Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Tuesday, June 12, 2012

UMOJA

Sheria za Uislamu na adabu zake zinasimama juu ya msingi wa kumzingatia mtu mmoja mmoja kuwa ni sehemu isiyo tengeka na muundo wa jengo la umma. Na ni mwana familia anaye ungana na kiwiliwili cha umma, asiye pambanuka nao. Kwa hivyo basi yeye, atake asitake huchukua fungu/sehemu yake katika yale mafungu yanayo gawiwa kwenye kiwiliwili chote, kuanzia chakula, ukuaji na hisia. Na limeshakuja semezo la kimungu kulikiri weko hili, semezo ambalo halikumuelekea mtu mmoja peke yake kwa amri na makatazo. Na hakika si vinginevyo, semezo hilo limewagusa watu wote kama kundi na jamaa moja, kwa uadabishi na uongozi. Kisha katika darasa linalo tolewa kwa watu wote, mtu mmoja pia husikiliza na kunasihika. Kama hivyo ndivyo ulivyo fuatana ushereizi (uwekaji sheria) katika kitabu (Qur-ani) na Sunna (Hadithi).
“ENYI MLIO AMINI! RUKUUNI NA MSUJUDU, NA MUABUDUNI MOLA WENU MLEZI, NA TENDENI MEMA, ILI MFANIKIWE. NA FANYENI JUHUDI KWA AJILI YA ALLAH KAMA INAVYO STAHIKI JIHADI YAKE...”. [22:77-78]
Kwa hivyo basi, muislamu anapo simama mbele ya Allah ili amnong’oneze na kunyenyekea kwake, ibada hiyo haitapita ulimini kwake kama mja aliye pambanuka na ndugu zake. Bali ibada hiyo hupita ulimini mwake kama sehemu moja ya mkusanyiko ulio shikamana na kufungamana, husema: “WEWE TU TUNAKUABUDU, NA WEWE TU TUNAKUOMBA MSAADA”. [01:05] Na wala hasemi: Wewe tu ninakuabudu, na Wewe tu ninakuomba msaada.
Baada ya kuwajumuisha pamoja ndugu zake katika ibada yake binafsi, kisha ndipo humuomba Allah katika kheri zake na uwongofu wake, basi hajikhusu yeye tu kwa dua, bali hujitakia yeye rehema za Allah na watu wengine, ndipo husema: “TUONGOZE NJIA ILIYO NYOOKA, NJIA YA ULIO WANEEMESHA...”. [01:06-07]
Hakika Allah Atukukiaye hakuwaumba watu ili wapate kugawanyika na kutofautiana. Kwa yakini Yeye amewateremshia sharia ya dini moja na akawatuma mitume wake kwa kufuatana, ili wapate kuwaongoza watu wote kwenye njia moja. Na tangu azali amesha waharimishia kuifarakanisha dini na kutapanyika kuizunguka wakiwa makundi makundi yaliyo tengana. Pamoja na yote hayo ni kwamba matamanio maovu ya wanaadamu yamewasahaulisha wasiya huu mtukufu kutoka kwa Mola wao Mtukufu. Na yakawafanya waugeuze urithi huo wa kimungu, kwa ajili hiyo basi watu wakagawanyika makundi kwa makundi na kila kundi likawa linalipangia njama kundi jingine na kulingojea lifikwe na majanga.
Allah Ataadhamiaye amesema: “ENYI MITUME! KULENI VYAKULA VIZURI NA TENDENI MEMA. HAKIKA MIMI NI MJUZI WA MNAYO YATENDA. NA KWA YAKINI HUU UMMA WENU NI UMMA MMOJA, NA MIMI NI MOLA WENU MLEZI, BASI NICHENI MIMI. LAKINI WALIKATIANA JAMBO LAO MAPANDE MBALI MBALI. KILA KUNDI LIKIFURAHIA KWA WALIYO NAYO. BASI WAACHE KATIKA GHAFLA YAO KWA MUDA”. [23:51-54]
Allah Atukukiaye amebainisha ya kwamba kufuata matamanio, dhuluma, hasadi na uadui, ndio siri ya mfarakano mkubwa uliopo baina ya watu. Na lililo la haki kusemwa, ni kwamba pale elimu inapo kosa akhlaaq (tabia) na ikatengwa na ikhlaasi, elimu hiyo huwa ni balaa na janga kwa mdau wake (aliyo nayo) na kwa watu wengine pia. Watu kabla ya kujiwa na dini, walikuwa wakipotezwa na ujaahili kwenye vijia vyake finyu vihemezavyo. Na pale ilipo kuja dini na viongozi wake wakaifanyia ukiritimba na kuihodhi kama mali yao, na kisha wakazifanyia biashara elimu zake kwa ajili ya manufaa na tamaa zao, hapo ndipo makundi ya watu awaami yalipo potea na kwenda hovyo kwenye njia za dhuluma. Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akimuomba Allah amuhifadhi na elimu isiyo na manufaa, na akasema: “Hakika yule nimcheleaye mno juu yenu baada ya mnafiki, ni mtu mjuzi mno wa ulimi”. Al-Bazzaar-Allah amrehemu.
Naam, ni kweli, hakika moyo gofu huifanya elimu kuwa ndio silaha ya kufanyia ufisadi/uharibifu. Na ulimwengu wa zamani na huu wa sasa umepatwa na matatizo mengi kutokana na elimu damirishi (hilikishi) hii. Na Allah Ataadhamiaye ametuambia ya kwamba wale walio wanachuoni (maulamaa) kwa ndimi zao na si kwa nyoyo zao, hao ndio walio yaharibu na kuyavuruga mambo ya jamii ya wanaadamu. Allah Atukukiaye amesema: “AMEKUAMRISHENI DINI ILE ILE ALIYO MUUSIA NUHU NA TULIYO KUFUNULIA WEWE, NA TULIYO WAUSIA IBRAHIM NA MUSA NA ISA, KWAMBA SHIKENI DINI WALA MSIFARIKIANE KWAYO. NI MAGUMU KWA WASHIRIKINA HAYO UNAYO WAITIA . ALLAH HUMTEUA KWAKE AMTAKAYE, NA HUMWONGOA KWAKE AELEKEAYE”. Halafu akasema: “NA HAWAKUFARIKIANA ILA BAADA YA KUWAJIA ILIMU KWA SABABU YA HUSUDA ILIYO KUWA BAINA YAO...” [42:13-14]
Na akasema: “...NA WALA HAWAKUKHITALIFIANA ILA WALE WALIO PEWA KITABU HICHO BAADA YA KUWAFIKIA HOJA ZILIZO WAZI, KWA SABABU YA UHASIDI BAINA YAO...”. [02:213]
Ndugu msomaji wetu mwema-Allah akurehemu-hebu liangalie vurugu la elimu pale inapo kosa ikhlaasi kwa Allah na huruma kwa waja wa Allah, namna inavyo chochea mfarakano na kuyakata yale aliyo amrisha Allah kuungwa. Hakika ikhtilafu ya ufahamu na mgongano wa rai/mawazo/fikra, si jambo geni katika mlolongo wa maisha ya wanaadamu. Lakini ikhtilafu hiyo na mgongano huo usiwe ndio sababu halalishi ya watu kukatana pande na kuzozana. Lakini sababu ya mzozano inarejea kwenye kujiunga na vitenda kazi vingine vinavyo itumia fursa ya kugongana kwa mitazamo na fikra, ili kufikia malengo yaliyo jificha .
Na kutokea hapo ndipo utafutaji wa hakika (kweli halisia) ukageuka na kuwa ni aina ya inda (ukhalifu na ukataa haki), isiyo na mafungamano yoyote na elimu kabisa. Lau nia zingeli takasika katika kutafuta hakika na wataka hakika nao wakaja wakiwa mbali na kutafuta kuwashinda wengine, kupata umaarufu, uongozi na mali. Basi isingeli kuwepo mizozo na makindano yaliyo ijaza tarekh (historia) vunju na masaibu. Na tumemsha pata kuona mambo madogo madogo ya kipuuzi, yameleta khilafu kubwa na ikaenea, kwa sababu khilafu hiyo imekutana na manufaa ya kisiasa. Wakati ambapo khilafu imenywea katika mas-ala muhimu na zikaachwa nyajihi za uoni mambo zigote zipatakapo, kwa sababu natija ya khilafu hiyo ni ya maono matupu. Na khilafu itiayo mashaka hii ilipo kuwa ni chombo cha kuifisidi dini ya Allah na Dunia ya watu, Uislamu ukaizingatia ni sawa na mtu kujitoa Uislamuni na ni kufuru. Allah Ataadhamaiye amesema: “HAKIKA WALIO IGAWA DINI YAO NA WAKAWA MAKUNDI MAKUNDI, HUNA UKHUSIANO NAO WOWOTE. BILA YA SHAKA SHAURI YAO IKO KWA ALLAH; KISHA ATAWAAMBIA YALE WALIYO KUWA WAKIYATENDA”. [06:159]
Na Allah akawatahadharisha Waislamu dhidi ya kukhitalifiana katika dini na kurafikiana katika ufahamu wake, wakawa makundi yenye kuchinjana, na kulaaniana kwa walivyo fanya wale wa mwanzo: “WALA MSIWE KAMA WALE WALIO FARIKIANA NA KUKHITALIFIANA BAADA YA KUWAFIKIA HOJA ZILIZO WAZI. NA HAO NDIO WATAKAO KUWA NA ADHABU KUBWA. SIKU AMBAYO NYUSO ZITANAWIRI NA NYUSO ZITASAWIJIKA. AMA HAO AMBAO NYUSO ZAO ZITASAWIJIKA WATAAMBIWA: JE! MLIKUFURU BAADA YA KUAMINI KWENU? BASI ONJENI ADHABU KWA VILE MLIVYO KUWA MNAKUFURU. AMA WALE AMBAO NYUSO ZAO ZITANAWIRI WATAKUWA KATIKA REHEMA YA ALLAH. WAO HUMO WATADUMU”. [03:105-107]
Hakika kuzoeana kwa nyoyo na hisia, na kuwa moja malengo na njia, ni katika jumla ya mafundisho ya Uislamu na ni katika mambo lazima mno ya Waislamu wenye ikhlasi. Na wala hapana shaka kwamba kuungana kwa safu za Waumini na kuwa safu moja na kuwa na sauti moja, mawili hayo ndio nguzo imara/madhubuti ya kuubakisha umma wa Kiislamu na kudumu kwa dola yake na kufanikiwa kwa risala yake. Ijapo kuwa kalima ya tauhidi (LAA ILAAHA ILLAL-LAAH) ndio mlango wa Uislamu, hakika kuwa na sauti moja ndio siri ya kubakia kwake (hiyo tauhidi). Na ndio dhamana ya kwanza ili kukutana na Allah kwa uso umemetukao na kwa kitabu safi (cha amali za mja).

No comments:

Post a Comment