SIKU chache baada ya kutokea kifo cha Padri Evarist Gabriel Mushi na
watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi kichwani eneo la Beit el Raas,
Jana Imamu wa Msikiti wa Mwakaje amefariki dunia baada ya kupigwa
mapanga hadi kufa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja,
Ahmada Khamis amethibitisha kutokea kwa tukio hilo hapo jana mchana
majira ya saa 8 mchana na kumtaja aliyefariki ni Sheikh Ali Khamis
ambaye ameuawa na watu wasiojulikana.
Kamanda Ahmada alisema Sheikh Khamis mbali ya kuwa ni Imamu wa
Msikiti lakini pia ni mkulima na ameuliwa wakati akiwa katika mazingira
ya kazi zake ndani ya shamba lake huko Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akielezea mazingira ya tukio hilo Kamanda Ahmada alisema tukio hilo
limetokea baada ya Sheikh Khamis kwenda shambani kwake katika shmba la
minazi Kidoti ambapo wakati akiwa shambani hapo ndipo walipotokea watu
kadhaa na kumpiga mapanga sehemu za shingoni mwake na kusababisha kifo
chake muda mfupi baada ya kipigo hicho.
Alisema baada ya tukio hilo, watu walimchukua na kumkimbizwa
hospitali lakini kutokana na kupoteza damu nyingi alifariki dunia wakati
akiwa njiani na hivyo harakati za mazishi zinafanyika za kumzika baada
ya kuchukuliwa vipimo vya wataalamu wa afya.
Kamanda Ahmada ametoa wito kwa wananchi kutopuuzia taarifa za watu
ambao wanawashuku na wenye kuleta maafa yakiwemo mauaji hapa nchini,
kwani kuwaficha wahalifu ni kuendeleza utamaduni usiofaa katika jamii
ambayo imeanza kuharibika kutokana na mauaji hayo yanayoendelea kila
kukicha. Inna lillahi wainna ilayhi rajiiun.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment