Japan imeahidi kutoa msaada wa dola
bilioni 32 kuzisaidia sekta za umma na za binafsi katika nchi za bara la
Afrika ili kusaidia ustawi na maendeleo na kuyashajiisha mashirika na
makampuni ya Kijapani kuwekeza barani humo katika kipindi cha miaka
mitano ijayo. Ahadi hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo
Abe, katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo wa Maendeleo ya
Afrika (TICAD) na inajumuisha msaada rasmi wa maendeleo wa dola bilioni
14 na dola bilioni 6.5 za kusaidia sekta ya miundombinu. Kwa mujibu wa
takwimu rasmi kiwango cha uwekezaji wa moja kwa moja wa Japan barani
Afrika katika mwaka 2011 kilikuwa dola milioni 460 kikiwa ni cha chini
mno kulinganisha na uwekezaji wa dola bilioni 3.17 uliofanywa na China
katika nchi za bara hilo. Tangu achaguliwe kuwa Waziri Mkuu wa Japan
mwezi Disemba mwaka uliopita, Shinzo Abe amechukua hatua kubwa katika
uga wa diplomasia na amesisitiza kwamba anapanga kufanya safari katika
nchi za Kiafrika mapema iwezekanavyo. Inafaa kuashiria kuwa viongozi
wapatao 50 wa nchi za bara la Afrika wanashiriki katika mkutano wa siku
tatu wa TICAD unaofanyika huko Yokohama karibu na mji mkuu wa Japan,
Tokyo unaojadili masuala kadhaa yakiwemo ya maendeleo ya uchumi, kuleta
amani na kupambana na uharamia…/
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment