Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Friday, June 8, 2012

Muungano wa Speed and Standard

Sasa kumepambazuka,mapabazuko mapya yanatarajiwa kutokeza katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sio jambo jengine ni lile linalozungumzwa kila siku la wananchi kutaka kuwepo kwa Muungano wenye kumaliza malalamiko ya miaka mingi. Watu hawataki kusema kweli, sijui wanaogopa kitu gani,lakini hakuna anayeweza kusimama mbele ya umma akisema kwamba wanaodai kuwepo kwa mabadiliko katika muundo wa Muungano ni watu wachache,ikiwa anaamini hivyo, anatakuwa anajidanganya nafsi yake.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Wilson Churchill aliweza kubashiri mabadiliko katika mataifa ya Afrika ambayo yalikuwa yakitawaliwa na wakoloni, waingereza wenzake hawakuamini kama ambavyo aliyekuwa Gavana kule Rhodesia ya Kusini (sasa Zimbabwe) Ian Smith.
Wakati ndio unaofanya watu kuwasukuma kwenye maamuzi, sio jambo jengine kwani mwaka 1970 au miaka ya mwishoni mwa 1980s mijadala ya Muungano haikuwa na nguvu kama hivi leo.
Vyama vingi vilirejeshwa tena katika mataifa mengi baada ya Uhuru mwaka 1992, wapo watu wakati ule waliapa katu hatutaweza kubadili mfumo wetu tuliouzoea tangu mwaka 1961 na 1964.
Miongoni mwa wazee wanaostahiki kupongeza ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyekubaliana na wanamageuzi kuhusu vyama vingi, asilimia 80 walikataa kubadili mfumo,lakini Chama cha CCM chini ya Uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi ikapima na ikaamua kukubaliana na asilimia 20 ya Watanzania waliotaka mfumo ubadilike na kuwa wa vyama vingi.
Baadhi ya waliopinga vyama vingi mwaka 1992 ndio leo wapo viongozi katika vyama hivyo na wengine Wabunge na wenye nyadhifa kubwa kubwa ndani ya vyama vyao,lakini walikula viapo vya kinafiki kupinga na kuwabeza wanaotaka mabadiliko wanamageuzi ya kweli.
Siku zote wanamageuzi ya kweli hawayumbi, wanakuwa wanaamini na wako tayari kutetea msimamo wao, sio kama popo ambaye anaweza kwenda kwenye vikao vya ndege na pia vikao vya wanyama anaweza kushiriki, wanasiasa wa aina hii hawanaweza kupata mafanikio katika medani za siasa kama alizopata Mzee Nelson Mandela wa Afrika Kusini.
Kuwepo kwa vuguvugu la kutaka mabadiliko hasa Zanzibar ni matokeo ya muda mrefu ya kuchelewa kushughulikia kero za Muungano ambazo zimeundiwa kamati hizi na zile,lakini kasi yake haikuwa kama ile ya Mzee wa Speed and Standard katika Bunge lililopita chini ya Samuel Sitta.
Muungano unahitajika na kila mtu na ukisikiliza hoja za wanaotaka mabadiliko hawakupeleki katika hatua ya kuvunja, wanachotaka ni kuwepo kwa Muungano wenye kukidhi mahitaji ya leo,kesho na miaka hamsini baadaye ambao kizazi cha wakati huo baada yetu nacho kinaweza ama kuufanyia marekebisho au wakaamua kuendelea na mfumo uliopo baada ya kujiridhisha na mahitaji yao ya wakati huo.
Ule usemi wa Mji wa Roma haukujengwa siki moja, unaweza kufaa sana kwa mazingira ya Muungano wetu, ambao hatutaujenga kwa siku moja chini ya katiba mpya, unaweza kufanyiwa marekebisho kila panapohitajika maana Muungano huu haukuumbwa na Mwenyezi Mungu,umebuniwa na binadamu na bila shaka kutakuwa na upungufu wa hapa na pale.
Kwa mfano, kwanini wafanyakazi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliopo Zanzibar makato yao yatokanayo na kodi yasibaki Zanzibar na badala yake yanaingia katika mfuko mkuu wa hazina ya Tanzania!
Kwanini gesi asilia ni jambo la Muungano mbona Zanzibar hainufaiki na mapato yanatokanayo na rasilimali hiyo? Ndio maana SMZ ikaamua kuyaondoa mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya Muungano kupitia uamuzi wa wananchi katika Baraza la Wawakilishi.
Ukiacha kero hiyo, kuna nile ya watumishi wa Zanzíbar katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukianzia Mabalozi, Mafias Kibalozi na sehemu nyengine katika utumishi wa SMT bado ni tatizo, hakuna usawa katika zile Wiraza za Muungano.
Zanzíbar kwa maumbile yake kijiografia kama nchi ya kisiwa inamahitaji maalum ya kuzingatiwa kama ilivyo kwa nchi zinazofafana nazo ambazo sio kwamba zinalindwa Kimataifa,lakini inatizamwa kwa jicho la huruma na hasa suala zima la mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la watu.
Dunia ya leo ni ya majadiliano, sio ya ubabe kwani matokeo ya ubabe au kudharau mambo ndio yaliyowakuta katika mataifa mengine ambayo badala ya kuziba ufa yamejenga ukuta, Tanzania ni nchi ya kideokrasia na bila shaka itakuwa tulivu kusikiliza raia wake wanataka nini na kwa namna ipi.
Kisa kimoja kilitokea kule Malaysia kwa watu wawili ambao ni majirani kwa miaka mingi wakiishi mtaa mmoja na nyumba zao kukaribiana sana kama zile za mitaa ya kwetu.
Mzozo wa tofauti yao ulidumu kwa muda wa miaka mitatu waliamua kukubaliana kumaliza tofauti zao kwa kutia sahihi makubaliano ya ushirikiano wa ujirani mwema maana wahenga wanasema hálahala jirani.
Kutokuelewana kwa majirani hao kumeripotiwa na Shirila la habari la uingereza, Reuters ambalo limesema kwamba majirani hao wanaoishi katika jimbo la kusini la Johor Malaysia umedumu kwa miaka mitatu, na hata polisi walishindwa kuusuluhisha.
Gazeti moja la Star limeelezea sakata la ugomvi huo ni mbwa waliokuwa wakipiga kelele, na jirani mwingine kujibu mashambulizi kwa kufungua muziki kwa sauti ya juu katika radio yake.
Hata hivyo baada ya miaka mitatu ya mzozo uliokuwa ni pamoja na kurushiana taka na hata kugonga mageti kwa kutumia magari yao, majirani hao waliamua kutia saini makubaliano ya maelewano kumaliza kero zilizokuwa zikiwakorofisha.
Kwa hivyo katika dunia hii lazima kutakuwa na tofauti ama ya fikra, hulka na mahitaji, ndio maana wengi wanazungumzia sasa kuwepo kwa mfumo wa muundo wa Muungano unaofafana na ule wa Muungano wa nchi za Ulaya.
Ukizungumza na vijana, watu wa rika la kati na hata wazee wanaelezea msingi dhaifu uliojengwa wakati ukiasisiwa mwaka 1964, na kwa hali ya mambo inavyokwenda muundo wa Muungano unahitaji kutamwa na watazamaji wanapendekeza bila kuzunguka kwamba Muungano uwe imara ni kubadili muundo wake.
Wengine wanaweza kusema hata ukibadili kero zinakuwepo,mimi sitaki kuamini hivyo kwani sijapata kusikia Muungano wa Ulaya una kero hata kama zikiwepo basi ni zile ndogo ndogo sio kama hizi za hapa kwetu ambazo karibú Marais wote walioongoza Tanzania wamemaliza vipindi vyao vya uongozi na kuziacha hazijatatuka.
Ni lazima tukabili na tuende na wakati maana wakati ni ukuta, ukitupita hautakuja tena, tukijenga muundo madhubuti tutakuwa tumeijenga vema nyumba yetu hatutavujiwa na mvua za masika wala vuli.
Wapo wenye kufikiri na kubaki na msimamo kwamba Muungano utabaki wenye mfumo wa Serikali mbili kuelekea moja hatuwalaumu,lakini mbona wameachwa nyuma sana maana kasi ya sasa ni sawa ile iliyokuwa imeasisiwa na aliyekuwa Spika, Samuel Sitta, katika Bunge la “Speed and Standard” Muungano nao ni wa kasi na viwango,viwango vya Serikali moja havipo.
Waswahili wa pwani wanamsemo wao lipitalo ,hupishwa,pengine ningewashauri wale wenye ndoto ya kuwa na Serikali moja wakapisha majadala uendelee wa kuwa na mfumo wa Muungano wenye kutakiwa na wananchi.
Kwa kuwa mamlaka ya uendeshaji nchi ni ya wananchi wenyewe hatutegemei kutokea mtu akaanza kubeza mtazamo wa wananchi wenzake maana cheo ni dhana tu na tunatakiwa kutokitumia vibaya cheo kwa maana hiyo viongozi wakiwa na mawazo na misimamo yao inawapasa kupima kwa kipimo sahihi jamii inatakaje.
Sisi wengine tunaweka bayana mawazo yetu,wengine ndio wale wenye kusubiri fwataa kuingia jahazi la Nabii Nuhu wahenga wanatwambia heri karipio la rafiki, kuliko busu la mnafiki.
Katika mchakato wa katiba watazuka watu wenye kuyumba kimsimamo na kimantiki, ingawa hawatapata uungwaji mkono,lakini wataweza wenyewe kujionea hali itakavyokuwa wakati Tume ya Katiba itakapoanza kukusanya maoni kutoka kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment