Mapigano makali yanaripotiwa
kuendelea kati ya wanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini na waasi
wanaoongozwa na makamu wa zamani wa rais Riek Machar.
Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Philip
Aguer amesema siku ya Jumatano walipambana vikali na waasi katika
kupigania udhibiti wa Bor, mji mkuu wa Jimbo la Jonglei. Aidha mapigano
yanaripotiwa kuendelea katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Nile ya
Juu. Msemaji wa waasi Youhani Musa Pauk amesema hakutakuwa na usitishaji
mapigano hadi pale serikali ya Juba itakapowaachilia huru wanasiasa
wapinzani ambao walitiwa mbaroni punde baada ya machafuko kuibuka wiki
tatu zilizopita. Huku hayo yakijiri wapatanishi kutoka jumuiya ya kieneo
ya IGAD wanasema mazungumzo baina ya pande hasimu yanaendelea vizuri na
kwamba Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesitiza kuwa mgogoro wa sasa
ni wa kisiasa na kwamba anaunga mkono suluhisho la kisiasa. Machafuko
nchini Sudan Kusini yalianza Disemba 15 katika mji mkuu Juba, pale
wanajeshi wanaoaminika kuwa watiifu kwa Riek Machar, walipojaribu
kuipindua serikali ya Rais Salva Kiir. Uhasama wa kisiasa nchini humo
ulianza mwezi Julai mwaka jana baada ya Kiir kumfuta kazi Machar. Kiir
ni kutoka kabila la Dinka ambalo ndilo lenye nguvu zaidi na Machar ni wa
kabila la Nuer.
No comments:
Post a Comment