بسم لله الرحمن الرحي
Alhamdulillaahi Rabil-´Aalamiyn, swalah na salaam zimwendee mja wake na Mtume Wake Muhammad (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ahli zake na Maswahaba wake (radhiya Allaahu ´anhum). Amma ba´ad:
Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Kaumba mume na mke kutokana na hekima kubwa. Lau kusingelipatikana ila mwanaume tu, au kusingelipatikana ila mwanamke tu, kungekuwepo kasoro nyingi kwa kila mmoja na kusingelipatikana utulivu. Hili lamuhusu mwanaadamu. Hali kadhalika kwa viumbe vingine vyote.
وَمِن كُلِّ شَيْءٍ خَلَقْنَا زَوْجَيْنِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ
”Na katika kila kitu Tumeumba kwa jozi ilimzingatie.” (51:49)
وَالَّذِي خَلَقَ الْأَزْوَاجَ كُلَّھَا
”Na Ambaye ndiye Aliyeumba katika kila kitu jike na dume.” (43:12)
Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Kafanya hili kwa hekima kubwa. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Kamkirimu mwanaadamu.
وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ
”Na hakika tumewatukuza wanaadamu.” (17:70)
Kamkarimu zaidi ya viumbe vingine vyote. Na katika ikram za Allaah kwa mwanaadamu ni kuwa hakumwacha hovyo kama wanyama ambao wanaingiliana wao kwa wao wanaume kwa wanawake kwa ajili ya kujitoa matamanio tu, kisha wanafarakana na wala hawajuani baadhi yao, na wala hawana nyumba na jamii. Ila Allaah Kamkarimu mwanaadamu kwa mengi, na katika hayo ni pale Aliposema:
وَللهُّ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم بَنِينَ وَحَفَدَةً وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ
”Na Allaah Amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na Akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na Akakuruzukuni vitu vizuri vizuri.” (16:72)
Hizi ni katika neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa mwanaadamu.
Hekima ya ndoa katika Uislamu ni kubwa na pia ni kujilinda na tabia mbaya, zinaa na kufanya machafu. Kwa kuoa, mtu hujilinda na mambo haya kwa idhini ya Allaah – kwa watu wa iymaan; ama makafiri na watu wanaofuata matamanio hawa hawazingatiwi. Ama kwa watu wa iymaan wanapata utulivu kwa hilo.
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْھَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً
”Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu.” (30:21)
Hii ni katika hekima kubwa ya Allaah Kujaalia baina ya mume na mke mapenzi na huruma, ili wasifarakane na wasichokane.
Hakika mwanamke ana haki zake juu ya mume wake.
Ya kwanza ni juu yake kumhudumia, matumizi ni kwa mwanaume na siyo mwanamke. Mwanamke hamhudumii (hampi matumizi) mwanaume. Bali matumizi ni kwa mwanaume yeye ndiye humhudumia mwanamke.
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاء بِمَا فَضَّلَ للهُّ بَعْضَھُمْ عَلَى بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُواْ مِنْ أَمْوَالِھِمْ
”Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Allaah baadhi yao juu ya baadhi, na kwamali yao wanayo yatoa.” (04:34)
Na alipokuja Hind kwa Mtume wa Allaah ( صلى لله عليه وسلم ) akimshtaki mume
wake kuwa hawapi matumizi yakuwatosheleza na yanawatosha watoto wake
tu. Akamwambia Mtume ( صلى لله عليه وسلم ) chukua kinachokutosheleza kwa
wema. Akamwambia Mtume ( صلى لله عليه وسلم ) achukue matumizi yake kwa
mume ikiwa ni bakhili, atachukua mke matumizi yatayomtosheleza yeye na
watoto wake.
Hii ni wajibu kwako. Na si pendekezo, bali ni haki wajibu juu yake [mume]. Na matumizi inatakikana iwe kwa wema, kwa mambo yanayojulikana na watu katika kila zama na mahala. Tajiri ana matumizi yake na fakiri ana matumizi yake, na mtu wa kati na kati ana matumizi yake. Hii ni katika haki ya mke juu ya mume wake, matumizi kwa wema. Amsimamie kumpa matumizi yake.
Na wala siyo lazima mwanamke ashiriki katika [kusaidia] matumizi, hata akiwa na mali nyingi si lazima kwake kutoa kitu katika matumizi ila kwa kupenda kwake mwenyewe. Kwa kuwa matumizi yake ni wajibu kwa mume kwa mujibu wa ndoa, na kwa mujibu wa mkatabaulio baina yao. Na hili ni katika Alilomfadhilisha Allaah mwanaume zaidi kuliko mwanamke. Ni kule suala la matumizi likawa jukumu la mume na si mwanamke.
Hali kadhalika utulivu, haki ya mke juu ya mume wake ni kumpa utulivu utaoleta amani na pozo.
Katika haki za mke juu ya mume wake kumkatia nguo inayomfaa khasa wakati wa sherehe n.k, katika mavazi wanayovaa wanawake katika mji huo. Na mambo haya ni katika haki za mke juu ya mume wake. Matumizi, utulivu na kumkatia nguo. Na ikiwa mume hawezi mambo haya, hapo mwanamke ana khiyari aidha ya kubaki na kuvumilia hali hii - Alhamdulillaah, na akitaka kufarakana naye anaacha naye. Ili kumuondolea madhara mwanamke. Hizi ni katika haki za Uislamu ilizompa mwanamke.
Katika haki za mke juu ya mume wake, ni kumlinda na haramu - kwakumjamii kadiri na atavyoweza. Na hili ni katika kusudio kubwa la ndoa. Mwanamke kumlinda mwanaume na mwanaume kumlinda mwanamke. Ama mume akimtenga na hawana maingiliano yoyote, hili litaleta madhara. Akitaka mwanamke kusubiria hali hii sawa, la sivyo wafarakane ili kujiondolea madhara ikibainika kuwa mume hana uwezo wa kujimai.
Katika haki za mke juu ya mume wake; ni pale mume atapotaka kuoa mwanamke wapili, au watatu au wanne - ana ruhusa ya hilo. Allaah Kamruhusu. Mwanamke awe radhi kwa hilo kwa kuwa hili ni jambo kamruhusu nalo Allaah. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):
فَانكِحُواْ مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ
“Basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane.” (04:03)
فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً
“Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu.” (04:03)
Ama mkijiamini katika nafsi zenu kusimama na uadilifu - ukifanya uadilifu, ukitaka hilo ni ruhusa kwako au ni mwenye haki ya hilo. Na hili la ukewenza lina maslahi makubwa katika jamii, [maslahi] kwa wanawake. Maslahi ya ukewenza ni zaidi kwa wanawake kuliko maslahi yanayopatikana kwa waume. Kwa kuwa mume ndiye mwenye kuchukua jukumu la kupambana na baadhi ya hao wake zake; kila mmoja ampe matumizi, kumkatia nguo, makazi na mengineyo.
Isitoshe wanawake katika kila jamii ndio wengi zaidi kuliko wanaume, kila mwanaume akibaki kuoa mke mmoja kutabakia wanawake wengi sana. Kutokana na rahma ya Allaah [kwa wanawake] Akaweka katika Shari´ah ukewenza, kwa ajili ya kuondosha uchafu na wanawake [wasiyokuwa na waume] kuwa wengi. Lau mume ataishia kuoa mwanamke mmoja wanawake watakuwa wengi katika jamii, na ufisadi utaenea kunako tabia. Mwanamke ni mwenye haja ya ataemsimamia, atamlisha, kumtetea. Yeye ni mwenye haja ya mume.
Hivyo hekima ya ukewenza ni kubwa. Wale wanaopinga ukewenza - wanasema kuwa hii ni dhuluma kwa mwanamke. Hili ni kutokana na ufahamu wao mbaya au ni kutokana na ´Aqiydah [itikadi] yao mbovu. Bali la ukewenza lina khayr nyingi kwa wanawake na si kwa wanaume.
Kwa kuwa maslahi ya ukewenza kwa wanawake ni makubwa kuliko maslahi wanayopata wanaume. Kwa kuwa wanawake ndiyo wenye haja kubwa kwa wanaume kuliko wanaume. Na ni bora kwa mwanamke kuolewa na mume aliye na wake wanne; na mume anaemsimamia kwa mahitajio yake na anamhifadhi, anakuwa mahram wake, na huenda Allaah Akawaruzuku
watoto. Haya maslahi ni bora kuliko kubaki bila ya kuwa na mume. Hata akiwa ni mwanamke wanne. Jambo la ukewenza katika Uislamu lina hekima kubwa.
Hawa wanaopinga ukewenza na wanasema kuwa ni dhuluma kwa mwanamke, huku ni kujidanganya na kuwa na ufahamu mbaya. Au ni upotofu! Subhaana Allaah! Wanaruhusu uzinzi na wanapinga ndoa ya Kishari´ah! Hizi ndizo dini za kijaahiliyyah na dini ya kinaswara ambao nao wanapinga ukewenza. Wanapinga ndoa ya Kishari´ah nzuri na wanaenda kufanya uhuni wa kila ainanje. Mwanaume na mwanamke wanafanya wapendacho ila tu wasifanye ndoa, kisha wanaita [ukewenza] ndiyo uchafu!! Uchafu ni kwao - A´udhubillaah. Na huku ni katika kubadilisha maumbile. Na wao wanataka waislamu wawe hivyo. Na waumini hawataki hilo.
Hivyo mume akitaka kuongeza mke hana kipingamizi, si kwa hakimu, si kwa mke wake wala kwa walii wa mke. Kwa kuwa hili ni jambo kamruhusu nalo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), na hili ni kutokana na maslahi ya jamii. Hana kipingamizi. Isipokuwa tu ikiwa mwanamke alimuwekea sharti wakati wa ndoa asioe mwengine, alimuwekea sharti asioe mwengine; tunasema hili haliwezi kuzuia yeye kuoa, hata kama mwanamke alimuwekea sharti haliwezi kumzuia kuoa. Kwa kuwa hili ni jambo kamruhusu Allaah na wala hakuna yeyote awezae kumkataza. Lakini mwanamke ana khiyari, akio mwanamke mwengine ana khiyari. Akitaka atabaki naye na akitaka ataomba kufarakana naye. Ana khiyari aidha ya kubaki au kufarakana. Lakini mwanamke ana khiyari, akioa mwanamke mwengine ana khiyari. Akitaka atabaki naye na akitaka ataomba kufarakana naye. Ana khiyari aidha ya kubaki au kufarakana. Kwa kuifanyia kazi kauli ya Mtume (´alayhis-Salaam):
"Waislamu wako kwa masharti yao [wanayowekeana]."
Lakini si katika sharti yake [mwanamke] kumkatalia kuoa, hapana ni haki
yake. Lakini akitaka kutengana naye ataenda mahakama na athibitishe kama
kweli alimuwekea sharti, halafu hapo yeye ndio atakuwa na khiyari. Ima
abaki naye au wafarakane kwa kuifanyia kazi sharti.Lakini ukewenza
alioruhusu Allaah Kauwekea sharti la mtu kufanya uadilifu baina ya wake
wawili.
فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً
“Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu.” (04:03)
(Allaah) Akaweka sharti ya ukewenza, mtu afanye uadilifu baina ya wake zake.
Na uadilifu ni kufanya nini?
Uadilifu alioweka Allaah ni ule unaowezekana; uadilifu katika matumizi, utulivu, kumkatia nguo, kitandani kuwagawia siku sawa. Na haijuzu huku walala siku kadhaa kwengine chini ya hapo. Haijuzu kufanya hivi. Lazima wote uwagawie siku sawa. Huu ndiyo uadilifu unaotakikana. Wanawake lazima watendewe haki sawa katika matumizi, utulivu, kuwakatia nguo na siku za kulala.
Ama mapenzi ya moyoni ukampenda mmoja zaidi kuliko mwengine, hili halimiliki yeyote ila Allaah (Jalla wa ´Alaa). Mume anaweza kuwapenda baadhi ya wake zake zaidi kuliko wengine, yaliyo moyoni yanamilikiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hili mume hakalifishwi. Si katika sharti kuwapenda wote sawa, hutoweza. Huwezi kugawa mapenzi baina ya wake sawa sawa, hili liko kwenye Mkono wa Allaah (Jala wa ´Allaa). Na kutokana na hili Kasema Allaah (Jalla wa ´Alaa) katika Aayah nyingine:
وَلَن تَسْتَطِيعُواْ أَن تَعْدِلُواْ بَيْنَ النِّسَاء وَلَوْ حَرَصْتُمْ فَلاَ تَمِيلُواْ كُلَّ الْمَيْلِ فَتَذَرُوھَا كَالْمُعَلَّقَةِ
“Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake, hata mkikakamia. Kwa hivyo msimili moja kwa moja mkamwacha (mmojapo) kama aliye tundikwa.” (04:129)
Mahaba na mapenzi ya moyoni haya yako kwenye Mkono wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Lakini mume asimili kwa mke mmoja akadhihirisha [wazi wazi] kuwapenda baadhi ya wake zake zaidi kuliko wengine, akawapendelea wao na kumdhulumu wapili. Akampa vingi zaidi kuliko yule asiempenda. Akampa matumizi mengi, kumuweka katika makazi mazuri [kuliko mwengine], hili halijuzu. Kumilia. Analala kwa yule ampendae siku nyingi zaidi ya yule asiempenda, huku ni kumilia. Na imekuja katika Hadiyth:
"Yule mwenye wake wawili, akamkandamiza mmoja zaidi kuliko mwengine, atakuja siku ya Qiyaamah na bega lake likiwa limepinda."
Itakuwa ni fedheha kwake - Allaah Atukinge. Na malipo yanatokana na chanzo cha amali. Haya ni makemeo makali.
Tumejifunza katika haya kuwa uadilifu umegawanyika namna mbili, uadilifu unaowezekana na ndiyo alioutaja Allaah (Ta´ala):
فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً
“Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu.” (04:03)
Na audilifu usiowezekana. Na huu ndio uliousema Allaah (Ta´ala):
وَلَن تَسْتَطِيعُواْ أَن تَعْدِلُواْ بَيْنَ النِّسَاء وَلَوْ حَرَصْتُمْ
“Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake, hata mkikakamia.” (04:129)
Makusudio ni ulaini wa moyo na mapenzi ya moyo, hili liko kwenye Mkono wa Allaah. Lakini asimili ikiwa anapenda baadhi ya wake zaidi kuliko mwengine, asidhihirishe hilo ikawa anampendelea mmoja na anamkandamiza mwengine kunako haki zake. Uwezo wa kuwapa matumizi, utulivu na mavazi sawa unamiliki haya, haya unayaweza. Na kutokana na hili Akasema:
فَلاَ تَمِيلُواْ كُلَّ الْمَيْلِ
“Kwa hivyo msimili moja kwa moja.” (04:129)
Yaani akamili mapenzi ya moyoni na mapenzi ya matendo. Huku ndio kumili moja kwa moja.
فَتَذَرُوھَا كَالْمُعَلَّقَةِ
“(Mmojapo) akawa kama aliye tundikwa.” (04:129)
Hajulikani ana mume na isitoshe siyo mwenye kutalikika. Ni dalili kuwa kilichokatazwa ni kumili moja kwa moja, ama kulimi kidogo nako ni kumili kwa [mapenzi ya] moyo, hili haliko katika uwezo wa binaadamu. Anaweza kuwapenda baadhi ya wake zake zaidi kuliko wengine. Mapenzi hili linatokana na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), na [mapenzi ya] moyo yako kwenye Mkono wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Sisi tumekalifishwa kwa yale tunayoweza.
Hizi ni katika haki za mke juu ya mume wake, akioa mwanamke mwengine - wapili, watatu au wanne afanye uadilifu kwa mambo yanayowezekana kufanya uadilifu. Kwa kuwa baadhi ya watu wengi, na hili hutokea sana; wanapooa mwanamke, anamfanyia uadilifu yule mwanamke mpya tu na anamwacha mwanamke wakwanza, hataki kuongea naye, anamdhulumu na anamuona mbaya; kana kwamba ni dhalimu na ni mujrima [mwanamke huyu]. Hili halijuzu katika Uislamu. Bi mkubwa na bi mdogo wote ni sawa kunako haki. Si kwamba mwanamke akiwa mkubwa anakuwa na haki zaidi, na anakuwa mwanamke mjane ana haki zaidi ya yule mkubwa, hapana! Haki ni zile zile kwa mkubwa na bi mdogo maadamu wako katika khidima yako. Ila tu ikiwa mwanamke atachagua kubaki nawe katika hali hi [mume akawa si mwadilifu], uamuzi ni wake.
Na kutokana na hili Mtume ( صلى لله عليه وسلم ) alipotaka kumtaliki Sawdah bint
Zam’ah (radhiya Allaahu ´anha), aliomba kutoka kwa Mtume ( ( صلى لله عليه وسلم
kubaki katika khidma yake na kubaki naye na kusamehe haki yake kumpa
´Aaishah.
Mtume ( صلى لله عليه وسلم ) akamkubalia hilo. Hivyo mwanamke akiridhia
kubaki hata kama mume wake hamjamii nakadhalika, akiridhia ni haki yake.
Na ikiwa hayuko radhi kwa hilo ana haki ya kuomba wafarakane. Au ikiwa
yeye [mume] hana matamanio kwa mwanamke [huyo], asimwache akabaki
kama aliye tundikwa. Akitaka kubaki na watoto wake na nyumba yake nawe
uko katika hali hiyo, hakuna neno. Na kama hawezi, hii ni haki yake.
Ama [mwanaume] hamjali kabisa naye kashughulishwa tu na huyo
mwanamke mpya kama kwamba yule mwanamke wakwanza ni adui na
mujrima, hii ni dhuluma. Na hili ndilo alilolielezea Mtume ( ( صلى لله عليه وسلم
kuwa atakuja simu ya Qiyaamah na bega lake likiwa limepinda, hii ni fedheha
kwake kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).
Ni wajibu kwa wanaume wamche Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) katika mambo haya na wasitumie udhaifu wa wanawake kwa kuwadhulumu au kuwanyima haki zao khasa ikiwa mwanamke anakereka na hawezi kujitetea na wala hana pakukimbilia, ni wajibu kwa mwanaume kuwa naye vizuri na kumpa haki zake anazopaswa maadamu yuko katika khidma yake. Ampe haki zake. Na ajue akibaki [mwanamke] katika khidma yake na akamuacha na kumtenga na kutomjali, atahesabiwa kwa hayo siku ya Qiyaamah na atahesabika ni katika wenye kudhulumu siku ya Qiyaamah. Amuamrishe swalaha, amuamrishe kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), amkataze munkari, asitoke ila kwa adabu za Kishari´ah. Hizi ni katika haki za mke juu yake [mume]. Yeye ni mchungaji kwake.Anasema Allaah (Ta´ala):
يَا أَيُّھَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَھْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُھَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ
“Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe.” (06:66)
Miongoni mwa ahli, ni mke wako. Kama jinsi unavyoihofia nafsi yako na moto, ni wajibu vile vile kuwahofia ahali zako na moto. Anasema (Subhaanahu wa Ta´ala):
وَأْمُرْ أَھْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْھَا
“Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo.” (20:132)
Na Anasema kuhusiana na Mtume Ismaa´iyl (´alayhis-Salaam):
وَكَانَ يَأْمُرُ أَھْلَهُ بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ وَكَانَ عِندَ رَبِّهِ مَرْضِيًّا
“Na alikuwa akiwaamrisha watu [ahli] wake Swalah na Zakaah, na alikuwa mbele ya Mola Wake mwenye kuridhiwa.” (19:55)
Katika haki za mke juu ya mume wake ni kumshaji´isha katika khayr na amkataze na shari na amkanye aonapoanatoka katika utiifu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Na wala asimwachie uhuru; akamwachia akatoka apendavyo, akaongea kwenye simu na ampendae, akaenda sehemu za kipuuzi au akaenda kwenye hafla zisizo na heshima, hafla za harusi zisizo na heshima na zenye munkari - akamwacha. Yeye ni msimamizi juu yake, ni mchungaji. Na hii ni katika haki ya mke juu yake mume, kwa kuwa huyu ni mwanamke na hajui maslahi yake. Ni juu yake amsimamie na kumwangalia. Na huku ni kumkarimu.
Kwa kuwa baadhi ya watu wanafikiri kumkarimu mwanamke ni kumpa uhuru wake, huku siyo kumkarimu bali ni katika kumdhuru. Ni juu ya mwanaume kujua kuwa ni msimamizi wa mke wake. Kila mukhaalafah [kupinda] kwake, ataulizwa na Allaah kwa nini hakumuamrisha, hakumkataza, hakumuelekeza na wala hakumkataza kwa mambo yasiyompasa. Na hii ni katika ya mke juu ya mume. Haki juu yake si kumlisha na kumnywesha na kumpa mavazi tu, hizi ni haki lakini hazitoshi. Haki kubwa ni kumsimamia na kumlazimisha kumtii Allaah na kumkataza na kumuasi Allaah. Hii ni katika haki kubwa kwake [mume]. Na walii wake [mkeo] kakupa mtoto wake kama amana kwa dhima yako.
Walii wake hajui chochote kuhusiana naye. Wewe ndiye utaulizwa kuhusiana na yeye [mke] na ni amana uliopewa. Na Mtume (´alayhis-Salaam) katika Hijah [ya mwisho] ya kuaga anasema:
"Ninawausia kuwatendea wanawake khayr [wema]. Kwani wao ni wafungwa wenu." (Ibn Maajah (1851))
Mwanamke ni mfungwa kwa mume wake. Ni wajibu kwake mume kuwa naye vizuri mke huyu na mfungwa huyu, amuongeleshe vizuri, amtendee mazuri na amchukulie mke wake ni mtu mwenye hadhi na cheo chake, pozo la maisha yake na mama wa watoto wake na msimamizi wa nyumba yake. Awe naye vizuri na kumchunga vizuri, hili ndilo linalotakikana. Na wajibu mkubwa kwa mume ni kumlinda mwanamke na yasiomstahiki. Na awe msimamizi wake. Kama Alivyosema Allaah (Jalla wa ´Alaa):
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاء بِمَا فَضَّلَ للهُّ بَعْضَھُمْ عَلَى بَعْضٍ
“Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Allaah baadhi yao juu ya baadhi.” (04:34)
Kwa sababu baadhi ya wanaume hawana usimamizi, badala yake wao ndio wakwanza kumharibu mke kwa kumuwekea TV, dish nk; Haya ni madhara ewe ndugu, haya si katika mashali yake na wala katika haki za mke juu yako mume, bali ni kumuwekea madhara.
Ni wajibu kwa wanaume kuzingatia haya, na wajue kuwa mke ni amana kuanzia pale alipomuongelesha kwa walii wake. Ni wajibu kwake kumwangalia na kumkarimu na asimame kwa haki ambazo ni wajibu juu yake.
No comments:
Post a Comment