Mkutano kati ya Tanzania na Malawi
wa kujadili suluhu ya mgogoro wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa umeingia siku
yake ya pili jijini Dar es Saalam huku washiriki wakitoa mapendekezo
mbalimbali kuhusu jinsi ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo. Mkutano huo
unaowahusisha wataalamu kutoka Wizara na Idara mbalimbali za Serikali za
Tanzania na Malawi, unatarajia kuandaa mazingira ya kufanyika mkutano
wa ngazi ya mawaziri baadaye hapo kesho. Akifungua Mkutano huo, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania,
Bw. John Haule alisisitizia umuhimu wa wajumbe kutoka nchi zote mbili
kujadili na kupendekeza njia zitakazosaidia kupata suluhisho la kudumu
la mgogoro huo. Aidha, Bw. Haule aliweka bayana kuwa serikali ya
Tanzania ina dhamira ya dhati kufanya kazi pamoja na serikali ya Malawi
kutafuta suluhu ya mgogoro huo jambo ambalo pia lilisisitizwa na Bw.
Julius Chisi, Kiongozi wa Ujumbe wa Malawi. Mazungumzo kati ya nchi
mbili hizo yalivunjika mwezi Septemba baada ya Tanzania kutangaza ramani
mpya ya nchi hiyo. Malawi ilijiondoa kwenye mazungumzo hayo kwa madai
kwamba ramani hiyo mpya ya Tanzania inajumuisha eneo la Ziwa Nyasa
linaloendelea kuzozaniwa na pande mbili hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment