Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Monday, November 26, 2012

MAALIM SEIF SHARIF HAMAD AFUNGUA MKUTANO WA ARIPO ZANZIBAR BEACH RESORT


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akitoa Hotuba ya Ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa Baraza la Utawala la ARIPO linaloratibu na kusimamia haki za Mali za wabunifu Barani Afrika huko katika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort ilioko Mazizini Nje ya Mji wa Zanzibar.
PICHA NA YUSSUF SIMAI-MAELEZO ZANZIBAR.
………………………………………………………………………………….
                    NA RAMADHANI ALI/HABARI MAELEZO
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema ipo haja kwa  Baraza la Utawala linaloratibu na kusimamia haki za Mali za Ubunifu Afrika (ARIPO) na Jumuiya za kimataifa zinazosimamia sekta hiyo kuandaa  miongozo na kuimarisha  mikakati itakayo wabana  wezi wa haki miliki.

 Amesema uporaji wa haki miliki umekuwa ukiendelea kwa kasi  Duniani kote na kupelekea hasara kwa vitega uchumi vya Wasanii, Watengenezaji filamu na muziki ambapo  hupelekea hasara kwao na mataifa yao kwa jumla.
 Makamu wa kwanza wa Rais ameeleza hayo alipokuwa akifungua mkutano wa 36 wa ARIPO unaofanyika kwa mara ya kwanza Zanzibar katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Mbweni.
 Amesema Tasnia ya haki miliki inamchango mkuwa katika kukuza maendeleo ya kiuchumi ndani ya nchi na kuongeza maslahi kwa wamiliki wa kazi za ubunifu  iwapo zitalindwa.
 Amewaeleza wajumbe wa Mkutano huo kwamba  Zanzibar imeamua kuanzisha utaratibu wa Haki Miliki kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ya kuweka alama ya utambulisho (nembo) kwa  zao lake la  karafuu na viungo  ili kuimarisha usafirishaji wa mazo hayo na kuongeza pato la taifa.
 Amesema Serikali kwa msaada mkubwa wa Shirika la Mali za Ubunifu Duniani (WIPO)  zinaandaa utaratibu mwengine wa kuweka  sera ya kulinda mali za ubunifu nchini ili kuzilinda na maharamia wa kazi hizo.
 Makamu wa kwanza wa Rais ameipongeza ARIPO kwa kuendeleza  utaratibu wa kuandaa mafunzo ya muda mrefu na mfupi wa kuzijengea uwezo  Taasisi na wadau wengine wanaohusika na kazi za ubunifu katika Bara la Afrika.
 Hata hivyo amewaeleza wajumbe wa  Baraza la Utawala la ARIPO kwamba masuala ya Utawala wa mali za ubunifu na haki miliki sio  ya Muungano na kila upande unahaki ya kuandaa utaratibu na sera zake zinazokubaliana na mazingira yao licha ya kuwa na lengo moja.
 Maalim Seifa amelipongeza Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Korea (KOICA) kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuisaidia ARIPO na nchi wanachama wa Baraza hilo kuimarisha mfumo wa Teknolojia ya Habari na kupunguza tofauti iliyopo kati ya mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea duniani.
 Mwenyekiti wa Mkutano huo  ambae ni Naibu Mrajisi nchini Ghana Bi Jemima Oware amesema ulinzi wa mali za ubunifu na masuala ya haki miliki yanapewa umuhimu mkubwa katika Baraza la ARIPO ili kunyanyua maslahi kwa wabunifu.
 Mkutano huo wa wiki moja unahudhuriwa na wajumbe zaidi ya 75 wakiwemo nchi 18 wanachama wa  ARIPO, Shirika la Dunia la Mali za Ubunifu WIPO, Wawakilishi wa Jumuiya ya Ulaya, Shirika la Kimataifa la KOICA na wajumbe kutoka nchi  waalikwa.

No comments:

Post a Comment