Viwanja vyote vya Lumumba jana vilionekana vimezingizwa na ulinzi mkali tokea majira ya saa sita mchana huku magari ya polisi wa kutuliza ghasya FFU wakizunguka zunguka katika maeneo yote ya mji wa Zanzibar.
Mwananchi ilishuhudia vijana mbali mbali wakiwa kando ya uwanja wa Lumumba na wengine kujibanza vipembeni wakisubiri kuingia uwanjani lakini kutokana na hali ya ulinzi kuimarishwa wananchi hao walishindwa kusogea na walikaa umbali mkubwa wa uwanja huo.
“Ulinzi naona sio wa kawaida na inaonesha hawataki watu hata kusogea umbali wa mita mia mbili, si mnaona mabunduki yake yalivyosimamishwa? Kila mmoja amebeba bunduki yake wamefunga kabisa uwanja” alisema kijana mmoja ambaye alikuwa amekaa kusubiri kuingia uwanjani.
Maelefu ya waumini walihudhuria katika viwanja vya Malindi katika manispaa ya mji wa Zanzibar ambapo viongozi wa jumuiya hiyo walikutana na kukaa msikitini na kuanza kwa sala ya alaasiri na baadae kuanza mhadhara ambapo awali baadhi ya watu walikuwa wakiogopa kusogea katika ameneo ya msikiti huo kutokana na ulinzi mkali kuka kando ya barabara zote za darajani, malindi na barabara ya kuendea Bwawani.
Akizungumza kwa njia ya simu Kamishana wa polisi Mussa Ali Musa alisema mhadhara wa Lumumba haukuweza kufanyika kwa kuwa jeshi la polisi lilitekeleza amri ya serikali ya kutoruhusu mihadhara na mikusanyiko katika kipindi hiki.
Lakini alisema kufanyika kwa mhadhara huo katika viwanja vya Malindi wanahesabu kwamba bado hapo ni maeneo ya msikiti na hivyo hawajakataza watu kuendelea na shughuli zao za kidini iwapo watadumisha amani na usalama wa nchi.
Akizungumza katika mhadhara huo Sheikh Farid Hadi Ahmed amesema jumuiya na taasisi za kidini zitaendelea kufanya mihadhara yake na wataendelea kudumisha amani kwa kuwa lengo lao ni kutoa sauti yao ambao wanadai Zanzibar huru yenye mamlaka kamili.
Sheikh Farid alitoa pongezi wa jeshi la polisi na kamishna Mussa kwa kufahamu lengo la jumuiya hizo na kueleweshana namna ya kudumisha amani na utulivu hasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wa Zanzibar wamegawanyika kutokana na misingi yao ya kivyama.
“Sisi bado tunahitaji kupata utulivu, amani na umoja na hivyo tunapaswa kuwa makini na watu ambao wamekusudia kutugawa lakini tuwe macho na watu kama hao” alitahadharisha Sheikh Farid.
Kwa upande wake Kiongozi wa Uamsho Sheikh Mselem Ally alisema wazanzibari wanadai Zanzibar yao na hivyo hakuna kitu ambacho kitawarejesha nyuma katika madai hayo hadi hapo watakapopata haki yao lakini wataendelea kudai mpaka mwisho wa nguvu zao.
“Sisi madai yetu ni kutaka Zanzibar yetu yenye hadhi na mamlaka kamili kwa hivyo haya yanayotokea ni lazima tuwe na busara na tuwe na subira katika kudai haki yetu lakini tutaendelea kudai mpaka mwisho” alisisitiza Sheikh Msellem.
Sheikh Msellem alisema wazanzibari baada ya kutenganishwa kwa miaka kadhaa sasa wanatakiwa kujua wanachodai ndnai ya muungano na wasikubali kabisa kugaiwa kwa misingi ya kivyama kwani kumekuwepo na kitendo cha makusudi cha kuwagawa waumini wa kiislamu.
Azzan Khalid Hamad ambaye alikuwa nje ya nchi kwa matibabu alisema wazanzibari wamegawanywa kiwa muda mrefu na katika hili ilitokea khitilafu na baadhi na watu kuchukua nafasi ya kutaka kuwagawa tena jambo ambalo alisema wameweza kulirekebisha.
“Wakati wenzetu watanganyika wanaendeleza nchi yao sisi tunagombanishwa lakini tunasema kwa sasa hamtugawi tena na tumeshawafahamu “ alisema na kusisitiza suala la umoja na mshikamano kati ya serikali na taasisi hizo za kidini.
Alisema taasisi hizo zina imani kubwa sana na Rais wao Dk Shein na Rais Kikwete lakini wanaamini kwamba kauli walizotoa wamezitoa kutokana na kupotoshwa na watendaji wao lakini wakaahidi kuwa na mashirikiano mema na viongozi wao kwani nia ni kuweka amani na utulivu katika nchi.
Jeshi la polisi lilionekana likiranda randa katika eneo la darajani, michenzani, na barabara za viwanja vya Malindi ili kudhibiti iwapo kutatokea vurugu lolote, lakini hata hivyo mhadhara umemalizika kwa salama bila ya kutokea fujo na wananchi wameondoka katika viwanja hivyo kwa usalama wakati jeshi hilo likiwa kando mno na wananchi waliokusanyika.
No comments:
Post a Comment