Tutakuwa
pamoja nanyi tukizungumzia moyo wenye huruma, moyo wenye ulaini, moyo
ulio umbiwa huruma. Tutakuwa tukizungumzia moyo ambao umeumbwa siku
ulipoumbwa, ukapandikizwa huruma, tutakuwa na moyo wenye kuhurumia hata
kama unafanyiwa ukali. Je, mmeufahamu moyo huo? Hakika si mwingine bali
moyo huo ni mama.
Tunamzungumzia
mama ambaye maadui wa Allaah wamemuwekea siku moja tu na wakaiita "siku
ya mama" na hili si katika Uislamu kwa chochote. Uislamu umeamrisha
kumfanyia wema mama (kila siku) mwaka mzima.
Huyo ndiye mama enyi waja wa Allaah. Kiumbe ambaye ameendelea kuwa mbele na mshindi daima.
Mama
yako enyi waja wa Allaah, ni mara ngapi amehuzunika (ameingia katika
jambo la kumhuzunisha) ili wewe ufurahi, na akashinda au kulala njaa ili
ushibe, na akalia ili ucheke, na akakesha ili ulale, na akabeba mambo
magumu na mazito katika njia ya furaha yako (ili ufurahi). Unapokuwa
umefurahi naye ndipo hufurahi, na ukihuzunika, umemhuzunisha, ukipatiwa
na mfadhaiko, basi maisha yake yako katika shida kubwa. Matumaini na
matarajio yake, yako katika shida kubwa. Matumaini na matarajio yake
(yote) ni wewe uishi maisha ya kiungwana (matukufu) ya kuridhisha yenye
kuridhiwa.
Mama
kiumbe dhaifu ambaye hutoa bila kutaraji malipo yoyote. Anayemimina
(kheri zake zote kwako) bila kutumai shukrani zozote kwako. Je umewahi
kumsikia kiumbe anayekupenda kuliko mali yake? Hapana, bali zaidi kuliko
dunia yake? Hapana bali zaidi kuliko nafsi yake iliyopo kati ya mbavu
zake? Ndio, anayekupenda zaidi kuliko nafsi yake, hakika huyo si
mwengine bali ni mama yako, mama pekee ndio alama ya huruma.
Hebu
fikiria kwa makini ewe ndugu yangu mpendwa, hali uliyokuwa nayo udogoni
mwako (fikiria) kumbuka udhaifu wa uchanga wako, hakika alikubebea
mimba tumboni mwake miezi tisa kwa hali ya unyonge (udhaifu) juu ya
unyonge. Amekubebea mimba kwa taabu na akakuzaa kwa taabu, kuendelea
kukua kwako tumboni mwake kulimzidishia udhaifu na anabeba mzigo (taabu)
zilizo nje ya uwezo wake, na mama (kama alivyo mwanamke mwengine) ni
mdhaifu wa kiwiliwili, mnyonge wa nguvu, na wakati wa kujifungua huyaona
mauti mbele ya macho yake, machozi na masikitiko, vikwazo na machungu,
lakini yeye anajilazimisha kusubiri (mpaka anakuzaa) na pale tu
anapokuona u-pembeni mwake na akakukumbatia kifuani mwake, na akashumu
(akanusa) harufu yako, na akazihisi pumzi zako zikikariri (kuingia na
kutoka), basi husahau maumivu yake yote, na husahau machungu yake yote.
Anakuona
na kufungamanisha matumaini yake yote kwako. Na huona kwako uzuri wa
maisha na mapambo yake, kisha anageukia kukuhudumia mchana wa maisha
yako na usiku wake. Akikulisha kwa ajili ya siha yako, na akikukuza kwa
kujichakaza (kujizeesha) yeye, na kukuimarisha (kukutia nguvu) kwa
kujidhoofisha yeye, chakula chako ni chuchu zake, nyumba yako ni mapaja
yake, na gari lako ni mikono yake (au mgongo wake). Amezunguka na
kukuchunga (usipatwe na balaa lolote). Yuko radhi yeye abaki na njaa ili
wewe ushibe, na akeshe ili ulale, na yeye kwako ni mwenye huruma
nyingi. Na ana uchungu mwingi juu yako, akikaa mbali nawe (kidogo tu)
unamuita, na akikupa nyongo unamuomba akuelekee. Na likikupata la
kukuchukiza unaomba wokozi kwake. Unadhani kheri zote (kila jambo zuri)
ziko kwake tu. Na unadhani shari haitokufikia akikukumbatia kifuani
mwake, au akiwa anakuangalia kwa jicho la mazingatio.
Na
baada ya kutimia kuacha kwako ziwa ndani ya miaka miwili (mara nyingi),
na ukaanza kutembea huanza kuuzungusha umuhimu wake wote kwako, na
macho yake hukufuatilia (popote uendapo). Hukufuatilia haraka nyuma yako
kwa kukuhofia (kuanguka na mengineyo) kisha ukakua, na kuchukua kwako
miaka. Ikampata na kumuingia shauku na huruma, sura yako ni nzuri zaidi
mbele yake kuliko mwezi unapokamilika (duara lake), sauti yako kwake ni
tamu zaidi masikioni mwake kuliko sauti za bulbul na nyimbo za ndege
wengine. Harufu yako inanukia vizuri zaidi kwake kuliko manukato yote na
maua yote, utukufu wako ni kitu cha ghali sana kuliko dunia, lau
itapelekwa kwake pamoja na mapambo yake yote hakuna kitu ghali, bali
kila kitu ni rahisi kwake katika kuhakikisha unapata raha. Mpaka hata
nafsi yake iliyopo kati ya mbavu zake mbili si lolote si chochote, na
huchagua kufa ili wewe uishi salama salimini mwenye afya tele!!
Ni Mama Yako Ewe Mja Wa Allaah
Hebu
sikiliza kwa makini ewe mja wa Allaah, na ujue ya kwamba aliyenyimwa
kheri, aliyepotea na kuruka patupu (kula hasara) duniani na Akhera, ni
yule atakayepoteza haki za wazazi wawili na hasa hasa mama.
Amepokea Hadiyth Imaam Ahmad na An-Nasaaiy na Ibn Maajah, kutoka kwa
Mu'awiyah Ibn Jahimah As-Salamiy (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema.
Nilimuendea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (siku
moja) na nikamwambia; Ewe Mtume wa Allaah, hakika mimi nahitaji kupigana
jihadi pamoja nawe, nikitaraji kupata radhi za Allaah na nyumba ya
akhera, Mtume akasema: ((Nakuonea huruma (Usifanye Hivyo), hivi yuko hai
mama yako?)) Nikasema: Ndiyo. Mtume akasema: ((Rudi ukamfanyie wema
usiende kupigana Jihadi)). Kisha nikamuendea kupitia upande mwingine,
nikamuambia: Ewe Mtume wa Allaah, hakika mimi nataka kupigana Jihadi
pamoja nawe, nikitafuta kwa hilo radhi za Allaah na nyumba ya akhera,
Mtume akasema ((Nakuhurumia, usifanye hivyo, je mama yako yu hai?)).
Nikasema ndiyo ewe Mtume wa Allaah. Mtume akasema: ((Rudi kwake ukafanye
wema)). Kisha nikamuendea kwa mbele yake nikasema: Ewe Mtume wa Allaah,
hakika mimi nataka kupigana jihadi pamoja nawe, nikitafuta kwa hilo
radhi za Allaah na nyumba ya akhera, Mtume akasema: ((Nakuonea huruma,
usifanye hivyo, Mtume akasema: ((Nakuonea huruma, jilazimishe na mguu
wake hapo ndipo palipo na pepo)), Hakika mama ni pepo namuapa Mola wa
al-Kaabah, Lazimiana (shikamana) na mguu wake hapo ndipo ilipo pepo)).
Imepokewa Hadiyth (nyingine) kutoka kwa Ibn
'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtu mmoja alimjia Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na akasema: Ewe Mtume wa Allaah,
mimi nimekuja nataka kupigana jihadi pamoja nawe nikitaraji radhi za
Allaah na nyumba ya akhera, na kwa hakika nimekuja, huku wazazi wangu
wawili wanalia; Mtume akasema: ((Rudi kwao ukawachekeshe kama
ulivyowaliza)). [Ameisimulia Ibn Maajah na akaisahihisha Al-Albaaniy].
Na kutoka kwa Anas
bin Nadhwiri Al-Ashijainiy amesema: Siku moja mama yake Ibn Mas'uud
(Radhiya Allaahu 'anha) alitaka maji ya kunywa na ilikuwa usiku – kwa
mwanawe Ibn Mas'uud, akaenda kumletea maji, kurudi akamkuta keshalala,
Ibn Mas'uud akabaki amesimama na maji mbele ya kichwa chake mpaka
asubuhi, na walipofika Abu Muusa Al-Ash'ariy na Abu 'Aamir kwa Mtume wa
Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakampa Bay'ah
(kiapo cha utii) na wakasilimu. Mtume akawauliza (amefenya nini yule
mwanamke, miongoni mwenu aitwaye kadhaa wa kadhaa? Mtume akasema: (Kwa
sababu ya kumtendea mama yake akasema, alikuwa ana Mama bibi kizee, mara
akawajia muonyaji akisema, hakika adui anakusudia kuwadhuruni, Mama
huyu (Mama Ibn Mas'uud) akambeba mama yake mgongoni mwake, akichoka
anamtua chini (anapumzika) kasha anakutanisha tumbo lake na tumbo la
Mama yake (yaani anambeba kwa kumkumbatia tumboni) ikawa miguu yake iko
chini ya miguu ya Mama yake kutokana na kumkinga na joto kali, mpaka
akaokoka na adui yule). [Ameitoa 'Abdur-Razaaq katika Muswannaf yake].
Huyo ndiye Mama, ewe mwenye kutaka kuokoka, basi lazima ana miguu yake, hapo ndipo ilipo pepo yake.
Waja Wema Na Kuamiliana Kwao Na Mama
Siku
moja Ibn 'Umar alimuuliza mtu mmoja, je, unaogopa kuingia motoni? Na
unapenda kuingia peponi? Yule mtu akasema ndiyo. Ibn 'Umar akamwambia:
Basi mfanyie wema Mama yako, kwani namuapa Allaah, Kama utamlainishia
maneno na ukamlisha chakula, hakika utaingia peponi endapo utajiepusha
na madhambi makubwa yenye kuangamiza.
Hakika
kuwafanyia wema wazazi wawili ni tabia ya watu wema, na ni mwendo wa
wacha-Mungu. Inasimuliwa kuwa siku moja Ibn Al-Hasan At-Tamiymiy
alimpiga Ng'e akaingia shimoni na yeye akaingiza kidole chake nyuma yake
ndani ya hilo tundu, ng'e akamgonga kwa mwiba wake wa sumu; akaulizwa
kuhusu jambo hilo? Akasema: "Nilihofia asije akatoka na kumgonga mama
yangu''
Na
amesema Muhammad Ibn Siyriyn: ''Ulifikia mtende mmoja wakati wa Khalifa
'Uthmaan kuuzwa kwa Dirhamu elfu moja. Usaamah bin Zayd akajitahidi
akanunua mtende mmoja akautoboa na kutoa utomvu wake akamlisha Mama
yake. Watu wakamuliza, ni kipi kilichokupelekea kuuchezea mtende namna
hii na wewe unaona mtende umefikia kuuzwa ghali namna hii; dir'hamu alfu
moja? Akasema: "Hakika mama ameniomba. Na hawezi Mama yangu kuniomba
kitu chochote ninachokiweza isipokuwa nitampa).
'Abdullaah bin 'Awn nae siku moja aliitwa na mama yake, na yeye akanyanyua sauti yake ikawa juu ya sauti ya mama yake. Kwa kosa hilo tu akaamua kuadhibu nafsi yake kwa kuacha huru watumwa wawili!
Na
Zaynul-'Aabidiyn (pambo la wacha Mungu) naye alikuwa ni mtu mwenye
kufanya wema sana kwa mama yake. Lakini hakuwa akila naye sahani moja,
siku moja akaulizwa mbona wewe ni mwenye kufanya wema kwa mama yako
kuliko watu wote lakini hatukuoni ukila nae sahani moja? Akajibu
akasema: "Ninaogopea mkono wangu kutangulia kufika pale mahali lilipotangulia kuona jicho lake hivyo nikawa nimemvunjia heshima" Hakika washatangulia mbele yetu watu hawakuwa akirefusha mmoja wao nyumba yake kupita kimo cha mama yake!!
Hakika ni pepo, ewe mtafuta pepo lazimiana (shikamana) na nyayo zake hapo ndipo ilipo pepo.
Amepokea Hadiyth hii At-Tirmidhiy na akaisahihisha kutoka
kwa Abu Dardaa (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: nimemsikia Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Mzazi ni mlango
wa katikati ya milango ya pepo, ukitaka upoteze mlango huo au
uhifadhi)).
Na katika At-Tirmidhiy, kutoka
kwa 'Abdullaah bin 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) kutoka kwa Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Radhi za Mola
zinatokana na radhi za mzazi, na chuki zake zinatokana na chuki za
mzazi))
Amesema Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhu):
"Hakuna Muislamu yeyote mwenye wazazi wawili Waislamu akaamka akitaka
thawabu kwa Allaah kupitia kwao, isipokuwa Allaah Hufungua milango
miwili – yaani katika pepo na ikiwa ni mmoja basi utafunguliwa mmoja, na
akimkasirisha mmojawapo, Allaah Hatomridhia mpaka mzazi amridhie).
Akaulizwa hata kama wamedhulumu? Akasema: Hata kama wamedhulumu.
Anasema mshairi mmoja:
Mama yako ana haki kubwa sana kwako lau ungejua,
kingi chako wewe huyu mbele yake ni kichache.
Ni masiku mangapi amekesha akishitakia shida zako,
kwake akakesha akiungulia moyo wake na kupiga makelele.
Na wakati wa kujifungua hujui mazito yanayompata,
hivyo kwa yanayomkwaza nyoyo zinakaribia kuruka.
Na ni mara ngapi amekuoshea uchafu kwa mkono wake wa kulia,
na halikuwa paja lake kwako ni kitanda.
Na ni mara ngapi amepata njaa na akakupa chakula chake,
kwa sababu ya huruma na uchungu kwako ukiwa mdogo.
Ukamtupa pale ulipomfanyia ubaya katika hali ya ujinga,
na likarefuka kwako jambo na hali ya kuwa yeye ni mfupi.
Majuto ni kwa yule aliyeelewa (ubora wa mama) lakini akafuata matamanio,
na majuto ni kwa kipofu wa moyo hali ya kuwa macho yanaona.
Basi jipendekeze katika kukithirisha kumuombea dua,
kwani wewe unaloliomba una haja nalo zaidi.
Siku
moja Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) alimuona mtu mmoja M-yemen
akitufu Al-Ka'abah huku amembeba mama yake mgongoni mwake huku akisema:
Hakika mimi ni ngamia wake aliyedhalilishwa, ikiwa abiria wake
watamkorofisha, basi mimi siogopi, Allaah ndiye mola wangu mwenye
utukufu mkuu, nimembeba mara nyingi zaidi kuliko alivyonibeba, Je, ewe
Ibn 'Umar unahisi nitakiwa nimeshamlipa? Ibn 'Umar akasema: ''Hapana,
hujamlipa hata pumzi moja''
Nasaha kwa wale wanaowafadhilisha (wanaowatanguliza) wake zao kuliko mama zao;
Na kwa wale wanaowapa wake zao na kuwanyima mama zao.
Usimtii mke ukamkata mama juu yako, ewe kijana wa ndugu yangu umepoteza umri wako.
Ni vipi unamkana mama wakati mimba yako kaibeba yeye, tena umegaragara mapajani mwake kwa uzito.
Na akauguza maumivu ya nafsi kwa ajili yako na ni kwa kiasi gani, alifurahi alipozaa mtoto wake akawa ni mwanamme.
Na hakuonyesha mpaka miaka miwili iliyokamilika, na huku akitaka kunyeshelezwa katika kifua chake na matiti yake ya lulu.
Na kile ulichokinyonya kutoka kwake unakitoa na kumchafua, bila yeye kulalamikia uvundo wa uchafu.
Na ameamiliana nawe kwa wema na malezi mema mpaka, umelingana sawa na mpaka umekuwa namna unavyojiona.
Hivyo usimfadhalishe mke kuliko yeye milele, na wala usiache moyo wake ukivunjika kwa kumtenza nguvu.
Mzazi ndio mlezi wa kwanza hilo halipingiki, mlinde hasa hasa akifikia utu uzima.
Huwezi kumtekelezea haki zake zilizo juu yako hapo, juu ya macho yako amehiji nyumba tukufu na akafanya 'Umrah.
Enyi
waumini, ni masaa mangapi Muislamu ametumia kuwatimizia haja wazazi
wawili, kwa hilo Allaah Amekuondolea mawazo ya kufadhaisha shida, ni
wangapi katika mtoto wa kiume mwema kwa wazazi wake au msichana mwema
kwa wazazi wake, wamesimama mbele ya wazazi wao baada ya salamu au
maneno mazuri au zawadi kwa unyenyekevu, huku imefunguliwa milango ya
mbingu kwa ajili ya maombi yao yenye kujibiwa kutoka kwa wazazi wao
wawili walio dhaifu waliozeeka.
Hivyo
mcheni Allaah kwa wazazi wawili, hasa hasa wanapofikia umri mkubwa na
uzee kiasi walipofikia, na kudhoofika kwao mifupa, na kichwa kuwaka mvi,
watakapokuwa wamefikia hali waliyoifikia na wakawa wanakuangalia
muangalio ambao unangojea tonge kwa furaha au kipawa cha malipo.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) anasema katika Qur-aan Suratul Al-Israai aya ya 23 kwamba:
{{Amehukumu
mola wako kuwa asiabudiwe (yeyote) isipokuwa Yeye (tu) na wazazi
watendewe wema, kama mmoja wao amefikia uzee (naye yuko) pamoja nawe, au
wote wawili, basi usiwaambie hata aah! Wala usiwakemee, na useme nao
kwa msemo wa heshima}}
Hali Ya Mama Na Watoto Wake Katika Maafa Ya Moto
Anahadithia
mmoja wa askari wanaofanya kazi katika kitengo cha ulinzi wa mji
(zimamoto) akasema: "Hakika wao walifika katika nyumba moja inayowaka
moto na ndani yake alikuwepo mama mmoja na watoto wake watatu. Moto
ulianzia katika moja ya vyumba (vya nyumba ile) akajaribu yule mama
kutoka kupitia milangoni lakini akakuta milango (yote) imefungwa.
Akapanda haraka pamoja na watoto wake watatu mpaka sehemu ya juu ya
nyumba ili atokee kupitia mlango huo, akaukuta umefungwa vile vile.
Akajaribu kila njia bila mafanikio, akarudia rudia mpaka akachoka. Moshi
nao ukapaa na kuenea nyumba nzima, wakawa wanahema kwa taabu. Mama
akaamua kuwakumbatia watoto wake akawakumbatia kifuani mwake, na hali ya
kuwa chini ili usije ukawafikia moshi mzito. Na mama wa huruma anauvuta
moshi huo yeye (lakini si wanae). Baada ya kufika vikundi vya uokozi
juu ya nyumba wakamkuta amedondoka (amelalia) tumbo lake, wakamyanyua
mara wakawaona watoto wake watatu chini yake wakiwa maiti!!. Kama vile
ndege anayewafunika mbawa vifaranga vyake akiwaepusha na hatari.
Akiwakinga na adui mvunjaji. Wakakuta ncha za vidole vya mkono wake
vimevunjika, kwani alikuwa mara akijaribu kufungua mlango, kisha anarudi
kwa watoto wake ili kuwakinga na muwako wa moto na mpalio wa moshi kwa
mara nyingine, mpaka akafa na watoto wake wakafa!
Katika
picha inayopamba uzuri wa kujitoa muhanga, katika ubao uliohifadhiwa
kwa rangi za huruma na kunakishiwa na unyoya wa upole na huruma. Pamoja
na kujitolea na juhudi zote hizi na aina mbalimbali za kuhifadhi na
ulinzi ambao mama anautoa kwa mwanae na kwa kipande cha ini lake, mpaka
akasema
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika
kubainisha ukubwa wa haki ya mama pamoja na baba: ((Mtoto hawezi kumlipa
mzazi wake kwa wema aliomtendea isipokuwa, amkute akiwa mtumwa na
kumnunua kisha amwache huru)). [Ameisimulia Imaam Muslim].
Pamoja
na mapenzi yote haya yenye kububujika na upole mwingi na huruma yenye
kuchupa tunasikia na tunaona aina mbalimbali za ugomvi na ukanaji wa
wema, na ususuwavu wa moyo wa kushangaza, na ukali wa kutisha, na ubaya
wa matendo, na ubaya wa kuamiliana (na wazazi) kiasi cha kutokuingia
akilini (akili yoyote) wala kubebwa na moyo wowote (kuvumiliwa).
Barua Ya Mama Kwa Mwanawe
Hebu soma hii barua iliyoandikwa kwa wino wa machozi kutoka kwa mmoja wa akina mama.
Barua
yenyewe hii hapa aliyoiandika Mama mmoja kwa wino wa machozi yake.
Barua ameituma "Mama Makluumah" kwa kijana wake ambaye ni kama manukato
ya moyo wake, maskini yule mama anasema:
"Ewe
kijana wangu, tangu miaka ishirini na tano (iliyopita) ilikuwa ni siku
yenye mwanga katika maisha yangu pale aliponifahamisha Daktari wa kike
kwamba mimi ni mja mzito. Na akina mama ewe mwanangu, wanajua vizuri
maana ya hili neno (uja uzito) nalo linaleta maana ya kuchanganyika na
furaha na ni mwanzo wa matatizo na mabadiliko ya kinafsi na ya kimwili
kwa mama na baada ya ishara hii ya kuwa mja mzito ewe
mwanangu-nikakubeba miezi tisa tumboni mwangu kwa furaha, (nilitaka
kusimama) nasimama kwa taabu na ninalala kwa shida, na ninakula udongo,
na ninapumua kwa uchungu, lakini yote hayo hayakunipunguzia mapenzi
yangu kwako na furaha yangu kwako, bali yakamea mapenzi ya kukupenda
kadri siku zinavyosonga mbele.
Na
ikakuwa shauku kwako. Nimekubeba ewe mwanangu juu ya uchungu, isipokuwa
mimi pamoja na yote hayo nilikuwa nikifurahi na kufurahi kila
ninapohisi kutingishika kwako ndani ya tumbo langu, na ninafurahi kwa
kuongezeka uzito wako pamoja na kwamba ni mzigo mzito sana kwangu,
hakika yalikuwa ni mateso ya muda mrefu, mara ikafika baada ya hayo yote
Alfajiri ya usiku ule ambao sikulala ndani yake, na wala sikufumba
jicho, na ukanikuta uchungu na shida na hofu na woga ambao kalamu
haiwezi kuandika (kusifia) wala ulimi kuelezea, na nikaona kwa mboni ya
jicho langu- namuapa Allaah ewe mwanangu nikayaona mauti yakinijia mara
nyingi, mpaka ukawa umetokea duniani! Yakachanganyika machozi ya kilio
chako na machozi ya furaha yangu. Na yakaondoka machungu yangu yote na
majeraha yake. Ewe mwanangu, ikipita miaka katika umri wangu nikiwa
nakubeba, moyoni mwangu na ninakuosha kwa mkono wangu, nikajaalia mapaja
yangu kuwa kitanda chako. Na kifua changu kuwa ni chakula chako,
nimekesha usiku wangu ili ulale, nimetaabika mchana wangu ili uwe
muungwana, utukuke, matamanio yangu ni kuona tabasamu lako, na furaha
yangu kila wakati ni kukuona unanitaka nikufanyie kitu chochote. Huo
ndio mwisho wa utukufu wangu. Siku zikapita na mausiku yakapita nami
nikawa katika hali hiyo, nikawa mtumishi bila kupunguza utumishi wangu.
Na nikawa mnyonyeshaji asiyesimamisha huduma yake. Na nikawa mfanyakazi
asiyechoka, mpaka ikakomaa miguu yako na kulingana sasa ujana wako, na
zikaanza kuonekana kwako alama za kiume, mara nikaanza kwenda mbio kulia
na kushoto ili kukutafutia mke umtakae, ukafika muda wa ndoa yako, moyo
wangu ukakatika na yakatirizika machozi yangu kwa furaha kwa ajili ya
maisha yako mapya yenye utukufu, na nikawa mwenye huzuni kwa kutengana
na wewe. Yakapita masaa mazito, mara wewe sio yule mwanangu niliyemjua.
Hakika umenikana na umejisahaulisha haki zangu, yanapita masiku sikuoni
na wala sisikii sauti yako, umeshindwa kumuelewa mtu aliyesimama kidete
kwa ajili yako, umemsahau Mama yako.
Ewe
mwanangu sihitaji kwako ila kitu kidogo tu. Nifanye mimi ni katika
marafiki zako na machoni kwako, na wengine wasogeze hatua moja mbele
yako.
Nifanye
Mimi ewe mwanangu, ni moja ya vituo vya maisha yako ya mwezi ili
nikuone humo japo kwa dakika chache. Ewe mwanangu, mgongo wangu
umepinda, na viungo vyangu vimedhoofika, na maradhi yamenikondesha, na
yamenitembelea maradhi, sisimami ila kwa taabu, na sikai ila kwa
mashaka, na haukuacha moyo wangu ukizingazinga kwa mapenzi yako, kama
angekukirimu mtu yeyote siku moja ungemsifu kwa kitendo chake kizuri
alichokufanyia. Na ewe mwanangu Akulinde Mola wangu, mama amekufanyia
wema (ihsani) ambayo huioni, na wema ambao hutaki kuulipia; hakika
amekutumikia na kulisimamia jambo lako miaka na miaka, basi yako wapi
malipo yake?! Umefikia upeo huu na kuwa na moyo mgumu kiasi hiki, na
masiku yakakuzuia kiasi hiki kuja kuniona?!
Ewe
mwanangu, kila nikifahamu kwamba wewe ni Muungwana katika maisha yako,
furaha yangu huzidi, lakini naona ajabu na hali yakuwa wewe ni bidhaa
iliyotengenezwa na mkono wangu, na kujiuliza ni kosa gani nimelifanya
mpaka nimekuwa adui yako huwezi kuniona na kuwa mzito kwangu?!
Siwezi
kupelekea mashtaka yako kwa Allaah, wala huzuni zangu kwa sababu
nikiyapeleka juu ya mawingu na kuyakokota mpaka katika mlango wa mbingu,
utapatwa na shari ya kugombana na wazazi, na adhabu itakuteremkia, na
utashuka nyumbani kuwa kipande cha ini langu na manukato ya maisha yangu
na furaha ya dunia yangu.
Zinduka
ewe mwanangu, mvi zimeanza kuenea kichwani mwako, na itapita miaka
kisha utakuwa baba mzee, na malipo yanategemea matendo, utakuja andika
barua nyingi kwa mtoto wako, kwa wino wa machozi kama nilivyokuandikia
mimi barua hii. Na kwa Allaah watakusanyika wagomvi wote ewe mwanangu,
mche Allaah kwa Mama yako, mfutie machozi yake, na mpungizie huzuni
yake, ukitaka baada ya hapo chana barua yake, na elewa ya kwamba yeyote
mwenye kutenda wema, ni kwa ajili ya manufaa ya nafsi yake na mwenye
kufanya ubaya ni kwa madhara yake mwenyewe.
(Imetokana
na khutbah ya Maazin At-Tuwayjiriy amesema; "nilimuuliza Al-Hasan Al
Baswriy: "Ni ipi dua (maombi) ya mzazi kwa mwanae? Akasema Al-Hasan "Ni
kuokoka" akasema, nikamuliza tena na kwake (kwa mzazi)? Akasema:
"Kuangamia kwake (Yaani mzazi humuombea mwanae kuokoka na kila balaa,
lakini mtoto humuombea mzazi wake afe haraka ili apumzike na kero zake)!
Haki Za Mama Yako Anazodai Kwako
Hakika haki za mama kwa mtoto ni kubwa mno, usimuite kwa jina lake, bali muite kwa jina analolipenda au kun-yah
(yaani 'mama fulani') usikae kabla yake, na wala usitembee mbele yake,
kutana nae kwa uso mchangamfu, busu kichwa chake na shum mkono wake, na
ukimnasihi basi ni kwa mema bila ubaya (usimuudhi) itika wito wake pindi
akuitapo bila kumkemea au kumkirihisha. Zungumza naye kwa maneno laini,
mlishe akiwa na njaa, au akitamani kitu japo utafika mbali katika
kutafuta mletee, mpe zawadi kabla hajakuomba chochote, hisi
anachokipenda umpe, kuwa mtumishi mtiifu kwake, mtii katika mambo ambayo
si maasi, usimtanulie katika kula au kunywa, umfurahishe kwa kumuombea
usiku na mchana rehema na msamaha, funga jicho lako kuhusu makosa yake
na kuteleza kwake, usisikitike au kumhadithia makosa yake na kwa mtindo
wa kumshtaki au kumshinda.
Muheshimu
Mama yako na umkirimu, usimfanyie kibri wewe si chochote si lolote
mbele yake kwani uliishi kati ya mapaja yake na mikono yake. Muingizie
furaha, kaa naye kwa wema, taka dua kwake kwani milango ya mbingu
hufunguliwa kwa ajili yake.
Mama Yako Baada Ya Kifo Chake
Ndugu
yangu mpendwa, jua Akurehemu Allaah ya kwamba, hakika kuwatendea wama
wazazi wawili hakuishi kwa kifo chao, kwani imepokelewa Hadiyth kutoka
kwa Abu Usaydi As-Sa'adiy amesema: "Wakati
sisi tuko mbele ya Mtume, mara ghafla akamjia mtu mmoja kutoka kwa Banu
Salimah akasema: "Ewe Mtume wa Allaah, je, kumebakia chochote katika
wema kwa wazazi wangu wa kuwafanyia baada ya kifo chao? Mtume akasema:
((Ndiyo! Ni kuwaombea rahma kwa Allaah na kuwaombea msamaha na
kutekeleza ahadi zao baada yao, na kuunga undugu ambao hauungwi kwa wao,
na kuwaheshimu marafiki zao))
Wema kwa wazazi wawili unaendelea katika kizazi cha mwanadamu na kinachofuata baada yake, imepokelewa kutoka kwa Ibn 'Umar, amesema
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
((wafanyieni wema wazazi wenu, nanyi watoto wenu nao watajiheshimu))
Vile
vile wema kwa wazazi wawili unazidisha umri (Akipenda mwenyewe Allaah)
kwani imepokewa kutoka kwa Sahal bin Mu'aadh, ya kwamba Mtume
wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Yeyote atakayewatendea wema wazazi wake wawili, kheri nyingi sana ni zake yeye, Allaah Atamzidishia umri wake))
Tunamuomba Allaah Atusaidie kuwafanyia wema wazazi na kuwatii na kuwafanyia Ihsani wakiwa hai na wakiwa wamekufa, na asitufishe isipokuwa pale atakapokuwa Yu radhi na sisi, na tunamuomba Allaah Azishushe Rahma na Baraka na Amani Zake kwa Muhammad na kwa ahli zake na Maswahaba.
No comments:
Post a Comment