha nchi za Kiarabu kwamba ununuaji wa silaha wa nchi za Mashariki ya Kati umepanda kwa ajili 20 katika kipindi cha miaka mitano ya kuanzia mwaka 2004 hadi 2009. Kitu kinachotoa mguso hapa ni kwamba, madola manne makuu yanayoziuzia silaha nchi za Kiarabu yaani Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, ndiyo hayo hayo yanayoeneza propaganda za uongo kwamba eti Iran ni tishio kwa nchi za eneo hili na eti ina nia ya kuzivamia kijeshi. Nchi kama Umoja wa Falme za Kiarabu ni ya nne kwa kununua silaha nyingi zaidi baada ya China, India na Korea Kusini. Tab'an kama tutaangalia idadi ya watu milioni 6 wa Imarati na kulinganisha kiwango cha ununuzi wa silaha cha nchi hiyo tutaona kuwa inashika nafasi ya kwanza kwa kununua silaha kwa wingi duniani. Watu wanaokosoa ununuzi wa namna hiyo wa silaha wanasema kuwa, nchi za Kiarabu zinajilimbikizia silaha ambazo hakuna wakati wanazitumia huku ndugu zao wa Palestina kama vile katika Ukanda wa Ghaza wakiendelea kukabiliwa na ukandamizaji wa kila namna wa adui mkubwa wa Waislamu yaani utawala wa Kizayuni wa Israel. Wakosoaji hao wanazungumzia uzoefu ulioshuhudiwa hasa katika mapinduzi ya hivi karibuni ya wananchi dhidi ya tawala kadhaa za kidikteta za vibaraka wa Magharibi katika ulimwengu wa Kiarabu na kusema kuwa, kujilimbikizia silaha na kujipendekeza kwa madola ya kibeberu si kinga ya kuzilinda tawala hizo zisipinduliwe.

No comments:

Post a Comment