Idadi kadhaa ya wapiganaji dhidi ya serikali ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo, wamejisalimisha kwa vikosi vya Kimataifa
nchini humo. Vikosi vya Kimataifa vya kulinda amani nchini Kongo
vimetangza kuwa, wapiganaji hao wamejisalimisha kufuatia operesheni kali
zilizoanzishwa na majeshi hayo ya UN huko katika maeneo ya mashariki
mwa Kongo na mpakani na Rwanda. Baada ya vikosi vya Kimataifa kwa
kushirikiana na vikosi vya serikali ya Kongo kuwashinda wapiganaji wa
Harakati ya M23 hivi karibuni, vikosi hivyo vimeazimia kuwaondoa
wapiganaji wa Kihutu kutoka katika maeneo ya mashariki na katika mipaka
ya pamoja na nchi ya Rwanda. Hivi karibuni Martin Kobler, Mkuu wa
Operesheni ya Umoja wa Mataifa ya Kurejesha Amani nchini Kongo MONUSCO
amethibitisha kuanza kwa operesheni hizo kali dhidi ya waasi wa Rwanda
nchini Kongo tarehe 27 Novemba mwaka huu. Tangu mwaka 1990 mamilioni ya
watu huko mashariki mwa Kongo wamekwishapoteza maisha yao kutokana na
mapigano au njaa. Maeneo ya mashariki mwa Kongo yanatajwa kuwa na
utajiri mwingi wa dhahabu, urani, alimasi na madini ya shaba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment