Wapiganaji wa zamani huko magharibi
mwa Ivory Coast wamekabidhi silaha zao katika oparesheni ya kukusanya
silaha zisizokuwa na kibali nchini humo. Oparesheni ya kukusanya silaha
za aina hiyo ilianza katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika mwishoni
mwa mwezi Oktoba mwaka huu na inatazamiwa kumalizika tarehe 11 mwezi huu
wa Novemba.
Viongozi wa serikali wamesisitiza kuwa
wale wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wanaweza kukabidhi
silaha na zana za kijeshi walizonazo bila ya kuhofia kushtakiwa. Mtu
ambaye atakabidhi silaha zake kwa hiyari kwa serikali atapewa franga
3000 ambazo ni sawa na dola sita. Kitendo cha kuwalipa fedha wale wote
watakaokabidhi silaha zao ni hatua ambayo imechukuliwa na serikali ya
Kodivaa ili kuwashawishi wamiliki silaha kinyume cha sheria wakabidhi
silaha hizo.
Silaha nyingi na zana za kivita
zilitumbukia mikononi mwa raia wa Kodivaa wakati wa vita vya ndani
nchini humo kati ya mwaka 2010 hadi 2011. Kusalia silaha hizo mikononi
mwa raia na makundi ya wanamgambo ni moja ya sababu za kuweko ukosefu wa
amani na machafuko huko Ivory Coast. Mzozo wa kuwania madaraka kati ya
mahasimu wawili wa kisiasa huko Ivory Coast ulioibuka mwezi Novemba
miaka miwili iliyopita ulizusha mapigano kati ya wafuasi wa viongozi hao
na kusababisha mgogoro mkubwa kote nchini humo. Hatua ya Laurent
Gbagbo, Rais wa zamani wa nchi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi
ilikuwa chanzo kikuu cha kuzuka mgogoro na machafuko ya umwagaji damu
baada ya uchaguzi wa rais. Alassane Ouattara Waziri Mkuu wa zamani wa
nchi hiyo ambaye alishinda katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais mwezi
Novemba mwaka 2010 alitambuliwa na Jumuya ya kieneo ya Ecowas na Umoja
wa Afrika kuwa ndiye mshindi katika uchaguzi huo. Nchi mbalimbali na
taasisi za kimataifa kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia
zilimuunga mkono Ouattara baada ya kuthibitishwa kuwa mshindi na wakuu
wa nchi za Magharibi mwa Afrika katika Jumuiya ya Ecowas.
Pamoja na hayo, Laurent Gbagbo ambaye
alikuwa akiungwa mkono na baadhi ya vikosi vya jeshi alipinga matokeo
hayo ya uchaguzi na kwa mara nyingine tena Ivory Coast ikatumbukia
katika mgogoro. Vilevile kuliripotiwa pia ukiukaji mkubwa wa haki za
binadamu na kuuliwa raia wengi katika kipindi cha mwezi Novemba mwaka
2012 hadi Aprili 11 mwaka jana.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa
wanaamini kuwa mauaji ya hivi karibuni na mashambulizi yaliyofanywa
katika vituo vya jeshi la Ivory Coast yametekelezwa na wafuasi wa rais
wa zamani wa nchi hiyo Laurent Gbagbo. Japokuwa baadhi ya ripoti za
watetezi wa haki za binadamu zimewatuhumu pia wafuasi wa Alassane
Ouattara kuwa walikiuka haki za binadamu wakati wa vita vya ndani nchini
humo.
Kwa vyovyote vile zoezi la kukusanya
silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria na wapiganaji wa zamani
linahesabiwa kuwa hatua ya awali katika njia ndefu ya kurejesha utulivu
na amani huko Ivory Coast.
No comments:
Post a Comment