Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Friday, May 18, 2012

KISIWA PANZA HATARINI KUTOWEKA (PEMBA)

KISIWA Panza kilichopo Mkanyageni mkoani Pemba chenye wakazi 600 kiko hatarini kutoweka kutokana na kumezwa na bahari.
Hali hiyo inatokana na mabadiliko makubwa ya tabia nchi yanayosababisha kina cha bahari kuongezeka na hivyo kasi ya mawimbi ya bahari kushambulia maeneo ya fukwe za kisiwa hicho.
Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Sheha Mjaja Juma, jana alithibitisha kuwapo kwa hali mbaya ya mazingira katika kisiwa hicho.
Akifafanua, alisema mabadiliko hayo ya tabia tayari yamesababisha athari katika jamii baada ya mawimbi hayo kufukua makaburi ya watu waliozikwa zaidi ya miaka 50 iliyopita.
“Kisiwa Panza kilichoko Pemba kimeanza kupata athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi kutokana na kasi ya mawimbi ya bahari kuvamia maeneo ya fukwe na kufukua makaburi,” alisema Mjaja.
Athari nyingine kwa mujibu wa Mjaja ni baadhi ya sehemu ya maji ya bahari kuingia kwenye makazi ya wananchi zaidi wakati bahari inapochafuka.
Mjaja alisema tayari Idara ya Mazingira imetoa taarifa kwa Serikali kuhusu kuwapo athari hizo ambapo tathmini zinaonesha kwamba kisiwa hicho ni miongoni mwa visiwa vilivyo hatarini kutoweka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema juhudi na mikakati ya makusudi inahitajika kuokoa kisiwa hicho kutokana na tishio la kutoweka, kutokana na kasi ya mawimbi ya baharini kushambulia baadhi ya maeneo.
Wakazi wa kisiwa Panza ni wavuvi na kutokana na hofu ya bahari kuvamia kisiwa hicho baadhi ya wananchi wameanza kukihama.
Hivi karibuni wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanaoshughulikia mradi wa mabadiliko ya tabianchi wakati wakizungumza na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika semina kuhusu mabadiliko ya tabianchi, waliitaja Panza kuwa hatarini kutoweka kutokana na kasi ya bahari kuvamia nchi kavu.
Kisiwani Pemba kuna zaidi ya visiwa vidogo 15 ambavyo vinakaliwa na watu kikiwamo cha Kojani ambacho wananchi wake wengi ni wavuvi, huku visiwa vingine 10 vikiwa havikaliwi na watu na vinatumika kwa uvuvi na utalii kikiwamo cha Misali.

No comments:

Post a Comment