Mara
baada ya kurudi katika safari ya Miraji aliyopelekwa ndani yake mpaka
mbingu ya saba, kisha akasogezwa mahali panapoitwa ‘Sidratul muntaha na
kuzungumza na Mola wake Subhahanu wa Taala, kisha akarudishwa ardhini
katika usiku huo mmoja, na kabla ya kumhadithia mtu yeyote juu ya safari
yake hiyo adhimu, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
alikuwa amekaa kimya nje ya msikiti wa Al Kaaba, na Abu Jahal alipomuona
katika hali ile akamuendea na kuanza kumkejeli huku akimuuliza.
"Enhe! Vipi pana habari yo yote mpya kutoka mbinguni leo?"
Kwa
utulivu na upole Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
akamjibu: "Ndiyo, nilipelekwa usiku wa leo mpaka Baitul Maqdis
(Palestina)."
Abu Jahal: "Na asubuhi hii ukarudi Makkah?"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Naam, na nilisali na ndugu zangu Manabii huko."
Abu Jahal akapiga ukelele kama mwenda wazimu na kuwaita jamaa zake.
"He! Amma leo Muhammad ametia fora"
Akaanza
kuwahadithia yale aliyoyasikia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam), jambo lililowafanya hata baadhi ya waliosilimu
karibuni wastushwe na habari hizo na kurudi nyuma kidogo.
Washirikina
wa Kikureshi wakaona kuwa leo ndiyo siku ya kumfedhehesha Muhammad
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtenganisha na sahibu
yake Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu), wakaanza kusemezana;
"Abubakar
anajua kuwa inachukua miezi mingi kusafiri kutoka Makkah hadi Sham,
mahali ulipo msikiti huo wa Baytul Maqdis, maana kesha safiri kwenda
huko mara nyingi, na leo Muhammad anasema eti amesafiri hadi huko ndani
usiku mmoja tu"
Wakenda mpaka nyumbani kwa Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumgongea mlango huku wakimwita kwa sauti kubwa: "Abubakar!",
Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akauliza: " Kuna nini tena?"
Makureshi: "Rafiki yako Muhammad …"
Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu): "Amefikiwa na jambo lolote?"
Makureshi:" "Eti anasema kuwa amesafiri usiku wa leo kutoka Makkah hadi Baytul Maqdis na kurudi."
Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu): "Ni yeye Mwenyewe aliyesema hayo?"
Makureshi: " Ndiyo! Tena tumemsikia kwa masikio yetu!"
Abubakar
(Radhiya Allaahu ‘anhu): "Ikiwa Yeye Mwenyewe amesema hivyo, basi mimi
namsadiki. Mimi namsadiki kwa mambo makubwa kupita hayo. Nasadiki kuwa
anapata Wahyi unaotoka mbinguni, basi nisimsadiki juu ya kwenda hapo
Baytul Maqdis?"
Hii
ndiyo Imani ya Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambayo ikiwekwa upande
mmoja wa mizani na zikiwekwa Imani za watu wote upande wa pili, basi
imani ya Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) itazidi uzito.
Abubakar
(Radhiya Allaahu ‘anhu) akavaa nguo zake, akatoka na kwenda kumtafuta
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliyemkuta amekaa
kimya peke yake nje ya Al Kaaba, akamsogelea na kumkabili, kisha kwa
utulivu na khushuu akamkumbatia na kumwambia;
"WAllaahi wewe husemi uwongo na mimi nakusadiki , WAllaahi nakusadiki."
No comments:
Post a Comment