Benki ya Dunia imesema kuwa uchumi wa
Tanzania unaelekea kuimarika, lakini imeitaka serikali kuhakikisha
kwamba utajiri wa nchi unawanufaisha wananchi wake ambao wengi ni
masikini. Taarifa ya benki hiyo iliyotolewa hapo jana imesema, iwapo
bajeti itapangwa vyema nchini humo uzalishaji wa ndani utaongezeka kwa
asilimia 6.5 hadi 7 mwaka huu, mwaka ujao na mwaka 2014, kwa kusaidiwa
na uzalishaji katika sekta za madini, mawasiliano na benki. Benki ya
Dunia imesema, Tanzania inaweza kufikia malengo yake iwapo itajiepusha
na migogoro mikubwa ya kiuchumi na kuweka uwiano katika kukopa kwa ajili
ya miradi ya miundombinu na kulipa madeni.
Aidha Benki ya Dunia imesema Tanzania
ambayo ni nchi ya pili yenye uchumi unaoimarika zaidi Afrika Mashariki
itaweza kupiga hatua za maendeleo kwa kasi katika miaka 7 hadi 10 ijayo
kutokana na faida zitakazopatikana katika sekta ya gesi asilia. Hata
hivyo Benki ya Dunia imetahadharisha kwamba umasikini mkubwa
unaowakabili wananchi wengi wa Tanzania bado ni tatizo kubwa kwa nchi
hiyo.
No comments:
Post a Comment