Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Tuesday, November 20, 2012

Ujumbe wa Arab League wawasili Gaza



Ujumbe wa Arab League wawasili GazaUjumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ukiongozwa na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Nabiil al Arabi umewasili leo mjini Gaza kuonesha mshikamano na wananchi wa eneo hilo wanaoendelea kushambuliwa na jeshi la Israel.
Baada ya kuwasili Gaza al Arabi amesema nchi za Kiarabu zinapaswa kuwasaidia na kuwaunga mkono wananchi wa Palestina mbele ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesisitiza pia juu ya udharura wa kusitishwa mashambulizi hayo haraka iwezekanavyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Muhammad Kamil Amru ambaye pia yuko kwenye ujumbe huo amesema mashambulizi ya Israel yanayowalenga raia wa Gaza yanapaswa kusitishwa mara moja.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan anayeandamana na ujumbe huo wa Arab League Ali Karti amelaani jinai za Israel huko Gaza na kusisitiza kuwa mashambulizi hayo ya kidhalimu yameukasirisha ulimwengu mzima wa Kiarabu na Kiislamu.
Ujumbe huo wa nchi za Kiarabu unaojumuisha zaidi ya mawaziri kumi wa mambo ya nje umewasili Gaza huku ndege za kivita za Israel zikiendelea kushambulia vikali baadhi ya maeneo ya mji huo. Kanali ya televisheni ya al Manar ya Lebanon imeripoti kuwa Wapalestina 6 wameuawa shahidi leo sambamba na safari ya mawaziri hao katika Ukanda wa Gaza.

No comments:

Post a Comment