Watu wasiopungua 35 wameuawa katika
shambulio lililofanywa mapema leo na kundi la wanamgambo kwenye kituo
kimoja cha upekuzi cha jeshi huko Lakki Marwat kaskazini magharibi mwa
Pakistan. Kundi la Taliban ya Pakistan limetangaza kuhusika na shambulio
hilo lililoandamana na ufyatulianaji risasi na uvurumishaji makombora
kwenye nyumba moja. Kundi hilo limedai kuwa shambulio hilo ni jibu kwa
shambulio la mwezi uliopita lililofanywa na ndege isiyo na rubani ya
Marekani huko Waziristan Kaskazini na kupelekea kuuawa makamanda wawili
wa kundi hilo. Msemaji wa Taliban amesema serikali ya Pakistan imekuwa
ikishirikiana na Marekani katika mashambulio yake ya ndege zisizo na
rubani ndani ya ardhi ya Pakistan na kwamba shambulio hilo ni la
kulipiza kisasi kwa mauaji ya Faisal Khan na Toofani,
makamanda hao
wawili wa kundi hilo. Afisa usalama wa Pakistan amesema wanamgambo 12
na askari 13 waliuawa katika mapigano hayo yaliyoendelea kwa muda wa
masaa manne huku viwiliwili viwili vya waliouawa vikiwa na mikanda ya
mabomu ya kujitolea mhanga. Afisa huyo wa serikali ya Islamabad
ameongeza kuwa wanamgambo wa Taliban pia waliilenga kwa makombora nyumba
moja na kuua watu 10 wa familia moja wakiwemo watoto watatu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment