Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Thursday, November 8, 2012

Mawakili walalamikia kutotoendewa haki wateja wao



wakili NA SALMA SAID
MAWAKILI wa Sheikh Farid Hadi Ahmed na wenzake wameilalamikia ukiukwaji wa haki za binaadamu wanaofanyiwa wateja wao kwa wahanyimwa haki zao za msingi na kulalamikia hali mbaya ya gerezani tangu kukamatwa kwao wiki mbili zilizopita.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama Wakili wa watuhumiwa hao Abdallah Juma alisema wateja wao ambao ni Sheikh Farid na wenzake saba wamekuwa wakikoseshwa haki za msingi huko gerezani wakati bado wateja wao ni watuhumiwa na hawajatiwa hatiani.
Mawakilishi hao ni Abdallah Juma na Salim Tawfik aliliambia gazeti hili kwamba hali ya wateja wake ndani ya gereza hairidhishi kutokana na kuwa hawaruhusiwi kuonanana mtu yeyote tokea walipofikishwa gerezani hapo ambapo ni siku 16 hawajaruhusiwa kubadilisha nguo kwa kuwa wamekataliwa kuletewa nguo kutoka nyumbani.
Mbali na malalamiko hayo Juma alisema wateja wake pia wamelelemikia kulazwa sakafuni bila ya chochote katika siku nne za mwanzo mfululizo pamoja na kulazimika kujisaidia katika ndoo (mtondoo). Na chakula wanachopewa baadhi yao hawawezi kukila kutokana na kuwa na maradhi ya vidonda vya tumbo (ulsa).
“Nadhani uongozi wa magereza pamoja na polisi wanahitaji kuheshimu haki za binaadamu kwa sababu hawa bado ni watuhumiwa na wanapaswa kupewa haki zao za msingi. Kwa nini watuhumiwa wanyimwe haki ya kuonana na jamaa zao basi hata wake zao wanawakatalia, lakini tokea siku walipofika hawajaonana na mtu sisi ndio wa mwanzo kuonana nao lakini kibaya zaidi ni kuwa hawajabadilisha nguo tokea siku walipofika sasa hiyo tunaona sio vizuri, hii haipendezi na binaadamu haifai kufanyiwa hivyo” alilalamikia Wakilishi Juma.
Alisema kwa maelezo yao amethibitisha kuwa hawatendewi haki kwa kuwa hali inaonesha kwamba wananyimwa kutembelewa na watu wao maana hata mawakili awali walikataliwa kuonana nao na wakatakiwa kuomba kwa kuandika barua maalumu ili waweze kuwaona.
“Wakili ana haki ya kuonana na mteja wake lakini tulikataliwa siku ambayo tumetaka kuwaona wakatwambia tuandike barua wakati hiyo sio haki kuwakataliwa mawakilishi kuonana na wateja wao lakini tukaandika barua na kuomba wakati haki hii huwa haiombwi”
alisema.
Alisema serikali inatakiwa kuhakikisha watuhumiwa waweze kupewa haki zao za msingi akitoa mfano huo wa kuwasiliana na watu wao pamoja na kufanya ibada kwani hivi sasa wananyimwa haki za kufanya ibada na wenzao kwa kusali sala ya jamaa wakati baadhi ya watuhumiw awenzao wanapewa haki hiyo ya kusali pamoja wakati wao wamewekwa kila mmoja na chumba chake na hawaruhusiwi kutoka wala kuwasiliana.
“Tunajua kuwa hao ni waislamu na ni viongozi wa dini ni masheikh kuwanyima fursa ya kusali haipendezi na kuwavunjia haki yao ya ibada kuwanyima misahafu ya kusoma quraan ni kosa pia wakati tunajua wenyewe wanataka kusoma quraan, watuhumiwa wenzao wanakwenda kusali pale pamoja sala ya jamaa lakini wao wanawazuwia” aliongeza.
Alisema kibaya zaidi ni kule kuwalazwa chini sakafuni jambo ambalo amesema ni kuwavunjia haki zao za msingi kwani angalau wangewekewa magorodo kama wenzao au kupewa mabrangeti lakini wanalazwa chini huku wakitafunwa na mbui na hawapewi kitu chochotecha kujifunika.
Alisema watuhumiwa hao pia wamekataliwa kuonana na jamaa zao na yeye ndio mtu wa kwanza kuonana na wateja wake tokea siku walipopelekwa rumande na kwamba wanakoseshwa haki ya kusoma chochote ikiwa pamoja na kukoseshwa kusoma quran tukufu na kusali jamaa wakati wenzeiwao wote wanaruhusiwa kusali jamaa.
“Hapewi ruhusa ya kusoma kitu chochote wamesema waliomba misahafu lakini wamekataliwa na hivyo hivyo hata magazeti wanataka lakini wamekataliwa kupewa na kwa hivyo hata kutoka nje hawaruhusiwi kutoka nje wanakaa saa 24 ndani mfululizo wakati wale mahabusu wenzao ambao wanapewa ruhusa kutoka angalau pale nje” alisema Wakili huyo.
Wakili huyo alisema wateja wake wote wanane kila mmoja amewekwa katika chumba chake peke yake na pia hawaruhusiwi kuwasiliana kwa hali yoyote ile ndani ya gereza hilo, na wamekuwa wakilazwa chini bila ya godoro wala bramketi wakati wenziwao wanapewa brangeti wao wanalazwa sakafuni.
“Sisi mawakili wao tulikataliwa kuwaona na tokea kuwekwa ndani hawajaruhusiwa kuonana na mtu yeyote lakini jambo la kusikitisha wiki ya pili sasa nguo zile zile hawajaruhusiwa kuletewa nguo kutoka nje kwa hivyo hiyo sio haki kwa mwanaadamu” alisema Wakili.
Juhudi za kumpata kamishna wa magereza kuzungumzia madai ya mawakili wa watuhumiwa hazijaweza kuzaa matunda baada ya kukosekana kupatikana.
Watuhumiwa hao walikamatwa na kushitakiwa siku moja baada ya Sheikh Farid kuonekana baada ya siku nne za kutoweka kwa madai ya kutekwa na jeshi la polisi jambo ambalo lilizusha vurugu baada ya wafuasi wake kutoka barabarani na kuishinidkiza serikali kumtoa alipo.
Katika hatua nyengine watuhumiwa wote hao wanatarajiwa kupandishwa tena leo katika mahakama ya Mkoa Vuga wakikabiliwa na mashtaka ya uharibifu wa mali, kushawishi kuchochea na kurubuni watu kufanya fujo na kula njama za kujificha kwa Sheikh Farid huku Sheikh Azzan akisomewa shitaka la nne la peke yake la Uvunjifu wa amani.

No comments:

Post a Comment