Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad
ameelezea kuchukizwa kwake na vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani
vilivyotokea hivi karibuni visiwani Zanzibar.
Amesema vitendo hivyo vimeigharimu Zanzibar katika Nyanja mbali
mbali zikiwemo za kiuchumi, kisiasa na kijamii, sambamba na kuitia doa
katika jamii ya kimataifa.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya
demokrasia Kibandamaiti mjini Zanzibar, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amevilaumu vyombo vya dola kwa
kutochukuwa hatua zinazostahiki katika kudhibiti vitendo hivyo.
Amesema hatua zilizochukuliwa katika kurejesha amani baada ya
kutokea kwa vurugu hizo hazikuwa muafaka, kwani zimekuwa
zikiwadhalilisha na kuwanyanyasa wananchi wasiokuwa na hatia pamoja na
kuhujumu mali zao.
Amesema yeye binafsi amechukizwa na kitendo cha kuuliwa kwa askari
polisi katika eneo la Bububu, Koplo Said Abrahmani lakini bado serikali
na vyombo vya dola vina jukumu la kulinda haki za raia kwa kuwasaka
wanaohusika na tukio hilo, na sio kuwanyanyasa raia wasiokuwa na hatia.
“Nazungumza haya kwa unyonge sana leo, sikufikiria kuwa vitendo
hivi vingetokea Zanzibar katika wakati huu tunaotekeleza maridhiano
ndani ya serikali ya umoja wa kitaifa”,alieleza Maalim Seif na kuongeza,
“Sipendi kuisema serikali yangu na Rais wangu hadharani, lakini
inanibidi niseme ‘Rais wangu Dkt Shein unatuangusha’ kwa kuwa wewe ndiye
mwenye jukumu kubwa zaidi la kulinda amani ya nchi hii” alieleza.
Ametahadharisha kuwa huenda vitendo hivyo vimepangwa kuvuruga umoja
wa Wazanzibari ambao umeiletea sifa kubwa Zanzibar, na kuwataka
wananchi kutokubali kuingizwa katika mtego utakaopelekea kuvunjika kwa
umoja na mshikamano uliopo miongoni mwa wananchi.
Katibu Mkuu huyo wa CUF alienda mbali zaidi kwa kudai kuwa vikundi
vinavyolalamikiwa kufanya vurugu vikiwemo vya ‘Ubaya ubaya, Mbwa mwitu
na Janjawid vilikuwepo kabla ya tukio hilo na kwamba vimetokana na kundi
kubwa la vijana la JANJAWID lililoahidiwa kupewa ajira na Serikali.
Katika hatua nyengine Maalim Seif ameitaka Tume ya mabadiliko ya
katiba kufanya kazi kwa uadilifu na kuheshimu mawazo ya wananchi
wanayoyatoa bila ya kuonyesha upendeleo kwa baadhi ya watu au makundi
fulani.
“Tume hii inaonekana kuanza kuwa na ‘bias’ kwa baadhi ya watu na
makundi fulani, lakini tunamwambia Jaji Warioba tume yake iheshimu
mawazo ya wananchi”, alitanabahisha.
Katika risala ya wanachama wa chama hicho kwa wilaya sita za Unguja
iliyosomwa na Katibu Mtendaji wa vijana CUF taifa Khalifa Abdallah
walitahadharisha juu ya uwezekano wa kuwepo kwa ajenda ya siri ya
kuvuruga Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa bado inahitajika
katika kupata ukombozi wa kweli wa Zanzibar, sambamba na kuendeleza
umoja na mshikamano wa Wazanzibari.
Nae Kaimu wa Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bw. Salim Bimani
amewasisitiza wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao
juu ya mabadiliko ya katiba, na kuiomba Tume inayohusika na ukusanyaji
wa maoni kuwapa fursa wananchi kutoa maoni yao kwa uwazi.
“Wananchi msikubali kuchokozeka, nendeni mkatoe maoni kwani hii ni fursa pekee ya kupata katiba tuitakayo” alisisitiza Bimani.
No comments:
Post a Comment