Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Saturday, November 3, 2012

KARIAKOO HOFU TUPU


Hivi ndivyo hali ilivyokuwa kwenye mtaa wa Kariakoo jijini Dar es Salaam ambapo askari na watu wachache wanaonekana jirani na jengo la DDC-Kariakoo, (Kushoto), baada ya hofu ya kuwepo kwa maandamano baada ya sala ya Ijumaa jana Novemba 2, 2012. Shughuli za kibiashara zilitatizika kwa muda wa masaa matatu baada ya sala ya Ijumaa, ambapo kikundi cha watu wachache wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa Sheikh Ponda Issa Ponda, kilionekana kikiwa nje ya msikiti wa Idrisa baada ya sala hiyo. Hata hivyo polisi baada ya kuwaeleza mara kadhaa kutawanyika na kutofanya hivyo, ilirusha mabomu ya machozi na kupiga risasi hewani ili kuwatawanya hali iliyozusha hofu kuu miongoni mwa wapita njia na wafanyabiashara na kupelekea kufunga maduka yao kwa muda. Sheikh Ponda na wenzake 49 wanakabilkiwa na kesi ya kuvamia eneo la Markaz, Chang'ombe jijini ambapo pamoja na mambo mengine, wanatuhumiwa kuvunja na kuiba pamoja na kujimilikisha ardhi kinyume cha sheria. Washtakiwa wote walikubaliwa dhamana juzi Alhamisi Novemba 1, 2012 isipokuwa sheikh Ponda ambaye bado Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hajaondoa pingamizi lake la kuzuia dhamana. Kwa waliopewa dhamana, masharti ni kuwa na wadhamini wawili na kuweka bondi ahadi ya shilingi milioni moja kila mmoja, pamoja na barua ya kuonyesha anuani maalum ya makazi. Sharti lingine kwa mujibu wa hakimu ......................ni washtakiwa kutokanyaga eneo la Markaz hadi hapo kesi yao itakapokamilika. Bado haijajulikana kama washtakiwa wote wametimiza masharti ya dhamana.

Mmoja wa watu wanaoaminika kuwa ni mfuasi wa Sheikh Ponda, akiwa mikononi mwa askari kanzu jirani na msikiti wa Idrisa, Kariakoo jijini Dar es Salaam, Ijumaa Novemba 2, 2012

Kijana anayetuhumiwa kuwa ni kibaka, akishushwa kwenye karandinga la polisi baada ya jaribio lake la kumkwapua mama huyu, (Kushoto), kugunduliwa na polisi eneo la Kariakoo

Mchuuzi huyu akikimbia na bidhaa zake kutafuta mahala salama baada ya polisi kurusha mabomu ya machozi na kupiga risasi hewani kuwatawanya wafuasi wachache wa sheikh Ponda Issa Ponda, waliokuwa wamejichimbia msikiti wa Idrisa baada ya sala ya Ijumaa Novemba 2, 2012

Machinga wakiwa na mabegi yao wakipita pembeni mwa maduka kadhaa yaliyofungwa mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Novemba 2, 2012, kufuatia hali ya wasiwasi ya kuwepo kwa maandamano ya wafuasi wa Sheikh Ponda Issa Ponda

No comments:

Post a Comment